
“Mke wangu ni mrembo sana!” akajisemea moyoni huku akiachia tabasamu mwanana usoni mwake.
Alichukua simu yake ili ampigie mkewe. Mtandao wa simu aliokuwa akiutumia, ulikuwa unatumika pia Kenya. Ikawa rahisi tu kupigia mkewe. Akampigia...
SASA ENDELEA...
ALIPELEKA simu yake sikioni na kusubiri majibu kutoka upande wa pili baada ya kumpigia. Haukupita muda mrefu sana, Vanessa alipokea simu ya mumewe Harrison.
“Niambie dear...” ilikuwa sauti ya Vanessa.
“Mpenzi wangu tupo Nairobi sasa, tumetua hapa kama robo saa iliyopita. Nusu saa ijayo tutaingia kwenye ndege nyingine kwa safari ya kwenda Mumbai moja kwa moja sasa,” akasema Harrison.
“Nitakukumbuka sana mpenzi wangu!”
“Nami pia mpenzi!”
“Naweza kuwa na mengi sana ya kuzungumza na wewe mpenzi lakini kwa sasa naomba nikuache. Nitakupigia nikifika.”
“Kila la kheri mpenzi wangu.”
Wakakata simu.
Ilikuwa kama ndiyo kwanza wamekutana katika uhusiano mpya kabisa. Haikuwa hivyo. Vanessa na Harrison ni mke na mume, tena wenye miaka nane ya ndoa yao. Mapenzi yao yalikuwa motomoto kama ndiyo kwanza wamekutana.
Kila mmoja alikuwa na hamu na mwenzake kila wakati. Mawazo yalikuwa kichwani mwake lakini Harrison akayafukuza haraka sana. Hakutaka kutawaliwa na mawazo juu ya mke wake.
Ilikuwa bado sana! Bado kabisa. Maana ya safari ya Mumbai haikutabirika muda wa kurudi Tanzania. Tangazo likasikika, abiria wanaosafiri na ndege hiyo, wakitumia daraja la kwanza walitakiwa kuanza kuingia kwenye ndege. Ni daraja hilo ndilo Harrison alikata tiketi yake na mdogo wake Brighton.
Wakainuka na kuingia kwenye ndege. Saa 11:15 jioni, ndege iliacha ardhi ya Jiji la Nairobi na kuinuka angani, kwa kasi ikipangua anga na kukata mawingu taratibu. Tayari Jiji la Nairobi lilikuwa linaachwa.
Harrison aliweza kuliona jiji hilo kwa sehemu kubwa sana akiwa angani. Taratibu wingu likazidi kuchukua nafasi na kumfanya asione chochote chini. Safari ya kuelekea jiji lenye vurugu nyingi, Mumbai, India ilipamba moto.
***
“Nimefurahi kuona kwamba, sehemu kubwa ya vipimo vyako vya damu na mkojo, hakuna tatizo. Kidogo mkojo wako ni mchafu lakini si tatizo kubwa sana,” alisema Dk. Roy Patankar kwa lugha ya Kiingereza akimwangalia Harrison aliyekuwa amekaa mbele yake.
“Nashukuru sana dokta,” akasema Harrison.
Sura ya Dk. Roy kidogo ilibadilika wakati akiangalia majibu ya vipimo vya MRI alivyokuwa navyo mkononi mwake. Kwa ilivyoonekana ni wazi kuwa, alikuwa na majibu yasiyofurahisha aliyotaka kumpa Harrison.
“Lakini kwenye majibu yako ya MRI, ambapo tuliangalia tatizo lako la msingi, ni kweli...utumbo wako umeathirika kwa sehemu kubwa. Mfumo mzima wa chakula hauko vizuri, lakini utakuwa sawa baada ya upasuaji kufanyika,” Dk. Roy alizungumza kwa sauti ya taratibu sana.
Akaweka lile faili mezani. Bila kuomba ruhusa, Harrison alilichukua na kuanza kupitia harakaharaka. Alikuwa amepimwa vipimo vingi sana. Wakati akiendelea kufungua ukurasa mmoja baada ya mwingine katika faili lile, alikutana na ukurasa uliokuwa na maandishi yaliyosomeka; HIV SCREENING TEST yakimaanisha, kipimo cha virusi vya ukimwi.
“Paaaaa!” moyo wa Harrison ukapiga kwa nguvu!
Akamwangalia Dk. Roy aliyekuwa kimya akimshangaa kisha akarudisha macho yake tena kwenye ule ukurasa ndani ya faili lake. Harrison akakunja uso!
***
Mwanga hafifu ulionekana vyema nje ya ndege ikiwa angani. Harrison aliweza kuona vizuri kwa sababu alikuwa ameketi siti ya dirishani. Kichwa chake kilikuwa kinawaza mambo mawili makubwa; mkewe na matibabu.
Kwa kawaida si mwoga sana wa mambo ya hospitali lakini hakuweza kuelewa ilikuwaje safari hiyo akawa mwoga kwa kiwango kile. Ni kama alikuwa akihisi kuna kitu kibaya kingetokea mbele yake.
Mapenzi juu ya mkewe yalimzidi. Ingawa kazi yake ya utangazaji wa redio na runinga ilimfanya asafiri mara kadhaa nje ya nchi kwenye mikutano, semina na mafunzo mafupi ya mambo ya habari na wakati mwingine kuripoti, hakuwahi kuwa na mashaka wala kuhisi kumkumbuka mkewe kwa kiwango kikubwa kama siku hiyo.
Harrison haraka akayahamisha macho yake. Akayatupa mbele ya siti aliyokuwa amekaa. Yaliweza kutazama vizuri sana sinema iliyokuwa mbele yake kwenye kioo kidogo mbele yake lakini haikumwingia akilini.
Mbele yake alimwona Vanessa tu. Kuna wakati Vanessa alitoka na kupishana na mwanaye mchanga, Junior. Alihisi kuwakumbuka sana.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment