Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Etoile Du Sahel ya Tunisia kwa mara ya kwanza umetoa taarifa ambayo haikuwahi kutolewa kuhusiana na mshambuliaji, Emmanuel Okwi kwa kusema alitoroka ‘kimafia’ nchini Tunisia na kusema ilikuwa kama sinema.
Etoile wamesema Okwi alizuiwa kwenda kuichezea timu ya taifa ya Uganda iliyokuwa inaivaa Liberia, lakini aliamua kutoroka bila ya taarifa yoyote kwa kiongozi au mchezaji yeyote.
Akizungumza na Championi Jumatano kutoka mjini Sousse, Tunisia jana, Ofisa Utawala wa Etoile aliyejitambulisha kwa jina moja la Amra, alisema wameshangazwa na tabia za Okwi na hawajawahi kuona.
“Ilikuwa kama sinema kabisa, kwetu kilikuwa ni kitu cha ajabu, hadi leo hapa ni gumzo kwa kuwa haijawahi kutokea. Okwi hakutakiwa kuondoka hapa Sousse na kwenda Uganda na hata alipoondoka hatukujua hadi siku iliyofuatia.
“Tulijua timu yake ina mechi muhimu, lakini alikuwa anapewa adhabu kwa kuwa akiondoka anachelewa kurudi. Hivyo kulikuwa na mjadala kati yetu na Shirikisho la Soka Uganda (Fufa), kama tungeelewana, basi angeondoka.
“Lakini akatoroka, hatukujua hata aliondoka vipi. Suala lake limefika Fifa lakini sisi sidhani kama tutakuwa tunamhitaji, ila tunasubiri mambo kadhaa yafikiwe halafu tutatoa tamko,” alisema.
Okwi ambaye alipata kibali cha kuichezea SC Villa ya Uganda kwa miezi sita kabla ya kusajili Yanga, amegoma kurejea Tunisia kwa madai ya kutolipwa mshahara wake.
Wiki iliyopita, uongozi wa Etoile ulisema haukutuma jina la Okwi kwenye Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa kuwa haukuona kama ni sahihi kwa vile wana mgogoro na Okwi.
Lakini Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, imesimamisha usajili wake Yanga kwa kuwa kuna kesi kati yake na Etoile na pia Etoile na Simba.
Okwi yuko nchini, lakini kesho atakosa mechi ya pili wakati Yanga ikisubiri taarifa kutoka Fifa na tayari TFF imeishaandika barua.
GPL
No comments:
Post a Comment