ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 29, 2014

WAZIRI MUHONGO APATA UGENI KUTOKA NCHINI UFARANSA

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiwa pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Marcel Escure (kulia kwa Waziri) pamoja na Waziri Mstaafu wa Viwanda na Nishati wa Ufaransa Bw. Eric Besson (kulia kwa Balozi), pamoja na watendaji kutoka Ubalozi wa Ufaransa na Wizara ya Nishati na Madini, wakati walipomtembelea wizarani ili kufahamu fursa za uwekezaji katika sekta hizo.
Waziri wa Nishati na Madini , Profesa Sospeter Muhongo (wa kwanza kulia) , Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Marcel Escure (kulia kwa Waziri), Waziri mstaafu wa Viwanda na Nishati kutoka nchini Ufaransa Bw. Eric Besson (kulia kwa Balozi), pamoja na mtendaji kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini, wakifurahia jambo mara baada ya kumaliza mazungumzo yaliyolenga katika kuendeleza sekta za Nishati na Madini nchini.

Na Teresia Mhagama
Balozi wa Ufaransa nchini Bw. Marcel Escure akiongozana na Waziri mstaafu wa Viwanda na Nishati kutoka nchini Ufaransa, Bw. Erick Besson wamemtembelea wizarani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ili kufahamu fursa za uwekezaji katika sekta za Nishati na Madini. Waziri huyo mstaafu wa Ufaransa, Bw.Erick Besson alikuwa akiiwakilisha kampuni ya GDF Suez ya Ufaransa. Katika suala la usimamizi wa bomba la gesi asilia, Profesa Muhongo alimweleza Bw. Besson kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) litahitaji kupata uzoefu na pengine mbia liyebobea katika usimamizi wa bomba hilo atakayeshirikiana na TPDC katika usimamizi wa bomba la gesi nchini. Kuhusu umeme. 

Waziri Muhongo alimweleza Waziri mstaafu huyo wa Ufaransa kwamba serikali inajikita katika miradi ya usambazaji umeme kwa utaratibu wa ubia au mikopo ya bei nafuu na ina mpango wa kujenga njia ya umeme ya msongo wa 400kv kuelekea ziwa Tanganyika hivyo aliikaribisha kampuni ya GDF Suez kuwekeza katika miradi hiyo ya usambazaji umeme.Aidha Profesa Muhongo alimweleza Bw. Besson kuwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linatafuta mbia watakayeshirikiana naye katika kuendesha mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe, Kiwira mkoani Mbeya hivyo kama wana nia ya kuwekeza katika eneo hilo pia wanakaribishwa kuingia katika ushindani wa kupata nafasi hiyo.

Naye Waziri mstaafu wa Viwanda na Nishati kutoka nchini Ufaransa, Bw. Besson alimshukuru Profesa Muhongo kwa taarifa nzuri kuhusu fursa za uwekezaji nchini na ameahidi kupata taarifa zaidi za uwekezaji katika mashirika ya TPDC, STAMICO na TANESCO ili kuona jinsi kampuni ya Suez itakavyoshirikiana na mashirika hayo katika kuendeleza sekta za Nishati na Madini.

No comments: