Wengi wamuita mbunge wa Mahakama
Wengine wasema chama hakitamwamini
Kigoma wamtetea, Chadema: Tunasubiri
Wametoa maoni hayo baaada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kupitia kwa Jaji John Utamwa juzi kukizuia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutojadili uanachama wa Zitto hadi maombi yake yatakaposikilizwa.
Maombi hayo ni vikao vya Chadema kutojadili uanachama wake, Katibu Mkuu wa Chadema kumpatia mwenendo wa kikao cha Kamati Kuu cha Novemba 22, mwaka jana kilichomvua wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu na Baraza Kuu kuamua rufani yake.
Ramadhani Juma, mkazi wa Arusha, alisema kumekuwa na kawaida kwa mahakama kulinda wabunge waliokataliwa na vyama vyao bila kujali Katiba na sheria inayovipa vyama vya siasa haki ya kuwakataa wanachama wao.
“Vyama vinawakataa, lakini mahakama inawakingia kifua kuwapa haki ya kuwa wabunge, hili ni jambo baya maana anabaki kuwa Mbunge wa mahakama ambaye hana nguvu zozote kwa sababu chama na wanachama hawamtaki,” alisema Ramadhani.
Alisema Zitto siyo wa kwanza ubunge wake kushikiliwa na mahakama na kwamba vyama vinanyimwa haki ya kuwadhibiti wanachama wanaokwenda kinyume na taratibu.
Alisema kuna haja rasimu ya katiba mpya kuweka utaratibu ili mahakama iheshimu maamuzi ya vyama vya siasa pindi wanapomvua uanachama mbunge badala ya kuwalinda.
Samuel Mollel, mkazi wa Ngulelo, jijini humo, alisema hata kama mahakama imezuia Zitto asijadiliwe, chama kisimtambue.
MAONI YA KIGOMA
Wakazi wa mji wa Kigoma walimtetea Zitto huku Abdalah Mussa, akisema Mbunge huyo wataendelea kumuunga mkono kwa kuwa aliwatetea wakati wa oparesheni Kimbunga ya kusaka wahamiaji haramu katika mikoa kadhaa nchini.
Alisema baada ya raia kukamatwa na kusumbuliwa, Zitto alikwenda Kigoma na kuwatetea hivyo hawawezi kutomuunga mkono mtu anayewajali kwa sababu wangepata tabu sana.
“Sisi kama wanachama wa Chadema Mkoa wa Kigoma tutashikamana na Zitto, tutamuunga mkono kwa hali na mali na kwa vyovyote, Zitto akihamia chama kingine kazi tukakayo kuwanayo watu wa Kigoma ni kuhakikisha kambi yote ya Zitto hawabaki Chadema kwa sababu amechaguliwa na wananchi na wanaosema ni mbunge wa mahakama wanajidanganya,” alisema.
Wazee kadhaa mjini Kigoma wamemtaka Zitto aende nyumbani ili aombewe dua ili atakaye mnyoshea kidole ang’oke yeye.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Msafiri Wamalwa, alisema hatua aliyoichukua Zitto kwenda mahakamani ni nzuri kwa sababu anataka demokrasia ya kweli, hivyo viongozi washirikiane ili kukijenga chama hasa wakati huu wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
MAONI YA TANGA
Mwanachama wa Chadema jijini Tanga, Johnson Mbwambo, alisema kitendo cha Zitto kukimbilia mahakamani ni kuongeza nguvu za utovu wa nidhamu na kupoteza sifa za uanachama wa Chadema kwani ameonyesha ubabe kwa kuvutana na chama chake.
“Zitto ni mkosaji na aliwajibika kuvuliwa nyadhifa zake na uanachama pia, kwenda mahakamani ni kuonyesha ubabe na kutaka kuvutana na chama jambo ambalo halitamsaidia chochote,” alisema Mbwambo.
Mbwambo alishauri uongozi wa Chadema kuangalia sheria na katiba yake na kuona kama kuna ukiukwaji na kwamba kinachofuata ni kuchukua hatua kwa mujibu wa mwongozo wa kanuni, taratibu zake na sheria zichukuliwe bila huruma.
-Elizabeth Kilindi alieleza kuwa hatua ya Zitto kukifikisha chama mahakamani ni kulewa umaarufu na kudai kuwa alichotakiwa ni kuomba radhi na kusikiliza matakwa ya wana-Chadema badala ya kujenga misingi ya mapinduzi ambayo imemuondolea heshima.
M
AONI IRINGA
Mhadhiri Msaidizi wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Iringa (IoU), zamani kikitambuliwa kama Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini, Emanuel Damalo, alisema uamuzi wa Kabwe kukisulubu
chama chake bila ya kujali maslahi ya wengi ni ishara kwamba anatumiwa na upande fulani wa wanasiasa wenye uchu wa madaraka wa kutwaa nafasi muhimu.
“Alichokifanya Zitto Kabwe ni kuchagua kaburi badala ya giza na kimsingi hili litampa picha halisi baadae, likimwonyesha upofu wake wa kisiasa kwa sababu hakutazama maslahi ya walio wengi na hata akiendelea kung’ang’ania kubakiziwa uanachama wake Chadema atakuwa amejiangamiza mwenyewe,” alisema Damalo.
Delivina Sanga, mwanaharakati na mkazi wa Chaugingi mkoani Njombe, alisema hatua ya mwanasiasa huyo kijana kujaribu kufifisha nguvu za upinzani kupitia kivuli cha mabadiliko ndani ya chama chake hakutaweza kubadili mitazamo na maisha ya Watanzania, isipokuwa kuondosha mizania ya ushindani wa kisiasa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) Mkoani Iringa, Rwezaura Kaijage, alisema inapotokea hali ya mkanganyiko baina ya wanasiasa na vyama vyao au dhidi ya serikali yao kutokana na maslahi binafsi, umma huwa unasikiliza sauti ya mantiki na si hisia.
“Watanzania wanajua nani mbaya na nani ni mzuri, katika siasa za sasa hapa Tanzania wanawajua wanaotumika kuwadidimiza na wanaosimama kupaza sauti za wasio na sauti. Sauti ya mantiki ni zaidi ya hisia,” alisisitiza Kaijage.
DODOMA
Mwanachama wa Chadema mkoani Dodoma, Asha Juma, alisema uamuzi wa Zitto kwenda mahakamani ni sahihi kwani baada ya kuona haki yake katika chama haipo ndio maana aliamua kufanya hivyo, lakini pia hatua hiyo itamfanya wananchi kutokuwa na imani naye.
Alisema baadhi ya viongozi wa Chadema walishamhukumu kabla vikao vya juu kukutana kutoa maamuzi dhidi ya uanachama wake hivyo hakuna na jingine ila kutafuta haki mahakamni.
Naye Mwenyekiti wa Jopo la Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paulo Loisulie, alisema kuwa Zitto angefanya subira angepigania demokrasia ndani na angekuwa mtu mkubwa sana ndani ya chama hicho hapo baadaye.
Alisema kuwa kwa sababu uvumilivu umemshinda na kukishtaki chama mahakamani, tayari ameikosa hiyo nafasi.
“Hata Rais Kikwete kuna wakati alivumilia kwenye chama, lakini sasa kwa hili la juzi kwa vyovyote vile ni kwamba Zitto hataweza kuaminika ndani ya chama chake,” alisema mhadhiri huyo.
Aidha alibainisha kuwa Zitto ataendelea kuwa mbunge wa mahakama mpaka hapo itakapofikia mwisho wake 2015 ndipo atakapoangalia nafasi zingine, lakini hataaminika tena kama ilivyokuwa awali.
“Licha ya hivyo hata baadaye kama akianzisha chama ajue kuwa ameshapoteza idadi kubwa ya watu kwani kuna watu wataendelea kumkubali na wengine watakuwa wamekatishwa tamaa,” alisema.
Naye mwanachama mwingine, George Mbara, alisema kuwa hatma ya Zitto Chadema ni kufukuzwa tu kutokana na kukimbilia mahakamani.
.MAONI YA KILIMANJARO
“Zito anaonekana ni mtu mwenye kutaka madaraka, ikumbukwe kwamba alishawahi kutaka kugombea urais na wakati fulani alikaririwa akisema kuwa hatagombea tena ubunge na baadaye akarudi nyuma akatangaza atarejea katika ubunge wake,” alisema kiongozi na mwanaharakati katika Chama Cha Mapinduzi na kuongeza:
Profesa William Makundi, mwanazuoni katika sayansi Kusini mwa Afrika, alisema Chadema tayari kimejipambanua hakitaweza kufanya kazi tena na Zitto kutokana na hali iliyojitokeza na kwamba ni vyema Kamati Kuu ya chama hicho ikakaa na kulitazama upya suala hilo.
“Wakisimamia msimamo wao (Chadema) dhidi yake labda asubiri katiba mpya apitie fursa ya mgombea binafsi kwa sababu anayogombana nayo ni taasisi ambayo inaweza kumfanya asiweze kuchaguliwa tena, lakini ukweli utabaki kwamba amejiharibia kisiasa,” alisema Profesa Makundi.
MAONI YA MOROGORO
Kaimu Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Boniface Ngonyani, alisema maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu yanaonyesha ni muendelezo wa maamuzi ya wabunge wengine wawili Hamad Rashid Mohamed (CUF) na David Kafulila(NCCR- Mageuzi) ambao kwa pamoja walifukuzwa na vyama vyao kwa kile kinachoelezwa kuwa ni usaliti.
Alisema Chadema Mkoa wa Morogoro bado inaendelea kuheshimu maamuzi ya Kamati Kuu na kueleza kuwa kwa sasa wanatambua kuwa Zitto ni Mbunge wa Mahakama kwa kuwa chama hakina imani naye tena.
“Sawa kaenda mahakamani kufuata haki kama alivyodai mwenyewe, maamuzi yametolewa na tunayaheshimu, lakini atambue huko nako pia atagonga mwamba tu, hatuwezi kukubali mtu anayetuvuruga kwa kutaka madaraka,” alisema Ngonyani.
Naye Aron Shembuta, kada wa Chadema mkoa wa Morogoro, alisema wanaheshimu maamuzi ya mahakama, lakini haitaweza kumsaidia Zitto kwani haitajiki tena ndani ya chama baada ya kubainika ni msaliti.
“Huwezi kuwapeleka viongozi wetu mahakamani halafu uendelee kuwa kwenye chama. Huko kwenye Baraza Kuu anapokutaka kamwe asitegemee maamuzi tofauti na Kamati Kuu,” alisema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo na Ukiziwi Tanzania, Henry Mtasiwa, aliwataka waasisi wa chama hicho kuwakutanisha Zitto na uongozi wa juu wa Chadema kumaliza tofauti kwani kumfukuza siyo suluhisho.
MAONI YA BUKOBA
Mwanachama wa Chadema mkazi wa Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Delifinus Rwabigene, alisema kuwa wanachama wanauchukulia ushindi wa Zitto mahakamani kuwa hautampeleka mbali kwa kuwa ni wa kulinda ubunge maana kama angefukuzwa uanachama angepoteza ubunge.
“Hata kama mahakama imeamua hivyo, lakini kwa wanachama tunachukulia kama msaliti, tumekwishakosa imani naye akae pembeni apishe watu wengine wenye mapenzi mema na chama ili chama kiweze kusonga mbele” alisema Rwabigene.
Alisema kuondoka kwa Zitto katika chama hicho hakuwezi kuwaathiri chochote na kuwa kama kuna wanachama wengine kama yeye inabidi waondolewe mapema kabla ya chaguzi za serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao.
Alisema Wanachadema wa Bukoba wanaunga mkono maamuzi ya uongozi wa ngazi za juu za chama hicho wa kumwondoa Zitto katika uongozi na kuwa wasiokubaliana na maamuzi hayo nao ni wasaliti.
Victor Kato, mjumbe wa mtaa wa National Housing katika Kata ya Rwamishenye kupitia Chadema, alisema maamuzi ya mahakama kwamba Zitto asijadiliwe hayatamsaidia.
MAONI YA MWANZA
“Ninachoweza kusema ni kwamba pamoja na Zitto kukiuka katiba ya chama na kukimbilia mahakamani, badala ya suala hilo kujadiliwa na vikao ndani ya Chadema, ninadhani kuna haja sheria zitazamwe upya ili masuala ya vyama vya siasa yaamuliwe na vyama vyenyewe badala ya mahakama,” alisema kiongozi wa M4C Kanda ya Ziwa, Tungaraza Njugu.
Kwa mujibu wa Njugu, ni kosa kesi za kisiasa kusajili na kusikilizwa na mahakama kwa vile waamuzi wa kesi hizo wanapaswa kuwa ni vyama husika.
Njugu alishauri sheria za kimahakama zifanyiwe marekebisho ili zisiingilie uhuru na kazi za vyama vya siasa. “Kimsingi ni kwamba Zitto ameyakoroga, sijui ataishije kisiasa baada ya ubunge wake wa mahakamani kwisha.
Kwa mfano, hawezi kujiunga na CCM kwa vile amekuwa akiwatuhumu kuwa ni chama cha mafisadi na wala hawezi kwenda NCCR-Mageuzi kwakuwa alishawakoroga miaka kadhaa iliyopita baada ya kutofautiana na Mbatia,” alisema Omoro Ontiti, mkazi wa Mbatini jijini Mwanza.
Onditi ambaye ni mwanachama wa Chadema, alimlaumu Zitto kufikisha kwenda mahakamani badala ya kutumia taratibu za chama kwa mujibu wa katiba yake.
“Mimi ninadhani mwisho wa historia ya Zitto utawadia baada ya ubunge wake wa kimahakama, kwa sababu hataaminika ndani ya chama kingine chochote cha siasa nchini,” alisema.
MAONI IRINGA
Haji Abdul, mfanyabiashara katika Manispaa ya Iringa, Zitto ni mwanasiasa mwenye ushawishi, lakini kwa mwenendo wake kwa sasa unaonyesha wazi kwamba anataka kukihujumu chama chake.
“Kimsingi mimi namsapoti kauli aliyoitoa mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei, kuwa atafute chama kingine cha siasa,”alisema.
Abdul na kusema kuwa Zitto asingekimbilia mahakamani kwa kuwa Chadema ndicho kilichompatia ubunge na siyo mahakama.
Nae Jackson Kalole, mkazi wa Manispaa ya Iringa, alisema kuwa imeonekana Zitto amekuwa akilalamikiwa kutoshiriki shughuli za chama muda mrefu, ingawa amekuwa kimya kujibu.
“Kotokana na kauli yake ya kusema kuwa chama pinzani kikitawala wananchi hawatapona, tafsiri yake ni kuwa CCM kiendelee kutawala,” alisema Kalole.
DK. BANA, BASHIRU
Wanataaluma wawili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamemwelezea Zitto kuwa maisha yake ya kisiasa ndani ya chama hicho yatakufa, uadui utakuwa mkubwa baina yake na viongozi wengine huku wakikishauri chama hicho kufanya mazungumzo ya kumaliza mgogoro huo. Dk. Benson Bana, alisema haamini kama Zitto atakuwa na maisha ndani ya Chadema kutokana na uadui kuzidi kuwa mkubwa na kuwa tofauti ndani ya chama hicho zinaweza kumalizika pindi Baraza Kuu na Kamati Kuu vitakapokutana.
Aliongeza kuwa Chadema kina viongozi makini wengi ambao wanaweza kuziba nafasi aliyoiacha Zitto, lakini alieleza kuwa bado muda upo wa kutatua matatizo hayo.
Dk. Bana alisema Chadema wanaweza kulijadili suala hilo nje ya kanuni na sheria za chama kwa manufaa ya uhai wa chama na uhai wa mwanachama.
Bashiru Ally, alisema vyama vya siasa nchini vinatakiwa kujijenga kidemokrasia zaidi kwa kutafuta mwafaka kuliko kukimbilia mahakamani.
Alisema mahakama kuingia katika kutoa maamuzi katika vyama vya siasa siyo ishara nzuri kwa chama chochote kwa kuwa kitakuwa kimeonyesha kushindwa kujisimamia chenyewe.
“ David Kafulila alikimbilia mahakamani, Hamad Rashid alikimbilia mahakamani, naye Zitto amekimbilia mahakamani ki ukweli haioneshi picha nzuri kwa vyama vya siasa,” alisema.
CHADEMA: TANASUBIRI
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, aliutaka umma kuvuta subira, kwani kesi ya msingi bado haijaisha na kwamba, uamuzi uliotolewa na mahakama juzi ulihusu zuio kwa chama kujadili uanachama wa Zitto pekee.
Hivyo, alisema mawakili wa Chadema wataendelea kusimamia kesi hiyo na kwamba, katika kipindi hiki, azimio la Kamati Kuu (CC) linalowataka wana Chadema kutompa Zitto ushirikiano katika mikutano atakayoifanya kwa jina la Chadema, bado haujabadilika.
Alisema katika kikao chake kilichofikia azimio hilo, CC haikuwa na ajenda hiyo peke yake, bali zilikuwa nyingi na kwamba, chama wakati wowote kitaeleza mambo mengine muhimu, yakiwamo maazimio mengine sita yaliyofikiwa na CC kuhusu maudhui na mchakato wa katiba mpya.
Imeandikwa na Godfrey Mushi, Iringa; Cynthia Mwilolezi, Arusha; Dege Masoli, Tanga; Augusta Njoji, Dodoma;
Charles Lyimo, Moshi; Ashton Balaigwa, Morogoro; Lilian Lugakingira Bukoba; Juma Ng’oko, Mwanza; Jacton Ngelly, Kigoma; Gwamaka Alipipi na Muhimu Said, Dar; Lilian Lugakingira, Bukoba na George Tarimo, Iringa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment