Mgombea Ubunge Jimbo la Kalenga kupitia Chadema, Grace Tendega akipungia mikono wananchi wakati msafara wa chama hicho ulipokuwa ukitoka Iringa mjini kuelekea katika jimbo hilo ulipofanya mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika kwenye Uwanja wa Kalenga, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Iringa. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbroad Slaa jana alizindua kampeni za kumnadi mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga, Grace Tendega, huku akionya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuongezewa posho.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Kalenga, Dk Slaa alisema chama hicho kimemtuma Mwenyekiti wake wa Taifa, Freeman Mbowe kuhakikisha posho haziongezwi.
“Naomba kabla ya kuendelea nitoe salamu za Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amebaki Dodoma kutokana na kuteuliwa kwenye Kamati ya Uongozi inayoshughulikia masuala yote ya Bunge la Katiba. Kamati ile inashughulikia masuala yote likiwamo la posho na tumemwambia mwenyekiti wetu ahakikishe posho haziongezwi,”alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Yeye ndani ya kamati yupo peke yake na wengine wote ni CCM, tutahakikisha anawashinda, wakimshinda sisi tutatoka nje,”alisema.
Katika kampeni hizo, Dk Slaa alisisitiza kampeni hizo za ubunge zifanywe kwa amani na kwamba chama chake kitakuwa cha mwisho kuona damu ya wananchi wa Kalenga inamwagika.
Alisema katika kampeni nyingi zilizopita Chadema imekuwa ikisingiziwa kuwa ndiyo imekuwa chanzo cha vurugu, lakini ukweli ni kwamba hizo ni propaganda za chama tawala.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Kimila wa Kabila la Wahehe (Mtwa) ambaye alihudhuria kampeni hizo, Abdul Sapi Mkwawa alimtaka mgombea wa chama hicho, Grace Tendega kufanya kampeni zake kwa amani huku akisisitiza kuwa hilo ndilo ombi lake.
“Mimi nimeitwa na nimekuja sababu mimi ni kiongozi wa watu wote, ninatoa baraka zote kwa dada yangu Grace, ninamwombea kwa Mungu aendelee na kampeni zake kwa amani hadi atakapomaliza,”alisema Sapi.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Mkoa wa Iringa, Chiku Abwao aliwataka wakazi wa Jimbo la Kalenga kutokubali kununulika na kusisitiza kuwa wakati umefika wa kujikomboa kutoka kwenye ukoloni wa CCM.
Alisema atakuwa wa kwanza kushangaa kama wananchi hao watamchagua kiongozi ambaye hajui matatizo ya Kalenga kwa kuwa muda mwingi ameishi nje ya Kalenga.
Naye Mgombea wa Jimbo hilo, Grace aliwaomba wakazi wa jimbo hilo wamchague ili aende bungeni kushughulikia matatizo yao.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment