‘Anayeona posho haimtoshi afungashe virago’
Kwa ufupi
Hoja ya kutaka nyongeza ya posho iliibuliwa na
wajumbe wawili ambao pia ni wabunge wa CCM, Richard Ndasa (Sumve) na
Suleiman Nchambi (Kishapu).
Dodoma. Wizara ya Fedha
imepigilia msumari maombi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya
kutaka waongezewe posho na kusema anayeona ameacha kazi inayomlipa zaidi
kwenda bungeni afungashe virago na kuondoka.
Msimamo huo umekuja
siku moja tu baada ya gazeti hili kudokeza kuwa madai ya wajumbe wa
bunge hilo kutaka waongezewe posho kutoka Sh300,000 za sasa kwa siku,
yamegonga mwamba baada ya kamati iliyoteuliwa kuchunguza uhalali wake
kusema kiwango hicho kinatosha.
Mwenyekiti wa muda wa bunge hilo,
Pandu Kificho alisema jana bila kutaja viwango, kuwa ripoti ya kamati
hiyo imewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi.
Madai ya
wajumbe kutaka waongezewe posho, yamechafua hali ya hewa ndani na nje ya
Bunge, huku baadhi ya wananchi wakipaza sauti zao na kumsihi Rais
Kikwete alivunje bunge hilo iwapo wajumbe watashikilia msimamo wa kutaka
nyongeza ya posho.
Jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
alisema wanaoshiriki kutunga Katiba ni Watanzania na siyo wataalamu
washauri waliokodiwa kutoka nje.
Alisema kwa msingi huo, Serikali ilitarajia kuwaona watu hao wakitanguliza uzalendo zaidi badala ya kudai malipo manono.
“Katika
kutengeneza Katiba hii, hatujakodi consultants (wataalamu washauri)
kutoka Uingereza, Marekani, Kenya, Uganda wala nchi nyingine yoyote…
Hawa ni Watanzania na kazi wanayoifanya ni yao,” alisema.
“Wangekuwa
wataalamu wa kukodi wangeweza kudai malipo hayo, lakini hapa ni
tofauti... wanafanya kazi yao na kila mtu anafanya kazi yake na anapaswa
kujivunia kushiriki katika tendo hili la kihistoria kwa kutanguliza
uzalendo,” alisema.
Nchemba alisema anazielewa hoja za baadhi ya
wajumbe walioibua suala la posho, lakini kwa mtazamo wake, hoja hiyo
hata kama ingekuwa na mashiko kiasi gani, imewasilishwa wakati usiokuwa
mwafaka. Alisema wapo makandarasi na wazabuni waliotoa huduma kwenye
taasisi mbalimbali za umma lakini hawajalipwa.
Alisema kwa
kawaida, Februari ni mwezi mbaya kwa kuwa baadhi ya wilaya zina historia
ya kukumbwa na uhaba wa chakula hivyo kuhitaji fedha nyingi za Serikali
ili kuokoa maisha ya watu katika maeneo hayo.
Pia alisema si
wakati mwafaka wa kudai nyongeza hiyo hasa ikizingatiwa kuwa kuna walimu
wapya 30,000 nchini kote ambao hawajapangiwa vituo kutokana na
kukosekana kwa fedha za kulipa stahiki zao.
Nchemba alisema mbali
na walimu hao wapya kutokupangiwa vituo, walimu wengine wanadai
malimbikizo ya fedha zao na kwamba hawajalipwa kutokana na ufinyu wa
bajeti serikalini.
“Siku zote ukweli unauma. Nasema kama kuna
mjumbe ambaye anaona huko alikokuwa kabla ya kuteuliwa alikuwa anapata
pesa zaidi kuliko hii, basi kwa heshima afungashe virago na kuondoka,”
alisema.
Via Mwananchi
1 comment:
Now you're talking!!!
Post a Comment