Mtoto Hamis Liguya, 13, akiwa Hospitali ya Ganga, Combatore, Tamil Nadu nchini India.
Stori: Imelda Mtema, India
HATIMAYE mtoto mwenye uvimbe wa ajabu, Hamis Liguya, 13, leo anatarajiwa kufanyiwa upasuaji kisha kukatwa mguu katika Hospitali ya Ganga, Combatore, Tamil Nadu nchini India.
Hamis Liguya akiwa na madaktari.
Hospitali hiyo ni maalum kwa ajili ya watu waliopata ajali na matatizo mbalimbali ya mifupa.
Kwa mujibu wa daktari atakayemfanyia upasuaji huo, Raja Sabapath ambaye ni mtaalam wa upasuaji na mifupa, ugonjwa unaomsumbua kitaalamu unaitwa Plexiform neurofibromatosis na amesema kutokana na uzito wa tatizo hilo, upasuaji utadumu kwa zaidi ya saa nne.
Akizungumzia zaidi tatizo hilo, daktari huyo alisema kwa kuwa mtoto huyo hakuwahishwa mapema hospitali, watalazimika kumkata mguu mmoja kwenye goti kisha kukwangua nyama katika sehemu ya paja ili kupunguza uvimbe.
“Tukishamkata mguu, tutapunguza uvimbe katika paja. Baada ya zoezi hilo kukamilika, atakuwa katika uangalizi maalum kwa takriban siku zisizopungua ishirini ili kuweza kumuangalia maendeleo yake, tukijiridhisha anaendelea vizuri baadaye tutamwekea mguu wa bandia na kumpa magongo ya kutembelea,” alisema daktari huyo.
Dokta Sabapath amesema mbali na tatizo hilo la uvimbe wa mguuni, wamebaini pia ana uvimbe mwingine kwenye uti wa mgongo ambao ulisababishwa na uvimbe huo wa mguuni.
Uvimbe huo ndiyo uliochangia kwa kiasi kikubwa mtoto huyo ashindwe kutembea ambapo daktari amesema watashindwa kuufanyia upasuaji kwa kuwa tayari umeshakuwa mkubwa.
Mtoto huyo ambaye ameteseka kwa muda mrefu na ugonjwa huo, aliondoka nchini Tanzania Februari 15, mwaka huu akiwa ameambatana na baba yake mzazi, Hamis Liguya na Mwandishi wa Kampuni ya Global Publishers, Imelda Mtema.
Mtoto akiwa hospitali.
Kampuni ya Global Publishers Ltd inayozalisha Magazeti ya Ijumaa Wikienda, Uwazi, Risasi, Amani, Ijumaa na Championi, ndiyo ilikuwa ya kwanza kuripoti habari za ugonjwa wa mtoto huyo ndipo wakajitokeza wadau na wananchi wengine kumsaidia fedha ambazo zilimwezesha kuja nchini humu kutibiwa.
Aidha, Mtangazaji wa Kipindi cha Mimi na Tanzania, Hoyce Temu anastahili pongezi kwani alijitoa kwa kiasi kikubwa kumtangaza katika kipindi chake.
Credit:GPL
2 comments:
Kuna habari iliandikwa kuwa alifariki,bado yu hai?
Hivi wewe unayeulizia uhai unamaanisha nini? Hapa sio mahali pake na acha kuchanganya habari!
Post a Comment