Mgogoro Manchester United
By Israel Saria
*Robin van Persie awachana wenzake
*Adai wanamziba nafasi yake dimbani
MPACHIKA mabao wa Manchester United, Robin van Persie ‘RVP’ amewachana wachezaji wenzake kwamba ndio wanaomkwamisha kufunga mabao.
Akizungumzia hali ya timu hiyo inayosuasua kwenye mashindano mawili ilimobaki, RVP alisema inamuwia shida kupata mipira kwa sababu wenzake wanamwingilia kwenye eneo lake.
Kwa namna ya pekee Mholanzi huyo aliyetoka Arsenal na anayedaiwa kutaka kurudi msimu ujao, anazungumzia mechi dhidi ya Olympiakos jijini Athens ambako walilambwa 2-0.
RVP aliwananga wenzake kupitia Kituo cha Televisheni cha NOS cha Uholanzi, akisema amekuwa akijaribu kujipanga kivingine lakini anashindwa.
“Wakati mwingine wachezaji wetu wengine wanahodhi nafasi ambazo nataka kuchezea. Wakifanya hivyo huniwia ngumu kuingia humo kwa hiyo wananilazimisha kutafuta sehemu nyingine kutegemeana na wapi wameng’ang’ania. Bahati mbaya sana ni kwamba wanakuwa wanacheza kwenye eneo langu mara kwa mara na hii ni aibu na fedheha kubwa,” anasema Mdachi huyo.
Van Persie anasema hayo baada ya kocha wao, David Moyes kusema Man U walionesha mchezo mbovu zaidi ya yote waliyopata kucheza Ulaya ambapo ni shuti moja tu lililenga goli katika dakika zote 90.
Van Persie mwenyewe alipaisha mpira ambao alikuwa wazi kufunga akiwa analitazama goli kutoka yadi saba tu.
“Niliharakisha mno kupiga shuti lile. Ni fedheha pia kwa sababu kwa kawaida sipati nafasi kama zile mara nyingi kwa hiyo inapotokea unatakiwa kufunga,” akasema RVP mwenye umri wa miaka 30.
Haijajulikana ni wachezaji gani hasa anawazungumzia RVP kwamba wanakaa kwenye eneo lake na kumkosesha kufunga mabao ambayo Moyes ana kiu nayo sana wakati huu katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Man U wameshatupwa nje ya Kombe la Ligi na Kombe la Fa, ambapo Moyes ameweka rekodi nyingi mpya na mbaya kwa miaka mingi.
Hata hivyo, Man U hawakupoteza mechi dhidi ya Olympiakos kwa sababu ya wachezaji wengine kuingia kwenye eneo la RVP, kwani mpira haukufika mara nyingi hata kwenye eneo hilo, ikionekana kiungo na ulinzi kulikuwa na matatizo makubwa.
Inadhaniwa kwamba mabadiliko makubwa yatafanywa Old Trafford, ambapo mawazo ya watu yamegawanyika kati ya kuondoa wachezaji kadhaa au kuachana na kocha ambaye inaelekea viatu vya Alex Ferguson, vinambana, kama siyo kumpwaya.
No comments:
Post a Comment