ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 23, 2014

Vita ya uenyekiti Bunge la Katiba

Andrew Chenge na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambao wametajwa kutaka kuwania nafasi ya uenyekiti wa Bunge la Katiba wakipeana mikono siku za hivi karibuni.

Dodoma. Kadiri siku zinavyosogelea uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, ndivyo mpasuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unavyozidi, kutokana na kuwapo kwa makundi mawili yanayojipanga kusimamisha wagombea na ambayo yameanza kuendesha kampeni kuchafuana.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa makundi hayo ni yale yanayomsaidia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambao wametajwa kutaka kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, wakati Chenge akiwa hayuko tayari kuthibitisha nia yake hiyo, Sitta hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo. Lakini habari zinasema vigogo hao wameshajipanga kwa ajili ya mbio hizo za uchaguzi na sasa wanatafuta watu wa kuwasaidia.
Makundi hayo yalianza wakati wa kikao cha ndani cha CCM kilichofanyika mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, ambako habari zilisema, baada ya chama kumteua Pandu Ameir Kificho kuwania nafasi ya mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba, mmoja wa wajumbe wa kikao hicho walimpendekeza Chenge kuwa mwenyekiti wa kudumu wa bunge hilo.
“Hapo ndipo mgogoro ulipoanza. Kwanza tulimkubali Kificho ili kupunguza wingu la ushindani kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu. Lakini wajumbe tulimkataa Chenge kwa hoja nzito na mwenyekiti alikubali na kuamua kuwa watu wakagombee bungeni.”
Tuhuma dhidi ya Chenge
Baadhi ya wabunge wa CCM wamesema ni ukweli ulio wazi kwamba Sitta na Chenge ndio wanaofaa kuwania nafasi hiyo, lakini mchuano utakuwa mkali kutokana na kila mmoja kuwa na ushawishi wa aina yake kwa wajumbe ambao ndio watakaopiga kura kumchagua mwenyekiti.
 “Wakati wa kuapa, wajumbe watatakiwa kushika Biblia au Qur’an. Ila tusema ukweli, unawezaje kufanya kiapo cha utii mbele ya mwenyekiti ambaye uadilifu wake unatia shaka? Alihoji mmoja wa wajumbe wanaomuungano mkono Sitta.
Mjumbe mwingine alisema Chenge hazuiwi kugombea, lakini ajiandae kujibu maswali makuu matatu, moja likihoji uadilifu wake wakati kuna mikataba mingi ya wawekezaji kwenye kampuni za madini iliyoshuhudiwa na yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni mibovu.
“Pia tutamtaka aeleze kwa nini alikubali Uenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri kwa uteuzi wa Spika, wakati kanuni zinasema wenyeviti wachaguliwe na wabunge wenyewe,” alisema mjumbe huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Kauli ya Chenge
Chenge mwenyewe amepuuza tuhuma hizo akisema kuwa ni za watu wasiopenda kuelewa.
Pinda aliwaasa wanachama wa CCM waache kupanga nani agombee na nani asigombee na kufafanua kuwa hali hiyo hujenga makundi ndani ya chama hicho.
“Tunahitaji kupata viongozi kwa kuzingatia umoja wetu na mshikamano miongoni mwa wanachama. CCM ikiwa imara itaunda Serikali imara. Chama kikiwa dhaifu ni wazi kuwa hata Serikali yake nayo itakuwa dhaifu,” alisema.
Mwananchi

No comments: