ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 10, 2014

Waliotangaza nia CCM kikaangoni

Akizungumzia suala hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula alisema mwanachama yeyote wa chama hicho hatakiwi kutoa michango, misaada, zawadi kwa mtu au katika shughuli yoyote bila kupata ridhaa ya uongozi.

Dar es Salaam. Baadhi ya makada wa CCM ambao wataitwa mbele ya Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho, wanakabiliwa na shtaka la kutoa rushwa kwa lengo la kushawishi kukubaliwa kwao, Mwananchi limebaini.
Makada hao ni wale wanaodaiwa kuwa katika harakati za kuwania urais wa 2015, hatua ambayo imekigawa chama hicho katika makundi yasiyo rasmi ya yanayowaunga mkono wagombea hao.
Tovuti hili imedokezwa kuwa mgombea mmoja wa nafasi hiyo mwenye ushawishi mkubwa aligawa fedha Sh200,000 zilizoambatana na kadi za kuwatakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya 2014 idadi kubwa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM.
Kadhalika, habari kutoka ndani ya chama hicho zinasema baadhi ya wanaojiwinda kwa ajili ya uongozi, pia waligawa fedha kwa kigezo cha kuwashukuru wajumbe waliowachagua kuingia katika Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinasema baadhi ya wajumbe waliopelekewa kadi hizo na fedha, walitoa taarifa kwa uongozi wa juu wa CCM pamoja na kuzirejesha, huku wakitaka wahusika wachukuliwe hatua.
“Kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya watu ndani ya chama kwamba ugawaji wa fedha nyingi kiasi hicho haupaswi kuvumiliwa hata kidogo, kwa hiyo ni dhahiri kwamba suala la chama kuchukua hatua halina mbadala, lazima hatua zichukuliwe,” alisema mmoja wa watendaji wa CCM makao makuu Dodoma na kuongeza:
“Waliorejesha hizo kadi na fedha hatukuwaruhusu waondoke hivihivi, bali tuliwataka waandike barua za malalamiko maana tunaweza kuwahitaji kwa ajili ya kutoa ushahidi mbele ya Kamati ya Maadili.”
Uchunguzi unaonyesha kuwa miongoni mwa waliorudisha fedha na kadi hizo ni wenyeviti wa wilaya na wajumbe wa NEC wa wilaya ambao ni sehemu ya walioshinikiza kuchukuliwa kwa hatua.
Akizungumzia suala hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula alisema mwanachama yeyote wa chama hicho hatakiwi kutoa michango, misaada, zawadi kwa mtu au katika shughuli yoyote bila kupata ridhaa ya uongozi.
“Kufanya jambo hilo ni kwenda kinyume na kanuni za chama. Ndani ya chama kila ngazi ina Kamati ya Maadili, wote ambao wameanza kwenda kinyume na kanuni za chama watahojiwa katika kamati hizo,” alisema Mangula na kuongeza:
“Hairuhusiwi kuwasafirisha wajumbe, kuwapa malazi, chakula, vinywaji na ukifanya hivyo utakuwa unakwenda kinyume na utaratibu uliowekwa na Kamati ya Sheria, Katiba na Kampeni.”
Akihutubia kilele cha maadhimisho ya miaka 37 tangu kuzaliwa kwa chama hicho, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete aliziagiza Kamati za Maadili na Usalama, kuwachukulia hatua stahiki viongozi na wanachama wake wanaomwaga fedha ili kupata uongozi. Kadhalika, Rais Kikwete alipozungumza na wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Mbeya, alisema kuanza kwa kampeni kabla ya wakati wake ni moja ya mambo yanayosikitisha na kwamba suala hilo limekabidhiwa kwa Mangula kwa hatua zaidi za kinidhamu.
Watakaowekwa kikaangoni
Mangula alisema wanaCCM watakaowekwa kikaangoni wapo katika makundi matatu, wakiwamo wale waliogawa fedha kwa lengo la kutaka kuungwa mkono katika harakati zao za kusaka uongozi wa nchi.
Alitaja makundi hayo kuwa ni wagombea wanaomwaga fedha kwa wanachama, mawakala wanaotumiwa na watu wanaoutaka urais 2015.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Mlilifuga joka wenyewe sasa limekuwa kubwa mnaanza kuhangaika. Lowasa yupo kila sehemu. Misikitini, makanisani ndani ya chama ananguvu kuliko yeyote.kazi mnayo ccm.