ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 22, 2014

WAZIRI ACHARUKA , ASIMAMISHA UJENZI WA STENDI YA IGUMBILO MANISPAA YA IRINGA

imc mahenge 3689c
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Dk. Binilith Mahenge (Aliyevaa shati la drafti) akiwa na viongozi wa mkoa wa Iringa na wa Manispaa ya Iringa.
Ujenzi wa kituo cha Mabasi cha Igumbilo Manispaa ya Iringa umesitishwa baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Dk. Binilith Mahenge kuamuru tathimini ya athari ya mazingira ifanywe upya.
Waziri amefikia uamuzi huo kufuatia kupata malalamiko juu ya athari za kujenga kituo hicho kutoka kwa Wizara ya maji, Mkoa wa Iringa na Mamlaka ya maji safi na maji taka mjini Iringa (IRUWASA) kuwa ujenzi wa kituo hicho utaathiri afya za watumiaji wa maji wa Iringa.
Anasema ni vema Halmashauri ya Manispaa hiyo kusitisha shughuli zote za kuendeleza eneo hilo kusubiri maamuzi ya serikali.
Waziri Mahenge anasema hayo mara baada ya kupata taarifa juu ya maji mkoa na kutembelea eneo la ujenzi wa kituo hicho.
Anasema kuwa hawezi kulitolea uamuzi suala la ujenzi wa kituo hicho bila kuwashirikisha wataalamu na kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bonaventura Baya kurudia kufanya tathimini upya ili kubaini tatizo lilopo pamoja na madhara yatakayojitokeza.
Naye Mkurugenzi wa NEMC , Baya anasema watafanya tathimini hiyo kwa muda wa wiki mbili na kuhakikisha kuwa majibu yatakuwa tayari ili kuweza kusaidia maamuzi kutolewa mapema kwa kufuata ushauri wa wadau mbalimbali juu ya ujenzi huo wa stendi ya Igumbilo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi anasema ni vema haki ikatendeka ili jambo hilo lisichukuliwe na kuonekana ni suala lenye maslahi ya kusiasa kwa baadhi ya wanasiasa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma alisema kinachotakiwa ni kufanya subira ya matokeo ya NEMC na maamuzi ya serikali na kuwa kujenga au kutojenga kituo hicho ni maamuzi yatakayotolewa na serikali.
Akitoa Taarifa kwa waziri, Katibu Tawala wa Mkoa, Wamoja Ayubu anasema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni mzuri na unadhana ya kuboresha miundombinu ya Manispaa ya Iringa, kukuza uchumi pamoja na kuvutia wawekezaji.
Aidha Wamoja anasema maji ya mto ruaha ni chanzo muhimu cha maji kwa wakazi wa Manispaa ya Iringa na kuwa IRUWASA imewekeza zaidi ya Sh70 Bilioni kwenye mto huo ili kuwapatia wananchi maji safi.
Iruwasa wanadai kuwa ujenzi wa kituo hicho utaendanana na shughuli za kibiashara na gereji jambo litakaloathiri maji kwa kuwa chujio zilizofungwa hazina uwezo wa kuchuja tqaka kemikali.
Wamoja alisema kuwa ujenzi huo endapo utatiririsha maji machafu taka ngumu na kemikali itaathiri maji ya mto Ruaha na pia itasababisha wakazi wa Iringa kuwa hatarini kutokana na kunywa maji yasiyo salama. Chanzo: Hakimu Mwafongo

No comments: