TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atafanya ziara ya kikazi ya siku tano
katika Jamhuri ya Watu wa China kuanzia tarehe 24 hadi 28 Februari, 2014. Ziara
ya Mhe. Membe inakuja kufuatia mwaliko kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa
Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi.
Mhe. Membe anafanya ziara hiyo nchini
China kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya Tanzania na
China. Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Membe atafuatana na Maafisa Waandamizi kutoka
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC).
Ziara hii pia ni muendelezo wa maeneo
ya utekelezaji baada ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi
Jinping aliyoifanya hapa nchini tarehe 24 na 25 Machi, 2013 na baadaye ziara ya
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda nchini
China mwezi Oktoba, 2013.
Akiwa
nchini China, Mhe. Membe atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Wang
Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China tarehe 25 Februari 2014. Siku hiyo hiyo
Mhe. Membe atamtembelea Makamu wa Rais wa China, Mhe. Li Yuanchao kwa lengo la
kumsalimia na baadaye atafanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Biashara wa China,
Mhe. Gao Hucheng.
Aidha,
tarehe 26 Februari, 2014 Mhe. Membe atatembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Poly Technologies yaliyopo katika mji wa
Shenzhen na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Kampuni hiyo kabla ya kutembelea Makao
Makuu ya Kampuni ya China Merchant
Holdings International ambako atapokea taarifa ya maandalizi ya kuanza kwa
mradi wa Ujenzi wa Bandari katika eneo la Mbegani huko Bagamoyo.
Mhe.
Membe pia atapata fursa ya kutembelea Kampuni ya HUAWEI ili kujionea shughuli
mbalimbali. Kampuni ya HUAWEI ina Mkataba na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi ya hapa nchini kuhusu Elimu kwa Njia ya Mtandao (e-Education) kwa Shule
za Sekondari.
Vile
vile tarehe 27 Februari, 2014, Mhe. Membe atautembelea Mji maarufu wa biashara
wa Guangzhou na kukutana na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi mjini hapo. Mhe.
Membe atatoa taarifa kuhusu hali ya uchumi, siasa na masuala ya jamii yalivyo
hapa nchini kwa sasa pamoja na kutoa
taarifa ya maendeleo ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Waziri
Membe pia atatembelea Eneo la Viwanda la Huadu tarehe 28 Februari, 2014 kabla
ya kurejea nchini tarehe 1 Machi, 2014.
IMETOLEWA
NA: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO
WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
24
FEBRUARI, 2014
No comments:
Post a Comment