Matokeo yalimaanisha kwamba Azam yenye pointi 53 sasa inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 7 juu ya Yanga iliyo na pointi 46 katika nafasi ya pili na mechi moja mkononi. Hata Yanga ikishinda mechi yake ya mkononi itabaki nyuma kwa pointi nne huku zikiwa zimebaki mechi tatu ligi kumalizika.
Mbeya City walijiimarisha katika nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 45 baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons kupitia goli la Paul Nonga katika dakika ya kwanza mjini Mbeya. Hata hivyo, Mbeya City wamecheza mechi mbili zaidi ya Yanga.
Mtibwa walishinda 3-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani. Wafungaji wa Mtibwa walikuwa Jamal Mnyate dk.14, Mussah Mgosi dk.31 na Mohammed Mkopi dk. 81 wakati la Coastal lilifungwa na Mbwana Hamisi dk. 17.
Kagera Sugar ilitoka 0-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera wakati JKT Ruvu ilishinda 3-1 dhidi ya Rhino kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Azam walitangulia kupata goli mapema katika dakika ya 16 kupitia kwa Khamis Mcha aliyefunga kwa shuti kali la mguu wa kushoto kufuatia pasi ya kifua ya mshambuliaji Kipre Tchetche aliyepokea mpira wa krosi safi ya beki wa kushoto Gadriel Michael.
Simba ilisawazisha goli hilo katika dakika ya mwisho kipindi cha kwanza beki wa kati Mganda Joseph Owino kuunganisha kwa kichwa kikali mpira wa 'fri-kiki' iliyochongwa na kiungo Uhuru Selemani.
John Bocco 'Adebayor' aliipatia Azam bao la pili kwa kichwa mpira wa 'tiktaka' ya Kipre Tchetche uliogonga nguzo ya lango na kumpoteza maboya kipa Ivo Mapunda katika dakika ya 56.
Mgambo, ambao waliwafunga Simba 1-0 kwenye uwanja huo katika mechi yao ya mzunguko huu wa pili, walipata goli la kwanza mapema katika dakika ya pili kupitia kwa Fully Maganga aliyemalizia vyema pasi ya Bashiru Chamacha kwa shuti lililomshtukiza kipa Juma Kaseja na kutinga wavuni moja kwa moja.
Katika dakika ya 14, refa Alex Mahaggi kutoka Mwanza alimuonyesha Mbuyu Twite kadi ya njano baada ya kuruka na kuuzuia mpira kwa mkono wa kulia katika harakati za kumdhibiti mchezaji wa Mgambo asiuwahi mpira.
Mgambo walilazimika kubaki 10 tangu dakika ya 30 wakati Mohammed Neto alipotolewa kwa kadi mbili za njano zilizofuatana. Alionyeshwa njano ya kwanza baada ya kukataa kukaguliwa na refa Mahaggi na ya pili kwa kuzozana na refa huyo kufuatia .kukataa kukaguliwa ndani ya uwanja akidaiwa kuficha kitu ndani ya jezi yake.
Hata hivyo, mwenyekiti wa chama cha soka Tanga (TRFA), Said Soud, alienda vyumbani kumkagua mchezaji huyo na kueleza kwamba hakuwa na kitu chochote. Soud alibainisha kuwa alimvua nguo Neto ili kujiridhisha na hakukuta chochote.
Mwenyekiti huyo alilalamika kwamba Mgambo imeonewa na kueleza kwamba watalipeleka TFF suala hilo kulalamikia kadi nyekundu hiyo.
Katika dakika ya 42 shuti la Mrisho Ngasa lilipanguliwa na kipa wa Mgambo, Tony Kavishe na kuwanyima Yanga bao katika mechi ambayo Uwanja wa Mkwakwani ulihudhuriwa na mashabiki wachache tofauti na kawaida ya mechi za Yanga hasa inapokuwa na mfululizo wa matokeo mazuri.
Nadir Haroub 'Cannavaro' aliisawazishia Yanga kwa njia ya penalti kufuatia mchezaji wa Mgambo kuunawa mpira ndani ya boksi katika dakika ya 52.
Malimi Busungu aliipatia Mgambo bao la pili kwa penalti iliyotolewa na kufuatia mfungaji huyo kuangushwa na Kelvin Yondani wakati akielekea kufunga katika dakika ya 63.
Mashabiki wa Simba walilipuka kwa furaha kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kila waliposikia taarifa za Yanga kufungwa goli Mkwakwani, Tanga na katika hali isiyo ya kawaida, mashabiki wa Yanga walikuwa wakiishangilia Simba wakati Wanamsimbazi wakiishangilia Azam FC.
Katika dakika ya 83, kipa Kavishe alidaka mpira wa kichwa uliopigwa na mtokea benchini Hamis Kiiza aliyeingia kuchukua nafasi ya Simon Msuva na dakika moja baadaye beki wa Mgambo Salim Mlima aliokoa mpira wa shuti la Didier Kavumbagu uliokuwa ukielekea langoni wakati kipa ameshapotea langoni.
Hassan Dilunga naye akapoteza nafasi nzuri ya Yanga kusawazisha wakati alipopaisha juu mpira kufuatia pasi ya Okwi katika dakika 86.
Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa;
Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadriel Michael, Aggrey Morris, David Mwantika, Michael Bolou, Himid Mao/ Bryson Rafael (dk.75), Salum Abubakar, John Bocco 'Adebayor', Kipre Tchetche/ Brian Umony (dk.80) na Khamis Mcha/ Kelvin Friday (dk.55). Simba: Ivo Mapunda, William Lucian, Issa Rashid, Joseph Owino,
Donald Mosoti, Jonas Mkude, Henry Joseph/ Abdulhalim Humoud (dk.66), Haruna Chanongo, Amisi Tambwe, Uhuru Selemani na Ramadhani Singano.
Mkoani Tanga vikosi vilikuwa;
Mgambo: Salehe Tendega/ Tony Kavishe (dk.32), Salim Mlima, Salim Gilla, Bashiru Chamacha, Bakari Mtama, Novatus Lukunga, Mohammed Samata, Peter Mwalyanzi, Mohammed Neto, Fully Maganga, Malimi Busungu.
Yanga: Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvini Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva/ Hamis Kiiza (dk.77), Hassan Dilunga, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa/ Hussein Jabu (dk.61) na Emmanuel Okwi
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment