Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Taasisi na
washirika wa Maendeleo bado wana fursa nzuri na pana ya kuendelea
kushirikiana na Serikali katika uendelezaji wa miradi mbali mbali ya
Maendeleo na Kiuchumi.
*********
Alisema
fursa hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuleta ustawi bora wa Wananchi
sambamba na kuimarisha nguvu za uendeshaji wa Taasisi na Mashirika hayo
katika mipango yao ya uzalishaji. Balozi Seif alisema hayo Ofisini
kwake katika Jengo la Msekwa Bungeni Mjini Dodoma wakati akizungumza na
Wawakilishi wa Taasisi za uwekezaji vitega uchumi kutoka Kampuni mbali
mbali za Kimataifa zinazojihusisha na masuala ya Ujenzi wa miradi
tofauti ambao tayari wameshafungua Umoja wa tawi lao Nchini Tanzania.
Alisema
Serikali inaendelea na sera na mipango ya ujenzi wa nyumba kwa
kushirikiana na washirika wa Maendeleo ili baadaye zikopeshwe au kuuzwa
kwa wananachi hasa wale wa kipato cha chini kwa lengo la kuondosha
tatizo la makazi ya Jamii.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza Kampuni za Kimataifa za Ujenzi
za Jamuhuri ya Watu wa China ambazo zinatoa huduma zake katika miradi
mbali mbali hapa Zanzibar.
“
Tumejenga imani kubwa kwa Makampuni mengi ya China ambayo yamekuwa
yakifanya kazi mbali mbali za Miradi ya Ujenzi kwa umahiri na umakini
wakizingatia zaidi muda katika Visiwa vyetu vya Unguja na Pemba “.
Alisema Balozi Seif.
Aliwaomba
wawakilishi wa Taasisi na Mashirika hayo ya miradi ya ujenzi kutenga
muda maalum wa kutembelea na kukagua fursa zilizopo Zanzibar ili waweze
kuwekeza miradi yao ya maendeleo. Balozi Seif alisema Sekta ya Utalii
bado ina nafasi nzuri kwa wawekezaji wa Kimataifa kuwekeza miradi yao
itakayiosaidia kutoa ajira pamoja na kuongeza mapato ya Taifa.
Akizungumzia
suala la huduma za Umeme wa hakiba inapotokezea hitilafu ya uliopo hivi
sasa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali Kuu inaendelea
kuangalia mazingira ya kuwa na hadhari na suala hilo.
Alisema
hivi sasa Kisiwa cha Unguja kinategemea huduma za Umeme za kianzio
kimoja tuu cha huduma hiyo kutoka Mjini Dar es salaam wakati Kisiwa cha
Pemba kikitegemea huduma hiyo kutokea Mkoani Tanga.
Mapema
Msaidizi wa masuala ya Biashara kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi
yenye Makao Makuu yake katika Mji wa Dalien Nchini China { CDIG } ambayo
tayari imeshafungua Tawi lake Dar es salaam Tanzania Bwana Lin Heng
alisema Taasisi yake iko huru kushirikiana na Mashirika ya Kizalendo
katika kuendeleza miradi mbali mbali ya Ujenzi.
Bwana
Lin Heng alisema Taasisi hiyo inajihusisha zaidi na miradi ya ujenzi wa
Bandari, Uwanja wa Ndege, Umeme pamoja na ujenzi wa nyumba ambapo
baadhi ya miradi inatekelezwa katika baadhi ya Mataifa Barani Afrika.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe
wa Wawakilishi wa Taasisi za uwekezaji kutoka Kampuni mbali mbali za
Kimataifa zinazojihusisha na masuala ya Ujenzi wa miradi tofauti ambao
tayari wameshafungua Umoja wa tawi lao Nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment