ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 3, 2014

Bunge la Katiba njiapanda

Kampeni ya kura ya siri au wazi kulisambaratisha
Kanisa latoa waraka mzito, mawaziri wadaiwa kuhaha
Bunge Maalum la Katiba lipo njiapanda baada ya kuwapo mivutano isiyoisha miongoni mwa wajumbe huku kukiwa na taarifa kwamba ikiwa leo muafaka kuhusu upigaji kura hautapatikana, baadhi ya wajumbe watajiuzulu.

Ikiwa hali hiyo itatokea, uwezekano wa Mkutano wa Bunge hilo kuendelea ni mdogo hivyo linaweza kuvunjika.

Taarifa za uhakika kutoka Dodoma zinaeleza kuwa baadhi ya wajumbe wanataka kura ya leo inayolenga kuamua juu ya kanuni za bunge hilo katika kupitisha rasimu ya katiba iwe ya siri au ya wazi, nayo iwe ya wazi.

“Kwa kweli hadi sasa tuna zaidi ya majina 250 ya wajumbe ambao wanapinga vikali jaribio lolote la kutaka kura ya kumua kanuni leo iwe ya wazi badala ya siri. Hili likitokea nafikiri Bunge hili litakuwa limefikia ukomo,” kilisema chanzo chetu kutoka Dodoma na kuongeza kuwa:

“Yaani ni mambo ya kushangaza saba, Chama Cha Mapinduzi inaelekea kimetoa maelekezo kuhusu hali hii. Waameamu kutumia njia hii kuwatisha wabunge. Wanataka kutumia wingi wao vibaya kushawishi vitu ambavyo havina maana.”

Kutokana na mvutano huo, wajumbe hao wameazimia kuwa leo watajiuzulu ujumbe kwenye Bunge hilo kwa madai kwamba wenzao hasa wanaotoka CCM, wanataka kura ya wazi kuamua mgogoro uliokuwa umetokea wiki iliyopita kuhusu upigaji kura wa kupitisha rasimu ya kanuni zitakazosimamia uendeshaji wa Bunge hilo.

MAWAZIRI WAHAHA
Miongoni mwa viongozi wanaodaiwa kuwa mstari wa mbele kushawishi wajumbe kukubaliana na kura ya wazi ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye anadaiwa kuendesha kampeni hiyo kwa kukutana vikundi mbalimbali vya wana-CCM.

Wakati Pinda akidaiwa kuendesha vikao vya mashauriano ofisini kwake, NIPASHE jana iliwasiliana na Mwandishi Msaidizi wa Waziri Mkuu, Irene Bwire, ili kujua juu ya vikoa hivyo lakini alisema kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa hajui chochote.

Naye Katibu wa Waziri Mkuu, Ndositi Haonga, alisema kuwa jambo hilo ni kubwa sana kwake hivyo hawezi kulizungumzia.

Mbali na Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi, alipoulizwa juu ya yeye mwenyewe kuwa kwenye harakati za kushawishi wajumbe wa Bunge kukataa kura ya siri, alisema hausiki na kampeni hizo.

Alisema alichosema bungeni Ijumaa iliyopita ndiyo msimamo wake, na kwamba misimamo yake hutoa ndani ya Bunge.

Yupo pia waziri mwingine aliyeko Ofisi ya Rais, naye amekuwa katika harakati kubwa za kushawishi wajumbe.

Waziri huyu ambaye jana hatukufanikiwa kumpata hivyo tunasitiri jina lake kwa sasa, anadaiwa kumwendea mjumbe mmoja ambaye ni kiongozi wa dini ili kumuunga mkono katika kampeni ya kupitishwa kwa utaratibu wa kura ya wazi.

Kiongozi huyu ambaye aliomba asitajwe jina kwa sasa, alithibitisha kuwa ameshawishiwa na waziri huyo katika hoteli aliyofikia, mjini hapa.

Alisema siku chache baada ya kuwasili mjini Dodoma, waziri huyo akiongozana na baadhi ya watu wengine walimfuata katika hoteli aliyofikia na kuanza kumshawishi ajiunge katika kundi la wajumbe wanaounga mkono msimamo wa CCM juu ya yaliyomo kwenye rasimu hiyo.

“… alinifuata, akaniambia ananiomba niungane nao katika kutetea msimamo wa chama kuhusu katiba bungeni,” alisema kiongozi huyo wa dini. Hata hivyo, alisema ombi la waziri huyo na ujumbe wake alilikataa.

Alisema katika kulikataa ombi lake, alimweleza waziri huyo kinagaubaga kuwa anachojua yeye ni kuwa aliteuliwa na Rais kuwa mjumbe wa Bunge hilo akitokea taasisi za kidini na siyo kwenda bungeni kuiwakilisha CCM.

Kwa hali hiyo, alisema alimweleza waziri huyo kuwa yeye yupo bungeni akiwakilisha maoni ya waumini anaowawakilisha, hivyo kamwe hayuko tayari kuwasaliti.

WAJUMBE WA CCM, CUF WATIBUANA
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ambao pia ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi visiwani Zanzibar, kutoka vyama vya CCM na CUF, wametibuana mjini Dodoma, baada ya wawakilishi wa CCM kukana mapendekezo ya Serikali tatu kwenye rasimu ya pili ya Katiba.

Hali hiyo ilitokea jana mjini hapa baada ya Wajumbe wa CCM wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kumkana Spika Pandu Ameir Kificho kwa kuwazunguka na kupeleka maoni tofauti kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wamedai kuwa maoni yaliyopelekwa kwenye Tume hiyo kuwa BWZ wameunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali tatu, siyo ya kweli na kwamba Spika Kificho alifanya hivyo kwa maslahi yake na hakutumwa na wajumbe hao.

Kadhalika, wajumbe hao walisema watapeleka malalamiko ya kuzungukwa na Spika huyo kwenye Kamati ya Chama na kikao cha wabunge wa CCM ambao ni wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Waraka huo wa Kificho ulikanushwa jana na baadhi ya wajumbe la Baraza Wawakilishi wa CCM ambao waliongozwa na Katibu wa Kamati ya Wawakilishi (CCM), Salmin Awadh Salmin.

Alisema wawakilishi wa CCM hawakuwa sehemu ya maoni yaliyowakilishwa mbele ya Tume hiyo kwa kuwa jambo hilo lilifanyika kwa siri bila ya kutolewa taarifa kwa viongozi wakiwamo wa Kamati ya Uongozi.

Alisema katika kipindi hicho cha ukusanywaji wa maoni, Baraza hilo halikutumia fursa hiyo ipasavyo.

Aidha, alisema viongozi wa Kamati ya Uongozi na wajumbe wa baraza hilo la CCM hawakushirikishwa, hawahusiki wala hawautambui waraka huo.

Alisema ni viongozi wachache waliobeba jukumu hilo kubwa na zito bila kuwashirikisha wajumbe walio wengi.

“Sisi tukiwa kama wawakilishi tunashukuru kwa taasisi yetu hii kupatiwa heshima kubwa ya kutoa maoni yetu ingawa utekelezaji wake haukuendana na malengo yaliyokusudiwa.

“Tunaomba wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine wachukue nafasi ya kuuelezea umma juu ya dhamira na malengo ya kufanya hivyo… natambua kuwa mazingira na maslahi binafsi yalichukua jukumu la kuisemea taasisi na hivyo kutimiza jambo hilo baya na ovu kwa taasisi yetu hii.”

Alisema taarifa ya maoni hayo iliyotolewa kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi haikuwa na baraka wala haikuvihusisha vikao husika na hivyo ilibeba maoni binafsi ya viongozi waliohusika.

“Tunaendelea kusisitiza kuwa hatukuwahi kukutana wala kuamua kuwasilisha maoni hayo, tunatambua labda wenzetu walikuwa na dhamira njema na pana zaidi hadi kupelekea utaratibu kusahaulika.

“Sisi wawakilishi wa CCM tutaendelea kusimamia na kutekeleza ilani, kanuni na miongozo ya chama chetu. Sisi tunaendelea kuamini kuwa bado miongozo ya CCM ni dira pana na yenye muono wa mbali zaidi,” alisema.

Salmin alisema baada ya kugundua kuwa maoni yaliyopelekwa kwenye Tume hiyo siyo ya kweli walimtaka Spika huyo kukanusha na alidai kuwa muda wa kufanya hivyo bado.

Juzi, iliripotiwa kwamba Baraza hilo limesema kuwa kuna waraka bandia umesambazwa ukieleza Baraza hilo limeazimia kwa pamoja kutaka mamlaka kamili ya mataifa ya Zanzibar na Tanganyika.

Waraka huo umesababisha mgogoro na kutoelewana kwa wajumbe katika Kamati ya Uongozi chini ya mwenyekiti wake Spika Kificho na Katibu wa kamati hiyo, Yahaya Khamis Hamad, baada ya kujitokeza hadharani baadhi ya wajumbe wakisema waraka huo umeghushiwa na hawautambui.

CUF WANENA
Akizungumzia madai hayo, Mwakilishi wa Jimbo la Mjikongwe (CUF), Ismail Jussa, alisema walichofanya wawakilishi hao ni uhuni wa kisiasa, kukanusha kitu walichoshiriki.

Alisema anashangaa kusikia madai hayo yakitolewa sasa ikiwa ni miezi miwili tangu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipowasilisha kwa Rais Jakaya Kikwete, Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba, Desemba 30, mwaka jana.

“Huo ni woga na usaliti wa CCM, baada ya kufika hapa Dodoma na kutokana na shinikizo la chama chao baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu na kuanza kwa vikao vya Bunge Maalum la Katiba, wameamua kutoa madai hayo. Wamepewa shinikizo.”

“Walichofanya hapa ni kumchafulia jina Spika Kificho ambaye ana heshima kubwa Zanzibar,” alisema.

Alisema maoni hayo hayakupitishwa na BWZ isipokuwa Kamati ya Uongozi kwa niaba ya Baraza.

Alisema ripoti iliyowasilishwa kwa Tume hiyo ya Warioba inazungumzia mapendekezo ya Mamlaka huru tatu ya Tanganyika, Zanzibar na Muungano.

Alisema kamati hiyo ina wajumbe 16 akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na wajumbe watatu kutoka CUF.

Aliwaja baadhi ya wajumbe kutoka CCM kuwa ni Balozi Seif Hamid, Mohammed Abood, Omary Yusuf Mzee, Asha Bakari Makame, Mgeni Hassan Juma na Mahmood Hassan Musa.

Wajumbe kutoka CUF ni Abubakari Hamis Bakari, Omary Ally Sheha na Abdallah Juma Ally.

Wakati akikabidhiwa Rasimu ya Katiba, Rais Jakaya Kikwete alitumia muda mwingi kuwasihi wajumbe wa Bunge hilo kutumia busara kikamilifu wakati wa kuijadili rasimu hiyo ili matunda yanayotarajiwa na wananchi yapatikane kwa ajili ya Watanzania wote na siyo watu au kikundi fulani cha watu au taasisi fulani.

Imeandikwa na Muhibu Said, Jacqueline Massano, Salome Kitomari, Dodoma.
Mwisho.
CHANZO: NIPASHE

No comments: