ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 15, 2014

Chopa yazua mtafaruku uchaguzi Kalenga

Kalenga. Polisi katika Mkoa wa Iringa, imepiga marufuku matumuzi ya helkopta siku ya uchaguzi mdogo wa Kalenga, kwa madai kuwa kufanya hivyo ni sawa na kupiga kampeni.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhani Mungi alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa taarifa ya hali ya usalama tangu kampeni zilipoanza hadi sasa kwa vyombo vya habari.
Mungi alisema siku ya uchaguzi siyo siku ya kampeni na kwamba polisi hawatakubali kuona vitendo vya kampeni vikionekana miongoni mwa wakazi wa Kalenga ikiwamo helkopta kutumika katika jimbo hilo na watu waliosafiri kutoka mikoa mbalimbali kwa kisingizio cha kulinda kura.
“Sasa nataka niwaeleze kuwa sheria iko wazi. Siku ya uchaguzi si siku ya kampeni. Hatutaki kuona helkopta za vyama vyote zenye kuashiria kufanya kampeni. Kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wakala wa chama kinachoshiriki katika uchaguzi huo na hao ndiyo wawakilishi wa chama hicho na walinzi halali wa uchaguzi ni polisi”alisema Mungi na kuongeza:
“Hatutaki kuona walinzi wa chama chochote katika Jimbo la Kalenga. Jukumu la kulinda uchaguzi, maisha na mali ya wana Kalenga ni la polisi, hatutaki kuona watu wasiokuwa na shughuli maalumu wanapitapita katika maeneo ya kupigia kura”alisema.
Tume wazungumzia
Wakati Mungi akitoa kauli hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) ilishindwa kutoa jibu la moja kwa moja kama helkopta hiyo itatakiwa kutumika ama la, hali iliyosababisha maswali mengi kutoka kwa waandishi wa habari.
Majibu ya Tume yalitolewa katika mkutano ulioitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubava ambaye kabla ya yeye kutoa ufafanuzi alitaka wajumbe wenzake kutolea majibu.
Akijibu swali la matumizi ya Chopa liloulizwa katika mkutano huo, Jaji Mstaafu John Mkwawa alisema “Matumizi ya vyombo vya usafiri tume haijakataza, ila mtu hapaswi kutumia kitu chochote kinacholeta hali isiyo nzuri na kusababisha usumbufu, chopa inaweza kusababisha kelele”alisema.
Naye Profesa Amon Chaligha alisema matumizi ya helkopta ni sehemu ya kampeni na kuongeza kuwa kimsingi isingeruhusiwa kutumika siku ya kampeni.
Akifafanua, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema vyombo vyote vya usafiri vinaruhusiwa kutumika siku ya kampeni, lakini kwa namna ambavyo vitatofautina na namna vilivyokuwa vikitumika wakati wa kampeni.
“Kama Helkopta itapangiwa utaratibu utakaotofautiana na ule uliotumika wakati wa kampeni,…kumpelekea mtu kuruka kutoka uwanja wa ndege na kwenda eneo husika bila ya kuathiri kuonesha mazingira ya kupiga kampeni hapo sawa, lakini sheria inasema siku ya uchaguzi siyo siku ya kampeni” alisema.
Chadema wajibu
Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chadema, Godbles Lema alisema Chadema kitatumia helkopta kuzungusha mgombea kutembelea vituo vyote 216 vitakavyotumika kupiga kura.
Alisema hakuna sheria inayozuia chombo hicho kuruka na kuongeza kuwa umaskini wa chama kimoja usitumike kama sheria ya kuzuia na wengine kutumia vifaa vyao vya usafiri.
“Chopa itaruka siku ya uchaguzi, itazunguka vituo vyote ikimbeba mgombea kwenda kukagua vituo vya kupiga kura kama sheria inavyoelekeza itabeba mgombea na mlinzi wake” alisema Lema na kuongeza:
“Wao CCM watatumia bodaboda, magari na sisi pia tutatumia bodaboda na magari pamoja na chopa. Polisi kusema tukirusha na CCM nao wakarusha tutagongana angani, kwanza wao si wafanya kazi wa anga. Polisi kazi yake ni kulinda usalama wa watu na mali zao”alisema Lema.
Lema alitoa sababu za mgombea wa Chadema, Grace Tendega kutumia helkopta katika uchaguzi huo kuwa ni kutaka kurahisisha kazi ya usafiri kutokana na jimbo hilo kuw a kubwa na umbali wa kituo kimoja hadi kingine kuwa mkubwa.
Kamanda awavaa wageni
Katika hatua nyingine Kamanda Mungi alipiga marufuku uwepo wa watu aliodai ni wageni kutoka mikoa mbalimbali, ambao walipelekwa jimboni Kalenga akidai wameandaliwa kwa ajili ya kufanya vurugu.
“Tumewasikia viongozi wa vyama wakitamba kuingiza maelfu ya watu mkoani mwetu kutoka mikoa mbalimbali ikiwamo Arusha na Mbeya kwa visingizio vya kulinda kura, Sasa nataka niwaeleze kuwa sheria iko wazi kabisa. Kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wakala wa chama kinachoshiriki katika uchaguzi huo na hao ndiyo wawakilishi wa chama hicho na walinzi halali wa uchaguzi ni polisi”alisema Mungi.
Akijibu hoja hiyo, Lema alisema kauli ya kuwapiga marufuku wageni kuwapo katika Jimbo la Kalenga ni vitisho ambavyo havikupaswa kutolewa na kamanda wa polisi.
“Kuhusu uwepo wa wageni kutoka Sombetini Arusha, Tarime, Mbeya na maeneo mengine hivyo ni vitisho.
Chadema tumeleta watu 2000 na kesho (leo) wanakuja watu wengine 1000, tutakuwa na watu 3000”alisema Lema.
“Polisi haina mamlaka ya kumweka mtu kizuizini kama hana kosa.hawa wamekuja kulinda kura hawajatoka Ukraine, kama watu hawa wataiba wachukuliwe hatua bila ya upendeleo”alisema Lema.
Alisema ikiwa wataamua kuua demokrasia kwa kisingizio chochote kile watakuwa wamefanya kitu kibaya kwa kutengeneza kundi la waasi watakaotoka miongoni mwa wananchi wanaotaka mabadiliko.
Polisi inawashikilia watu 19 kwa makosa mbalimbali wakati wa uchaguzi.
Katika hatua nyingine, Polisi wamesema wanawashikilia watu 19 wakihusishwa na kesi 21 zilizoripotiwa na vyama vya siasa.
Alisema katika kesi hizo tatu ndizo kesi kubwa, huku 19 zikiwa ni kesi ndogondogo zisizo na madhara kwa binadamu.
Alisema jeshi hilo limeshakamilisha majalada ya kesi 10 na kuyafikisha kwa mwanasheria wa serikali na kuongeza kuwa wakati wowote watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya mwanasheria kumaliza kuyafanyia kazi.
Alisema miongoni mwa watuhumiwa katika kesi hizo ni Padri wa Makanisa ya Orthodox wa Parokia ya Mtakatifu Bazil Mkuu yaliyopo katika Kata ya Nzih, Contantino Mbilinyi ambaye tayari alishahojiwa na kuachiwa kwa dhamana.
Kamanda wa Polisi alieleza kusikitishwa kwake na taarifa alizotoa padri huyo kwenye vyombo vya habari kuwa alipigwa na kufungwa kamba na kwamba taarifa hizo hazikufikishwa kwao na kama angezifikisha jeshi hilo lisingesita kufanyia uchunguzi.
Pia Kamanda Mungi alitoa ufafanuzi juu ya jeshi hilo kutomkamataka Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga aliyeripotiwa na mmoja wa wafussi wa Chadema akidai tuhuma zake si za jinai.
Chadema walia na Dafrtari la mpigakura
Katika hatua nyingine, Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imeingia katika mgogoro na Chadema baada ya kusisitiza kuwa itatumia daftari lawapiga la 2010 ambalo limefanyiwa maboresho kwa kuhakiki taarifa zake 2014.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa marekebisho yaliyofanyika katika daftari hilo la 2010 yalilenga kuondoa kasoro ndogo zilizokuwamo katika daftari la kudumu la mpigakura.
Akizuzngumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi wa Oganizesheni na Mafunzo ya Ufundi wa Chadema, Benson Kigaila alisema daftari hilo limeboreshwa kwa lengo la kutaka kukibeba chama tawala.
Alisema ikiwa daftari hilo litatumika, Chadema kitachukua hatua huku akiongeza kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajia kutoa tamko lake leo.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Huwa najiuliza hawa viongozi wa Chadema Wana justify vipi hizi gharama za chopa kwa wanachama wao.Maeneo km ya Kalenga ambayo yanaweza kufikiwa kirahisi kwa magari ambayo niya gharama nafuu, chopa za nini?