Mtu mwenye mafanikio kwenye mapenzi ni yule anayeamini katika saikolojia ya kujitambua. Hapa nikupe msisitizo kuwa ni lazima ujitambue ili uweze kuwa bora kwenye mapenzi. Kama hujitambui, maana yake hutajua ulitendalo.
Ikiwa utashindwa kujua ulitendalo, wewe utageuka kuwa kero kwa mwenzi wako. Ukifikia hatua hiyo, unadhani ni nani anaweza kukuelewa? Ni vema ujijue, ujifahamu kasoro na uimara wako katika uhusiano wako. Kama unamfurahisha au kumchukiza, yote yanafaa kugota ndani ya kichwa chako.
Je, una wivu? Hilo unapaswa kulitambua kwa sababu lipo ndani yako. Bahati mbaya ni kwamba watu wanakuwa na wivu wa kupitiliza lakini wakiambiwa wanakuwa wakali. Wanadai wanasingiziwa. Ni vizuri ukatambua upungufu ulionao kabla ya kuelezwa na mtu wa pili.
Hivyo basi, haya ninayoelekeza hapa hayawezi kuwa na matunda kama mhusika hajitambui. Hajui wivu wake unamsababishia hasara kiasi gani. Si hasara ya fedha, nazungumzia hasara ya kufeli kwenye mapenzi. Hii inatoa muongoza wa kuelewa yaliyo na faida.
Mtu anapoona wivu wa ndani, husumbuliwa na maumivu ya moyo. Aghalabu, akili yake hushindwa kufanya kazi inavyotakiwa. Mantiki ya hoja hiyo ni kwamba mwenzi wako hawezi kukutendea mambo matamu, ikiwa kichwa chake hakitakuwa katika hali ya kawaida.
Unaweza pia kuvuta picha na kujadili muonekano wako pindi unapokuwa na wivu. Hakikisha mwenzi wako anakuelewa kinaga ubaga kile unachomaanisha. Je, umegundua umepoteza raha kiasi gani? Umefahamu namna ambavyo huwa unaboa? Mpe uhuru mpenzi wako akwambie ukweli.
Inawezekana akawa anasita kukwambia bayana kutokana na hofu. Unapaswa kulijua hilo mapema. Unaweza kumpa nafasi aseme, akakujibu hakuna kitu. Ukishagundua kuwa anakuzhofia, jaribu kumshawishi ili afunguke. Akikubali kueleza la moyoni, ni tiba kubwa kwako.
Bila shaka utagundua ni kiasi gani anakerwa na tabia yako ya wivu. Je, ni nani anapenda kumuudhi mwenzi wake kila siku? Hakuna na kwa hakika hata wewe mwenyewe hupendi. Hivyo basi, amani yake itatokana na tabia yako ya kumuonea wivu.
Fikiria kuwa anashindwa kuwa mtulivu kufanya jambo lolote kwa sababu anahofu unaweza kulipokea tofauti. Kwa nini unamnyima uhuru kwa sababu ya wivu wako? Fungu moyo leo, muoneshe kuwa unamuamini. Imani yako itamfanya aongeze upendo kwako. Siku zote, mapenzi husafiri kwa mtindo wa nipe nikupe.
Hata hivyo, njia hii kwa watu wengine hushindwa kufanya kazi. Inapasa mtu mwenyewe awe amedhamiria kurejesha amani na furaha kwake na kwa mwenzi wake. Vema uzingatie kwamba wivu ukizidi ni ushamba. Jamii itakudharau, hata mwenzi wako akikuchoka, anaweza kukugeuza zuzu.
Ukirejea makala ya wiki iliyopita, katika kipengele namba tatu ambacho ni cha nane katika mtiririko wa sindano 11, chini ya maneno UNARUHUSIWA KUULIZA, nilielekeza kuwa;
Kama kuna jambo linakutatiza au umeona mwenzi wako anawasiliana na watu ambao huwaelewi, inawezekana pia akawa karibu na mtu wa jinsi yako, kwa hiyo unahisi kwamba unaweza kuibiwa.
Suluhu hapo siyo kukaa na msongamano wa vitu kichwani, keti naye ukiwa na hali ya utulivu kisha muombe akupe ufafanuzi.
Kama una hasira usizungumze naye kwa sababu inaweza kuharibu maana. Siku zote, mazungumzo ya uhusiano wa kimapenzi, huendeshwa kwa njia ya upendo. Kama unahisi mbele utapandwa na jazba endapo hutapokea majibu mazuri, vema ungoje siku utakayokuwa na utulivu wa kutosha.
Usiyafanye mazungumzo yenu kuwa mahojiano.
Jiweke kwenye kipengele cha mapenzi, kwa hiyo wewe siyo polisi. Pengine majibu yake yakawa siyo ya kunyooka, unachotakiwa kufanya ni kumuelewa au pale anapokuwa anasitasita, jaribu kumuongoza kuelekea kwenye jibu ambalo litasaidia ujenzi wa uhusiano wenu.
Hasira, jazba, ukali na mikunjo ya sura yako, vinaweza kumfanya ashindwe kukupa majibu sahihi. Kutokana na woga ambao atakuwa nao baada ya kuisoma ndita iliyopo usoni mwako, si ajabu akakuongopea. Ni kosa kubwa mno kuwa na uhusiano ambao unadumishwa na uongo.
Tafuta uelekeo sahihi wa penzi lako.
Wewe ni muelewa, kwa hiyo unafahamu maana ya ‘kuchati’. Hoja zako zijenge katika mtindo wa majadiliano. Zungumza na yeye azungumze.
Tena apewe nafasi anayoona inastahili, asije akasema ulimnyima uhuru, kwa hiyo alishindwa kujibu inavyotakiwa kwa sababu ulimkomalia kupita kiasi.
Hata hivyo, unashauriwa kuachana na vitu vingi, badala yake unatakiwa kukusanya yote uliyopokea kuhusu mwenzi wako, mengine unapuuza halafu yale machache unayoona yanatakiwa majibu, ndiyo uyawasilisha kwake akupe majibu. Kumbuka kwamba unatakiwa uelewe kwa urahisi kile anachokwambia.
Tabia ya kukusanya mambo mengi na kutaka majibu kwa wakati mmoja ni mbaya, kwani hutoa picha kuwa umemkamia kwa maswali, kwa hiyo mwisho wake atakuona una gubu. Ishi kwa upendo, tatua mambo yako kidiplomasia. Usikubali uonekane una gubu, kwani hiyo ikipita itakufanya mapenzi yakushinde.
2. USIISHI KWA DHANA
Hutokea mtu ameketi, ghafla anaanza kusumbuliwa na mawazo kuwa mwenzi wake yupo sehemu ya hatari akifanya mambo yasiyokubalika. Hili ni tatizo la wivu ambalo huwatesa wengi, hivyo kuelekea kukamilisha mada hii, nakutaka uachane na maishi ya dhana. Tafsiri matukio.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment