
Labda fedha zako ndizo zinakufanya uwe na kiburi, unaamua kumtenda anayekupenda kwa dhati kwa hisia kwamba fedha ndiyo kila kitu.
Hao wanaovutika na wewe, hawaji kwa upendo wenye mguso wa moyoni, wanavutiwa na noti zako. Unaweza usifilisike lakini kama hali ipo hivyo, siku ukiumwa itakuwaje?
Unahitaji mwenzi wako ambaye utamuona ndiye wako wa kufa na kuzikana. Anayekupenda kwa dhati, hatakukimbia ukiwa huna fedha au ukisumbuliwa na maradhi. Atahangaika na wewe mpaka mwisho. Nilishaandika uhusiano wa marehemu Sajuki na Wastara, waliishi vizuri nyakati ngumu za kusaka mafanikio, wakala matunda pamoja na katika majanga walishirikiana pamoja.
Hivyo ndivyo mapenzi yanataka, siyo kurukaruka kama kunguru. Na kila eneo ambalo nimeligusia hapo juu, huwa na matokeo ya kuumiza sana kwa aliyetenda. Karibu kila mmoja hapo hutamani kurejea kwa mwenzi wake aliyemfanyia ndivyo sivyo. Sasa hapo ndipo kwenye swali, kwa nini ujute baadaye?
WASOME REINA NA GAUDENSIA
Walianza uhusiano wao wakiwa chuo! Wote walikuwa wanasoma Chuo cha Uhasibu, Kurasini, Dar es Salaam ngazi ya stashahada. Baada ya kuhitimu kiwango hicho cha elimu, waliamua kufunga ndoa kabla ya mambo mengine yoyote. Kwa bahati nzuri, wazazi wa Reina walikuwa na uwezo mkubwa kifedha
Walimhakikishia mtoto wao kuwa watampa sapoti yote na maisha yao yasingeyumba! Ndoa ikafungwa, wazazi wa Reina waliwazawadia gari la kutembelea, nyumba na maduka mawili, moja la vifaa vya ujenzi na la pili lilikuwa la kuuza vyakula kwa jumla.
Hawakuishia hapo, waliwapatia ekari kadhaa za mashamba mkoani Pwani pamoja na nyumba ya kisasa huko Kilimanjaro.
Maisha yanataka nini?
Mwezi mmoja wa ndoa yao, wawili hao waliishi kwa upendo wa hali ya juu, ilikuwa siyo rahisi baada ya kutoka kwenye shughuli zao kumkuta Reina hayupo na mkewe Gaudensia, kila sehemu walifuatana kama njiwa.
Hakika walipendeza, kila aliyewaona alitamani kuishi maisha ya furaha waliyoishi wanandoa hao.
Miezi miwili baada ya ndoa yao, Reina akabadilika kwa kiwango kikubwa sana. Kuna maneno ambayo hapo kabla hakuwahi kumtamkia Gaudensia lakini kipindi hicho aliyatamka. Mwanzoni, Gaudensia aliyaona kama majaribu ya ndani ya ndoa lakini siku zilivyozidi kwenda hali ikawa mbaya sana.
Siku za mwanzoni, walikubaliana Reina awe anasimamia mauzo ya duka la ujenzi na Gaudensia duka la vyakula lakini miezi miwili baadaye, ilibidi maduka yote awe anayasimamia Gaudensia kwa sababu Reina hakuwa na muda. Alitoka asubuhi pwee kwenda kujumuika na wanawake wa mjini na alirejea nyumbani alfajiri akiwa amelewa na siku nyingine hakurudi kabisa.
Gaudensia alivumilia, wakati mwingine alijitahidi kuzungumza na mume wake ili abadilike lakini haikuwezekana. Reina alimpiga marufuku Gaudensia kutumia gari walilopewa na wazazi wake.
Zaidi ya hapo akawa anachukua fedha bila utaratibu kwenye maduka yote, Gaudensia akihoji anajibiwa: “Tulia hizi mali ni zangu, nimepewa na wazazi wangu, hukutoka nazo kwenu.”
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment