
Baadhi ya wananchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro wamepoteza makazi na mali zao, huku wengine wakiyakimbia na kukosa mawasiliano kwa kukatika barabara kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.
Baadhi ya wananchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro wamepoteza makazi na mali zao, huku wengine wakiyakimbia na kukosa mawasiliano kwa kukatika barabara kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.
Wakazi wa eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam, walilazimika kuyakimbia makazi yao kwa muda kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Wengi wao walikwenda kulala katika eneo la ujenzi wa ofisi za Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, wengine kwenye vituo vya mabasi ya mradi huo na baadhi yao walidiriki kulala katika mabomba yatakayotumika katika ujenzi huo.
Akizungumzia tukio hilo, mkazi wa eneo hilo, Hawa Rashid alisema nyumba yake ilijaa maji na godoro lake kulowa, hali iliyomfanya atafute sehemu ya kujisitiri usiku huo.
“Usiku tulikuwa wengi hapa, wengine wamerudi kwenye nyumba zao baada ya maji kupungua. Nyumba yangu bado ina maji, sijui leo nitalala wapi,” alisema mwanamke huyo.
Mwaka 2011, Serikali iliwataka wakazi wote wa maeneo ya bondeni kuhama maeneo yao na kupewa viwanja huko Mabwepande. Baadhi yao walitii wito huo na kwenda kupata viwanja.
Bado watu wengi wanaishi katika maeneo hayo licha ya kuhatarisha usalama wao. Nyumba zilizopo zimeathirika vibaya na mafuriko, hali inayoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko na usalama wao.
Akizungumzia mpango wa kuhamia eneo la Mabwepande, Mwenyekiti wa Mtaa wa Chalambe – Upanga Magharibi, Christopher Lugemalila alisema ni kaya 600 tu za watu waliopata viwanja Mabwepande kati ya kaya 5,000 zilizokuwa zinaishi mabondeni.
Lugemalila alisema viwanja hivyo viligawiwa kwa upendeleo na baadhi ya waliopata viwanja hawakuwa na nyumba kabisa maeneo ya mabondeni.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Dk. Filbert Osenga alisema ni kweli viwanja vilikwisha Mabwepande, lakini waliobaki eneo la Jangwani waligoma kuhama wakafungua kesi ambayo bado ipo mahakamani.
Hata hivyo, wakazi wa eneo la Jangwani wanaonekana kuathirika na mvua hizo kwa sababu eneo hilo lipo bondeni na nyumba zao hazina uwezo wa kustahimili maji mengi.
Morogoro:
Zaidi ya kaya 10 Kata ya Kihonda, Mtaa wa Kaskazini L, Manispaa ya Morogoro nyumba zao zimezingirwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mafuriko hayo yalitokea juzi baada ya mvua kubwa iliyoambatana na radi kunyesha mkoani hapa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro.
Mmoja wa wananchi waliopatwa na maafa hayo, Andrew Nkiko alisema kuwa maji hayo yalifika nyumbani kwake saa 10.00 usiku wa Machi 27 mwaka huu na kuvunja uzio wa ukuta wa nyumba yake na kuingia ndani na kuharibu mali mbalimbali.
Pwani:
Wakazi wa Vijiji vya Kidogozero, Kitonga na Miro, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wamekosa mawasiliano ya barabara baada ya mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana na kusababisha kuvunjika makaravati ya barabara.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment