Freddy Macha
Majuma mawili yaliyopita, habari za mwanamke wa London aliyeoana na mbwa wake aitwaye Sheba zilitangazwa na gazeti la Metro.
Metro hutolewa bure, kila siku, kwa wasafiri miji mbalimbali ya Uingereza. Baadaye mwanamke huyo Amanda Rodgers, alipohojiwa na ITV mjini London alidai : “Nafahamu ndoa yangu na Sheba haitambuliki kisheria. Lakini ilikuwa njia nzuri ya kuonyesha ninavyomthamini Sheba. Sheba amekuwa nami miaka mingi, hunichekesha na kunifariji ninaposononeka. Sikuweza kumpata mwenzi mwingine wa maisha kama huyu.”
Sheba ni mbwa anayeongelewa na Amanda.
Mwenzenu alishachoka, baada ya kuishi na wanaume wawili, kuyeyushwa na uhusiano pamoja na kero akaamua kufunga ndoa na mbwa wake.
Mila ya wafuga mbwa wa ndani tofauti na wale walindao nyumba hata wanaosaidiana na polisi. Mbwa wa ndani hutunzwa kama sehemu ya familia, hutunzwa na kupewa majina kama ndugu yeyote wa damu.
Hivyo, Sheba ambaye ni mbwa jike, alitimiza kanuni za mapenzi ambazo mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 47 alizihitaji.
Wanasaikolojia huuliza: Siri ya mapenzi ni nini?
Niambie wewe msomaji.
Siri ya fenesi la moyo nini?
Wimbo mmoja wa taarabu uliwahi kushauri zamani : “Ukipenda Pendeka...”
Amanda Rodgers ameshaishi miaka 47.
Miaka arobaini na kitu kwa mwanadamu huitwa umri wa makamo kwa Kiswahili. Bado uzee kushtadi hakika, bali kukomaa kimaisha; kupitia mengi hata ikibidi kujaaliwa kajukuu. Lakini siyo wote tunaojaaliwa haya.
Hapa uzunguni, ndoa zimefikia kilele cha ugumu siku hizi. Ugumu kiasi ambacho ndoa za jinsia moja zinapigiwa madebe kukidhi haja.
Kihistoria miaka 50 sasa uhuru na ukombozi wa akina mama umeleta maendeleo katika uchaguzi wa kazi na taaluma, uhusiano na wanaume, malezi ya watoto, kujiamini, kujituma na kadhalika. Hapo hapo maendeleo haya yameporomoka kiuwiano.
Wanawake wamekuwa wahitaji na wakali zaidi. Matokeo yake ndoa hazidumu. Wanaume wanakimbia nyumba zao. Habari za baadhi ya midume kuzaa kisha kuua watoto, mke na wao wenyewe zinazidi kuenea. Wanaoumia ni watoto.
Katika hali hii ngumu, unawakuta wachache wanaoamua bora kuoana na viumbe wengine kuliko wanadamu.
Kuna habari za waliooana na nyoka, samaki, hata waliofunga ndoa na vitu walivyovihusudu, mathalan madaraja hata viwanja vya kuchezea. Yanachekesha, yanastaajabisha, yanakondesha, yanasikitisha.
Ila uhusiano mzuri kati ya mtu na mbwa ndiyo mbingu.
Mbwa ni kiumbe anayethaminiwa sana Uzunguni. Nakumbuka mara yangu ya kwanza kuzozana na utamaduni huu nilikuwa nikiishi Ujerumani mwaka 1985. Ongeza sasa hizo nafasi ndogo za kufungiwa ndani, mbwa hukosa jaha. Wanaojiweza huajiri watembeza mbwa, wanaotoza fedha kwa waliokwenda kazini na kukosa nafasi kuwatembeza na kuwafanyisha mazoezi.
Hilo, moja.
Pili, mbwa huyo wa jirani aliacha kinyesi chake pale mlangoni kwangu. Kila nilipolalamika nilionekana eti nimejaza chuki. Ilitokea hata siku moja mgeni wangu akakanyaga kinyesi cha mbwa. Zingatia harufu iliyokithiri na matusi yaliyotutoka.
Nilipogomba nikaambiwa; “Ah nyinyi Waafrika mnachukia wanyama, mnatesa wanyama, hamna utamaduni wa elimu viumbe.”
Baada ya malalamiko ya majuma kadhaa, kutosikilizwa na kupuuzwa, nikaamua sasa kumvizia yule mbwa. Asubuhi moja wakati akijisetiri mlangoni nikamvizia na tofali dogo (maana mawe hayapatikani ovyo miji ya Ulaya, nikambabua vizuri. Kilio alichokitoa kilizagaa eneo lote lile. Magari yalisimama. Wapita njia wakaduwaa.
Utadhani nimeua. Pamoja na yale mavi kuwa ushahidi nikaandamwa. Simu ikapigwa polisi, dakika kumi hazikupita, king’ora hicho. Askari watatu wakaja; pingu mkononi, vigongo. Nikazolewa mkuku hadi kituoni.
“Akili zako ziko sawasawa?”
Nikaelezea hali mbaya ya kinyesi na kadhalika.
“Kwa nini hukuja kituoni kushtaki?”
Nikasema sikujua kama unatakiwa kumshtaki mbwa kwa kwenda haja kubwa.
“Unatakiwa ndiyo. Huo ni uchafu wa mazingira.”
Yote yalikuwa mapya kwangu. Nilizoea mengine, Afrika.
“Umefanya kosa la jinai. Umemdhuru kiumbe na mali ya mtu.”
Maneno yalikuwa mengi. Lakini pamoja na ukali wao, sheria za nchi hizi zina haki. Ukishtakiwa unapewa pia wakili. Wakili akatetea sijaishi sana nchini. Nimezoea mazingira na utaratibu mwingine wa Bara la Afrika. Sifahamu utaratibu.
Nikaonywa. Lakini ilibidi kuhama; kila nilipopita nilinyoshewa vidole kitongojini. Kampiga mbwa. Mtesa wanyama.
Mbwa, paka na wanyama kwa jumla huheshimiwa zaidi. Siyo ajabu kwamba huyu Amanda Rodgers akaamua kufunga nao pingu za maisha. Ukitazama video au sinema zinazoonyeshwa katika mtandao wa You Tube utathibisha uhusiano huo. Taswira za wanaume kwa wanawake wakipigana mabusu (midomoni) na mbwa ni nyingi .
Kijana wa miaka 19, Wayne Bryson alifikishwa mahakamani mapema mwezi huu kwa kufanya ngono na mbwa wa mke wake. Mke anasema asingefahamu kilichokuwa kikiendelea kama siyo jamaa kujipiga picha ya video katika simu yake.
Kisa kilichojulikana zaidi duniani ni cha dada wa Kimarekani, Alyssa Rosales aliyefanya ngono na mbwa kwa takriban dakika moja halafu akasambaza video Facebook na You Tube. Baada ya malalamishi iliondolewa. Leo Alyssa katajirika kutokana na tendo hili. Ukitaka kuitazama filamu kuna malipo.
Lakini siyo Wazungu tu.
Video za Wakongo, Wakorea na Wachina wakichinja mbwa, kuwauza au kuwala kama kuku zimejazana You Tube.
Yote haya yanatueleza nini kuhusu maisha yetu ?
Je, mapya?
Sidhani. Tangu zamani wanadamu tulikuwa na tabia ya kufanya vitendo viovu na wanyama. Leo vyaonekana zaidi kutokana na uwazi na usambazaji haraka wa habari. Vilevile siku hizi wanadamu hatuoni aibu kuelezea mambo yetu ya undani, hadharani. Ni sura halisi ya maendeleo tuliyoyafikia.
Mwananchi
1 comment:
matokeo yote haya yanatufunza kwamba hatumuamini mungu anavyostahili kuaminiwa na kuheshimiwa na kuabudiwa na kuogopewa hatuna FEAR OF GOD,mtu ukiwa nayo hii hutofanya mambo kama haya ya ajabu ajabu na pia tuna pupa na maisha na kukata tamaa hajalishi hata ukifika miaka 59 kama hujaolewa au kuowa muamini mungu kuna siku utakuja kumpata mwenzako atakaye kupenda na kukuthamini tunakata tamaa sana wakati mungu hakati tamaa na sisi why?
fear god na muamini kwa moyo wako wote na mila na tamaduni zako zenzi usizitupe ukizitupa matokeo yake utakuwa mtundwa na kufanay matendo yasio ya kibinadamu kama haya ya kuoolewa na mbwa au kuowa au kufanya ngono na mbwa au mnyama yeyote yule
mungu wangu tusaidiye watanzania wote wakike kwa wakiume tusiwe kama hawa watu amen amen amen
Post a Comment