ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 3, 2014

MWENZI WAKO ANAKULIZA, UNAMLIZA? -2

HAPA ni mahali sahihi kwa marafiki kukutana na kupeana changamoto za hapa na pale kuhusu namna ya kuboresha uhusiano na wenzi wetu. Kama kawaida, lugha inayotumika hapa ni laini na rahisi kueleweka.
Ni mada iliyoanza wiki iliyopita, ikizungumzia zaidi kutafuta amani ya kudumu katika uhusiano (hasa ndoa) na kukaa mbali na matatizo yatakayoweza kusababisha machozi baina ya wapenzi.

Nilishafafanua vipengele kadhaa wiki iliyopita, lakini kubwa zaidi nilieleza kuwa, ni vizuri kupigania amani ya uhusiano wako. Ndugu zangu, popote pasipo na amani, machukizo hupata nafasi.

NJIA NZURI ZAIDI NI MAZUNGUMZO
Hata kama kuna tofauti kidogo imejitokeza kwenye uhusiano wenu, ni vizuri kukaa na mwenzako mkazungumza. Siyo sahihi kuweka mambo yenu bayana.
Epukeni ugomvi mbele za watu au watoto wenu. Matatizo yenu yote yamalizeni chumbani mkiwa wawili tu. Kwanza inajenga heshima yenu na ni rahisi kusikilizana.

BORESHA UHUSIANO WAKO
Wengine huamini ili uhusiano uwe bora lazima (labda) umnunulie mpenzi wako gari au kitu kingine kikubwa cha thamani. Si lazima. Yapo mambo mengi madogomadogo ambayo ukiyafanya yanazidisha thamani ya uhusiano wenu.

Kwa mfano vijizawadi vidogovidogo kwa wanandoa ni vizuri.
Tatizo baadhi wakiingia kwenye ndoa, wanasahau kila kitu. Hilo ni tatizo. Mnunulie mwenzako hata shati, saa au sketi, utakuwa umemfurahisha.

TENDA MUDA NA FAMILIA
Nyumba yenye furaha ni ile inayopata muda wa kutosha kukaa pamoja. Wanaume wengi wanakuwa bize zaidi na kazi na kuangalia maendeleo ya familia.
Sawa, unaacha chakula, watoto wanakwenda shule nzuri, mke yupo katika mazingira ya kuridhisha, lakini je, unapata muda wa kukaa nao pamoja?

Baadhi ya wanaume wana tabia ya kurejea majumbani mwao usiku, lini utapata muda wa kucheza na watoto wako?
Ni muda gani utasikiliza matatizo yao? Uwepo wako pekee unaongeza ladha na heshima ndani ya ndoa yenu.

Wakati fulani ujitahidi hata kutoka nao mwisho wa wiki na kupata chakula cha jioni nje ya nyumbani kwenu. Si tu itaongeza upendo na furaha ndani ya nyumba lakini pia utawafundisha wanao upendo na kushirikiana.

KWA NINI UMLIZE?
Una sababu gani ya kuishi kwenye ndoa kama vile ni simba na swala? Shughulisha ubongo wako, una kila sababu ya kuhakikisha mwenzako anakuwa mwenye furaha muda wote.
Hilo ni jukumu la wanandoa wote, maana mnategemeana. Furaha yako iko mikononi mwa mwenzako, naye anakutegemea wewe umpe faraja siku zote.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

GPL

No comments: