ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 26, 2014

Sitta akabwa koo

  Atuhumiwa kwa upendeleo Kamati ya Uongozi
  Lipumba akataa uteuzi, kamati imejaa CCM watupu
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta akiwa katika tafakuri nzito wakati mjumbe wa Bunge hilo, Prof. Ibrahim Lipumba alipokuwa akitoa maelezo ya kukataa kuteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, mjini Dodoma jana.Picha/Khalfan Said

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amekabwa koo kwa kutuhumiwa kwamba amefanya upendeleo katika uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Uongozi kwa kuwajaza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hali hiyo imemlazimisha Mjumbe wa Bunge hilo, Profesa Ibrahim Lipumba, kukataa uteuzi wake.

Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) alikataa uteuzi katika kamati hiyo, kwa madai kwamba hawezi kuwa chambo cha kutimiza malengo ya CCM.

Uteuzi wa wajumbe watano wa kamati hiyo, ambao wataungana na wenyeviti wa kamati 12, ulifanywa na Sitta, juzi usiku.

Walioteuliwa ni Fakharia Shomari (CCM), Mary Chatanda (CCM), Profesa Lipumba (CUF), Amon Mpanji (Kundi Maalumu) na Hamoud Aboud Juma (CCM).

Hatua hiyo imefuatia malalamiko ya kuwapo kwa upendeleo wa kuteua wajumbe wengi kutoka CCM na kuviacha vyama vya upinzani vikimezwa na chama hicho.

“Nimesikitishwa na mpango maalumu mlionao wa kulifanya Bunge hili Maalumu kuwa Bunge la CCM. Siwezi kuingia katika kamati ya uongozi,” alisema Profesa Lipumba.

Aliongeza: “Sitaweza kuwa chambo cha kutumiwa kuwa kamati hiyo ina mwenyekiti mkubwa wa chama kikubwa cha upinzani. Hilo siwezi kulifanya. Tutapambana kwenye kamati namba 10 ndani ya Bunge Maalumu kujenga hoja, lakini hili nawaachia wenzangu muweze kuendelea na mipango mliyonayo.”

Juzi wakati Sitta akitangaza kufanyika uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo, kuliibuka hofu ya Uzanzibari na Ubara, huku baadhi ya wajumbe wakidai kuwa kutokana na wingi wa wajumbe kutoka Bara na CCM, wajumbe wa Zanzibar watashindwa kupata nafasi za uongozi na kusababisha maamuzi kuwa ya upande mmoja.

Kati ya kamati 14 zilizofanya uchaguzi juzi, ni kamati moja tu, ambayo inaongozwa na mjumbe kutoka Zanzibar, ambaye ni Hamad Rashid. Profesa Lipumba alisema mwenyekiti ameeleza jinsi alivyojitahidi kupata aliowapanga hata wakaingia kwenye kamati hiyo.

“Kwa mantiki hiyo hiyo mmejipanga vizuri sana kuhakikisha viongozi wa vyama vya upinzani na wajumbe wanaotoka katika vyama vya upinzani hawaingii katika kamati ya uongozi.”

“Mimi ni mwenyekiti wa taifa wa chama cha CUF. Chama chetu ngome yake kubwa ni Zanzibar na sababu ya mimi kuingia CUF ni kuleta umoja wa kitaifa. CUF ilikuwa na nguvu sana Zanzibar kuliko Bara. Sababu yangu ilikuwa kuunganisha CUF Bara na Zanzibar kuwa chama cha kitaifa,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema katika hali hiyo na mchakato mzima ulivyokwenda katika kipindi hiki, tangu Sitta amekuwa mwenyekiti, hali inavyokwenda ndani ya Bunge hilo, ni wazi kabisa kwamba, hakuna nia njema ya kupata katiba ya wananchi.

Akijibu, Sitta alisema mjumbe ana hiari ya kuchukua ama kutokuchukua nafasi anapoteuliwa.

“Nakushukuru kwamba, umeamua kusema unachoona wewe. Ni ukweli na kwamba, unakataa uteuzi wa mwenyekiti.”

Akizungumzia wajumbe kulalamikia kamati zote kuongozwa na wajumbe kutoka CCM, Sitta alisema hawezi kulaumiwa kwa sababu uchaguzi ni matokeo ya uchaguzi na kwamba, mwenyekiti hahusiki labda kwenye uteuzi.

Kuhusu uwiano, alisema alishaeleza kuwa ndiyo hali halisi iliyomo ndani ya ukumbi huo, ndiyo maana ikawekwa kinga ya theluthi mbili kwa kuzingatia upande mmoja usipate kila kitu.

“Wale wanaotaka kusema mwenyekiti hakuteua huyu, hakuteua yule haitusaidii kitu,” alisema Sitta.

MAPALALA
Akitoa malalamiko yake, Mjumbe James Mapalala, alisema jinsi Bunge hilo linavyopeleka mambo ya kamati, hayaendi jinsi yanavyotakiwa.

Alisema anajua CCM ni chama kikubwa, ndiyo kina wabunge wengi zaidi, lakini haionyeshi kama kina heshima na kwamba, hakukuwa na sababu ya kuwaita wajumbe wa vyama vingine kutokana na kuwadhalilisha.

“Natoa mfano wangu jana (juzi), niko kwenye kamati namba moja, ambayo mheshimiwa waziri mkuu alikuwamo. Wakati tumekaa tunataka sasa kuanza majadiliano, hatujachagua mwenyekiti, bwana mkubwa mmoja akaruka kutoka kwenye kiti chake, akaruka kukaa kiti cha mwenyekiti akasema mimi sasa ndiyo mwenyekiti,” alisema Mapalala. Alisema alipoona hivyo, ikabidi amuulize: “Nani amekuchagua? Hujachaguliwa bwana.

Wewe tufuate taratibu. Wakasimama watu wengi wakasema huyo tumemchagua na kunifanya mimi mtu sifai nimefanya namna gani sijui.”

“Sasa wakatumia nguvu, wakaanza kuruka kuruka. Sasa ikabidi niwaambie mimi sitapiga kura, lakini basi baadaye waziri mkuu akaja kuniambia usiwe unafuata mambo madogo madogo ya watu wengine ya vijana wahuni na mimi nikawa sina la kusema, sina la kufanya. Nikamheshimu mheshimiwa aliyeniashauri, nikapiga kura.”

Alimuomba mwenyekiti kuwa watu wenye vyama vidogo wapate heshima kama wabunge wengine waliopo ndani ya Bunge hilo.

“Tunaomba haki yetu ya kawaida tuwe tunaheshimiwa. Tukitoa mawazo yazingatiwe vile vile. Lakini siyo kupelekwa namna hiyo,” alisema Mapalala.

Hata hivyo, Mjumbe William Lukuvi, alisimama na kutoa ufafanuzi kuwa kamati namba moja ilifanya uchaguzi wa kidemokrasia na kamati nyingi zilifanya hivyo. Alisema Mohamed Habib Mnyaa alimpendekeza Ally Keisy kuwa mwenyekiti wa muda na watu wote waliunga mkono na kwenda kuchukua kiti. Keisy aliwaongoza na kufanya uchaguzi vizuri.

“Waziri Mkuu hakusema Keissy ni mhuni, hayo ni maneno ya kutunga, hawezi kumuita mjumbe mhuni,” alisema Lukuvi.

SEMAKAFU
Naye Mjumbe Dk. Ave Maria Semakafu alisema kuwapo kwa idadi kubwa ya viongozi kutoka katika kundi moja la chama cha siasa, kunatokana na makosa yaliyofanywa awali katika mchakato huo wa kuruhusu wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi nao kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba.

Dk. Semakafu ambaye anatoka kundi la Taasisi za Elimu, alisema kilichopaswa kufanywa katika mchakato huo ni kuteua wawakilishi katika makundi hayo pamoja na vyama vya siasa ili kuweka uwiano sawa wa kuchambua rasimu hiyo na kuipeleka kwa wananchi kuipigia kura.

Alisema uwiano huo ungeleta sura halisi ya utaifa na siyo ushabiki wa chama kimoja kinachotaka kufanya maamuzi yao.

KAFULILA
Naye David Kafulila alimwambia Sitta kuwa amepata nafasi hiyo kutokana na uhalali wa kisiasa na kukubalika na makundi yote katika Bunge hilo, lakini tayari wajumbe wameanza kutokuwa na imani naye kutokana na kuonyesha dhalili za upendeleo wa chama chake cha CCM.

“Mwenyekiti wewe ni sawa na mzazi wangu. Nakuheshimu sana. Kuna uhalali wa kisheria na uhalali wa kisiasa. Wewe umechaguliwa na makundi yote kutokana na uhalali wa kisiasa.

Lakini tayari tumeshaingiwa na shaka kutokana na upendeleo wa wazi unaolifanya Bunge hili kama ni Mkutano wa Chama Cha Mapinduzi,” alisema Kafulila.

Alimtaka Sitta kujipa muda wa kutafakari upya kuhusu uteuzi wake wa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ili kuweka uwiano wa vyama vya siasa, ambao wamekosa nafasi za uongozi katika kamati za kawaida ili kuondoa dhana ya upendeleo katika kamati hiyo.

MBATIA
James Mbatia aliwataka wajumbe kujitambua kuwa wote ni viongozi na walishafanya makubaliano ya kuhakikisha Bunge hilo linakuwa na umoja wa kitaifa kwa kila mmoja kujivika sura ya kitaifa kuliko kuweka misimamo ya vyama vya kisiasa.

Alisema katika kikao hicho kilichofanyika Februari, mwaka huu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, viongozi wa dini pamoja na viongozi wakuu wa vyama vyote vya siasa walikubali, lakini anashangazwa suala hilo limekuwa tofauti kuonekana likiongozwa na CCM kwa maslahi yao.

LUGOLA
Kangi Lugola alisema iwapo Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo itakuwa na wajumbe wengi wa CCM, watasababisha ajali kubwa katika utungaji wa Katiba ya nchi.

Lugola ambaye pia ni Mbunge Mwibara (CCM), alisema CCM ni lazima ifanye kazi na vyama na makundi mengine ili Katiba ipatikane.

“CCM ni gari kubwa…na gari hili kubwa la CCM tukiliacha likiserereka bila ya kukanyaga breki za mara kwa mara…nina kuhakikishia kwamba tutasababisha ajali kubwa sana katika utungaji wa Katiba katika nchi hii,” alisema Lugola.

Alisema Sitta alipewa heshima na dhamana kubwa na wajumbe wa Bunge hilo, ambao wanawawakilisha Watanzania zaidi ya milioni 44 kutokana na umahiri na uweledi wake.

“Sasa katika mazingira haya nilitarajia sana ya kutomeza wadogo…dhana ya kutomeza wachache ndiyo ingekuwa msingi, ambao wewe ungeamua kuwateua wajumbe watano hawa na si mjumbe wa CCM…ungewateua watano hawa kwa kuangalia masuala ya jinsia, vyama na makundi maalumu, lakini asiwamo mtu wa CCM hata mmoja,” alisema Lugola.

MNYAA
Mohammed Habib Mnyaa, ambaye ni Mbunge wa Mkanyageni (CUF), alitaka kujua kama Bunge hilo la Katiba ni la CCM au ni la nchi nzima. Mnyaa alisema Bunge hilo linapoelekea, hata maneno ya Rais Jakaya Kikwete aliyoyatoa wakati alipokuwa akilizindua hayatafuatwa.

Alisema hata kwenye orodha ya majina ya wajumbe wa kamati hizo limewekwa jina na chama au kundi analotoka, kiasi ambacho hata mjumbe angegombea asingepata uongozi.

“Mimi jana (juzi) niliomba busara za kiti na katika majibu yako, nikaomba Mwenyezi Mungu lisitokee hilo…lakini viashiria vyote vya kitaalamu vilikuwapo kuonyesha litatokea hilo.

“Na Mungu kajaalia likatokea hilo…kwamba sasa katika kamati 12 wajumbe kutoka Zanzibar wenyeviti ni watatu tu kati ya 12…hii ina maana kubwa sana hata katika kamati ya uongozi,” alisema.

MSIGWA
Mchungaji Peter Msigwa alisema tayari hofu ya kumezwa kwa baadhi ya makundi na vyama vya siasa vya upinzani imeshaonekana wazi katika Bunge hilo kutokana na mwenyekiti wake kuonyesha wazi upendeleo wa chama anachotoka.

Alimtaka Sitta kutumia kiti chake kwa busara pasipo upendeleo wowote ule, kwani vyama vya upinzani navyo vina wafuasi wengi sana na wakishindwa hapo bungeni watatoka nje kwenda kuwaeleza Watanzania kuwa katiba itakayotengenezwa siyo ya umoja wa kitaifa bali ni ya chama kimoja tu cha CCM.

Imeandikwa na Beatrice Bandawe, Emmanuel Lengwa, Jacqueline Masano na Ashton Balaigwa, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Sita na Kamati nzima ni Wahuni. Tunakoipeleka nchi kwa katiba ya kulazimisha ni kubaya saana.