ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 24, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,
Mhe. Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Mhe. Frank-Walter Steinmeier, atafanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini tarehe 25 Machi, 2014 yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Ujerumani hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji.

Mhe. Steinmeier ambaye atafuatana na ujumbe wa watu 80 wakiwemo wafanyabiashara kutoka makampuni makubwa ya Ujerumani, Wabunge, watendaji wa Serikali na Waandishi wa Habari, ataonana kwa mazungumzo na Mwenyeji wake Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa siku hiyo hiyo katika Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yatafuatiwa na Mkutano wa pamoja kati yake na Mhe. Membe na Waandishi wa Habari (Press Conference).

Akiendelea na ziara yake, Mhe. Steinmeier atatoa hotuba na kujadiliana masuala mbalimbali na Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya Kituo cha Mafunzo ya Sheria cha Afrika Mashariki kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani(TGCL) katika Ukumbi wa Nkrumah uliopo chuoni hapo.

Vile vile siku hiyo hiyo ya tarehe 25 Machi, 2014, Mhe. Steinmeier ataitembelea Kampuni ya STRABAG iliyopo Ubungo, Dar es Salaam. Kampuni hii kutoka Ujerumani inajishughulisha na ujenzi wa Barabara za Mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam. Akiwa eneo hilo Mhe. Steinmeir atakutana na Waziri wa Ujenzi, Mhe. John Magufuli pamoja na Wawakilishi wa Makampuni ya Ujerumani yaliyopo hapa nchini.

Akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa kuondoka nchini, Mhe. Steinmeier atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu kuhusu masuala ya Uwindaji haramu wa wanyamapori Afrika Mashariki.


IMETOLEWA NA: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.

24 MACHI, 2014

No comments: