Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba, Sammuel Sitta amesema kuwa analo jibu la
matumizi ya Kura ya Siri na Wazi katika kufanya maamuzi ndani ya vikao
vya Bunge Maalum la Katiba. Akiongea na baadhi ya wadau wakiwemo
waandishi wa habari mara baada ya kuchaguliwa kwake, Sitta amesema kuwa
kura zote za Siri na Wazi zitatumika kutegemeana na aina ya maamuzi
yanayotakiwa kufanywa. Mathalan amesema kuwa katika kupitisha vifungu
kama Tunu za Taifa, ni wazi kuwa kura ya Wazi ndiyo itakayotumika.
Aidha, kwa upande wa vifungu vingine ambavyo ni nyeti na vitazua
mivutano bungeni, ni wazi kuwa kura ya Siri ndo itatumika katika kufanya
maamuzi. Ingawa hakubainisha vifungu hivyo shindani, naamini kuwa hata
suala la Muundo wa Muungano litaamuliwa kwa kura ya siri.
Hakika
Sitta ameonesha njia katika hili kwani mapendekezo yake yamejaa busara
za hali ya juu na ni imani yangu kuwa hata ile mivutano iliyojitokeza
awali itaisha. Pongezi ziwaendee Kamati ya Mashauriano ambayo inaendelea
kutafuta muafaka juu ya jambo hilo. Naamini kuwa aliyoongea Mwenyekiti
yametokana na kazi nzuri inayofanywa na kamati hiyo.
Katika
gazeti la mwananchi linaeleza kwa kina habari ya mh. Sitta na pia
unaweza kuisoma kwa makini kupitia blog hii, Habri ii inaanza kwa kusema
Mwenyekiti
Mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amezungumzia uwezekano
wa kutumia kura ya siri katika kuamua ibara nyeti katika Rasimu ya
Katiba.
Sitta
aliyechaguliwa juzi kushika wadhifa huo, alisema atashirikiana na
kamati ya uongozi itakayoundwa ya wenyeviti wa Kamati 15 za Bunge hilo
na kamati ya ushauriano kupata jawabu la suala hilo.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu nyumbani kwake mjini Dodoma juzi, Sitta
alisema: “Unajua kuna baadhi ya vifungu na ibara za Rasimu ya Katiba ni
vizuri vipigiwe kura ya wazi na vingine ambavyo ni nyeti zaidi vipigiwe
kura ya siri.”
Alisema si vizuri vifungu vyote vipigiwe kura sawa, yaani si lazima zote ziwe za siri au ziwe za wazi.
Alitoa
mfano wa ibara inayosema kutakuwa na Mahakama Kuu ya Tanzania na
kusema: “Hatuwezi kushindana katika suala la kuwapo kwa Mahakama na ni
wazi kuwa jambo hilo mnaweza kupiga kura ya wazi. Nasema hivyo kwa
sababu Katiba yoyote lazima ionyeshe mihimili yote ambayo ni Bunge,
Serikali na Mahakama.”
Sitta
ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alishinda kiti
hicho katika uchaguzi uliofanyika juzi kwa kura 487 kati ya 563 (sawa na
asilimia 85).
Mbunge
huyo wa Urambo Mashariki ambaye kaulimbiu yake ni ‘kasi na viwango’,
alisema vifungu na ibara za Rasimu ya Katiba vinavyoweka misingi ya
Katiba, ni vizuri vikapigiwa kura ya siri.
“Unajua
tuna viongozi wa dini na halitakuwa jambo la busara kama tukizijua
hisia zao. Kama wewe uko karibu na imamu au askofu halafu anapiga kura
ya wazi ya kutaka Serikali tatu wakati wewe muumini unataka Serikali
mbili ni wazi kuwa jambo hilo linaweza kuleta hisia tofauti na kuwanyima
watu haki na uhuru wa kuamua,” alisema Sitta.
Alitoa
mfano wa Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba inayozungumzia Serikali na
muundo wa madaraka katika Jamhuri ya Muungano na kufafanua kuwa katika
sura hiyo atapendekeza ipigiwe kura ya siri.
Kuhusu
suala hilo la muundo wa Serikali alisema: “Kikubwa ni wajumbe kujenga
hoja, hatuwezi kwenda na misimamo isiyobadilika kwa sababu tunataka
maridhiano. Nitatenda haki na nitatoa muda mrefu zaidi kwa wajumbe
kujadili sura ya kwanza na ya sita ambazo zina uzito mkubwa kuliko sura
nyingine ambazo ni za maelezo tu. Mfano suala la haki za binadamu ambazo
wote tunakubaliana nazo.”
Alisema
wakati wa kujadili muundo wa Serikali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ukifika, ataishauri kamati ya uongozi, kutenga muda wa ziada
katika suala hilo na mengine yenye utata.
Mwenyekiti
huyo alisema suala la upigaji kura linatakiwa kuamuliwa kwa busara na
atatumia hekima zake na za wajumbe wa Bunge hilo, kutatua mgogoro wa
kura ya siri au ya wazi.
Wakati
wa kujadili rasimu ya kanuni za Bunge hilo, kulizuka mvutano mkali
katika vifungu vya 37 na 38 vinavyozungumzia aina ya kura itakayopigwa
wakati wa kufanya uamuzi na kulazimika kuviweka kando. CCM kimekuwa
kikinadi kura ya wazi kikisema ni ya haki huku wapinzani wakitaka kura
ya siri.
Hata
hivyo, kamati ya muda iliyoandaa kanuni za Bunge hilo, ilipendekeza
kuwa Bunge Maalumu ndilo litakaloamua aina ya kura itakayopigwa.
Akizungumzia
suala hilo Sitta alisema: “Pamoja na kuwapo kwa hali hiyo, lazima
ifikie wakati tuamue. Hatuwezi kuwa na kanuni ambazo hazielekezi namna
ya kupiga kura kwa sababu upigaji wa kura unaweza kuanza kufanyika wiki
ya kwanza tu baada ya kuanza kujadili Rasimu ya Katiba.”
Samia Makamu Mwenyekiti
Wakati
huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia
Suluhu Hassan jana alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo
baada ya kumshinda mpinzani wake, Amina Abdallah Amour.
Akitangaza
matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi, Dk Thomas Kashililah alisema kati
ya kura 523 zilizopigwa, Suluhu alipata kura 390 sawa na asilimia 74.6,
Amina kura 126 sawa na asilimia 24.1. Kura saba ziliharibika.
Kukamilika
kwa uchaguzi huo kunafungua milango kwa Yahya Hamad Hamis kuapishwa
kuwa Katibu wa Bunge la Katika na Dk Thomas Kashililah kuwa Naibu Katibu
kwa mujibu wa sheria.
Makatibu
hao wataapishwa leo saa nne asubuhi na Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu
ndogo ya Dodoma. Baada ya kuapishwa, Katibu atawaapisha Sitta na Samia
katika Ukumbi wa Bunge kuanzia saa 10 jioni leo.
Awali
wakati wakijieleza Amina alizua gumzo baada ya kueleza kuwa licha ya
kuwa na watoto watano, ameachika na kwa sasa hana mume.
“Mimi
ni mama wa watoto watano, nina shahada ya uzamili ya masuala ya fedha,
nina stashahada ya sheria na nimefanya kazi katika Benki ya Biashara kwa
miaka 23 ila kwa bahati mbaya nimeachika,” alisema na kusababisha
wajumbe kuangua kicheko.
Baada
ya kuchaguliwa, Suluhu alisema: “Nitafanya naye (Sitta) kazi kwa
ushirikiano na uadilifu mkubwa. Pia ninawaahidi wajumbe wote kuwa
nitawapa ushirikiano.”
Mbowe amuonya Sitta
Wakati
huohuo; Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtumia salamu za
pongezi Sitta huku akimtaka kuachana na masilahi ya chama chake.
“Ningependa
kutuma salamu kwa Samuel Sitta ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu la Katiba, nataka aelewe kuwa alichokabidhiwa ni majukumu
si cheo,” alisema na kuongeza:
“Mamilioni
ya Watanzania watakuwa wanamfuatilia na kumtazama kwa makini mno… maana
wananchi kwa sasa wanajua mchakato wa Katiba Mpya umebeba matumaini ya
Taifa lao kwa miaka 50 hadi 100 ijayo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment