MAJIBU/MAELEZO YA PINGAMIZI LILILOWEKWA NA BWANA FABIAN L.SKAUKI
DHIDI YANGU MIMI MATAYO M.TORONGEY MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE
KUPITIA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA).
UTANGULIZI
Kwa mujibu wa ibara ya 67 (1) ya Katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania (1977) inaeleza wazi kuwa ili mtu ateuliwe kuwa mgombea ubunge ni lazima awe na sifa zifuatazo;
Kwa mujibu wa ibara ya 67 (1) ya Katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania (1977) inaeleza wazi kuwa ili mtu ateuliwe kuwa mgombea ubunge ni lazima awe na sifa zifuatazo;
(i)-Awe raia wa Tanzania
(ii)-Awe ametimiza umri wa miaka ishirini na moja
(iii)-Awe anajua kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza
(iv)-Awe ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa
(v)-Awe hajatiwa hatiani na mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa
kodi yoyote ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe
ya Uchaguzi.
Aidha, Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (2) na -(3) -ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania 1977; hata kama mtu ana sifa zote za kugombea -hataruhusiwa kugombea Ubunge kama :
(i)-Ni raia wa nchi nyingine; au
(ii)-Kwa mujibu wa Sheria iliyotumika katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imethibitishwa rasmi kwamba mtu huyo ana ugonjwa wa akili; au
(iii)--Amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na
kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda usiozidi miezi
sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa,
linaloambatana na utovu wa uaminifu; au
(iv)-Katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu
amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana
na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa
Umma; au
(v)-Siyo mwanachama na siyo Mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa; au
(vi)-Ikiwa mtu huyo ana maslahi yoyote katika mikataba na serikali ya
Jamhuri ya Muungano au serikali ya mapinduzi Zanzibar wa aina yoyote
aliyowekewa miiko maalumu kwa mujibu washeria iliyotungwa na Bunge, na
iwapo amekiuka miiko hiyo; au
(vii)-Ameshika madaraka ya Afisa Mwandamizi katika utumishi wa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa madaraka ambayo Rais anaweza au
anatakiwa kukabidhi kwa Mbunge kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano, au sheria iliyotungwa na Bunge; au
(viii)-Kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayoshughulikia makosa
yanayohusika na uchaguzi wa aina yoyote, mtu huyo amezuiliwa
kuandikishwa kama Mpiga kura au kupiga kura katika uchaguzi wa Wabunge.
(ix)-Ni mgombea Urais /Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, kwa mujibu wa masharti kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kifungu cha 5.3 kimeweka masharti ya Uteuzi wa Mgombea Ubunge na kuweka kama ifuatavyo;
Aidha, kwa mujibu wa masharti kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kifungu cha 5.3 kimeweka masharti ya Uteuzi wa Mgombea Ubunge na kuweka kama ifuatavyo;
(i)-Awe amedhaminiwa na wapiga kura wasiopungua ishirini na tano waliojiandikisha kupiga kura katika Jimbo hilo.
(ii)-Mgombea haruhusiwi kujidhamini yeye mwenyewe
(iii)-Awe na dhamana ya shilingi 50,000/=
(iv)-Awe ametoa tamko la kisheria mbele ya hakimu kwamba anazo sifa zinazotakiwa ili kugombea Ubunge
Vilevile, kwa mujibu wa masharti kwa vyama vya siasa na wagombea
uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya
uchaguzi kifungu cha 6.0 kimeweka utaratibu wa Pingamizi dhidi ya uteuzi
wa Mgombea Ubunge:
Na Kifungu cha 6.3, kimeweka sababu za kuweka Pingamizi kuwa ni:
(i)-Maelezo yaliyopo katika fomu ya uteuzi hayatoshi kumtambulisha Mgombea;
(ii)-Fomu ya Uteuzi haitimizi au haikuwasilishwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sharia;
(iii)--Kutokana na maelezo yaliyoandikwa katika fomu ya uteuzi ni dhahiri kwamba Mgombea uchaguzi hana sifa zinazotakiwa;
(iv)-Uthibitisho wa Msimamizi wa Uchaguzi unaopaswa kutolewa haukutolewa; (v)-Mgombea hana sifa zote zinazotakiwa;
(vi)-Hakuna uthibitisho kuwa Mgombea amelipa dhamana ya shilingi elfu hamsini (50,000/=); na
(vii)-Hakuna picha ya Mgombea.
(viii)-Mgombea hakujaza fomu Na.10 kuthibisha kuwa ataheshimu na kutekeleza maadili ya Uchaguzi.
Baada ya utangulizi huo hapo juu ambao unaonyesha dhahiri kuwa hapakuwa
na sababu yoyote ya mimi kuwekewa pingamizi na Mgombea ubunge wa Chama
cha CUF, kwani hakufuata masharti ya Katiba, Sheria na maelekezo
yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kwetu kama wagombea, kwani
aliamua kutunga mambo ambayo yapo nje ya utaratibu na hayakidhi haja,
hayakufuata Katiba, matakwa ya kisheria na hata maelekezo yaliyotolewa
na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Nayasema yote haya kutokana na ukweli kuwa mimi nimekidhi sifa zote za
kuwa Mgombea Ubunge na nimetimiza masharti yote yaliyowekwa kwa mujibu
wa Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na barua yako ya tarehe -13 Machi, 2014
yenye kumbukumbu namba HWB/E.50/21/76-nalazimika kujibu pingamizi hilo
kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya Uchaguzi sura Na.343 kifungu Na.40
(5)-kuhusu pingamizi,-hata kama halina nguvu kwa mujibu wa katiba,
sheria na maelekezo ya Tume ya taifa ya uchaguzi hoja kwa hoja kama
ifuatayvo. -
MAJIBU YA HOJA ZA PINGAMIZI LA FABIAN LEONARD SKAUKI:
1.-HOJA YA KWANZA;-Kwamba mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimejaza
taarifa za uongo kwenye fomu zangu kuwa kazi ninayoifanya ni BIASHARA na
kusema kuwa ni taarifa za uongo kwa kuwa sikuweka vielelezo vya
kuonyesha kuwa mimi ninafanya kazi hiyo, na kuwa sijulikani ninafanya
kazi gani .
MAJIBU YA HOJA YA KWANZA : Pingamizi na sababu zilizotolewa na Mgombea wa chama cha wananchi CUF Bwana Fabian L.Skauki hazina mashiko na kuwa yeye ameamua kukupotosha kuwa mimi sio mfanyabiashara kwa kuwa sikuweka vielelezo, japo ni wazi kuwa sikupaswa kuweka vielelezo vyovyote kwani fomu haikuwa inanitaka kuweka vielelezo vya aina yoyote kama ambavyo hata yeye hakuweka vielelezo kuwa anafanya shughuli gani. Ninasikitika kuwa hata wewe Msimamizi umekubaliana na hoja hii dhaifu ya pingamizi na kunitaka mimi kuijibu wakati unajua wazi kuwa haina mshiko wala mantiki kwa mujibu wa sheria za uchaguzi. Naambatanisha leseni yangu ya Biashara yenye jina langu namba B.No. 01299270-iliyotolewa tarehe 19/09/2011 na huo ni uthibitisho kuwa mimi ni mfanya biashara (kielelezo A) -
MAJIBU YA HOJA YA KWANZA : Pingamizi na sababu zilizotolewa na Mgombea wa chama cha wananchi CUF Bwana Fabian L.Skauki hazina mashiko na kuwa yeye ameamua kukupotosha kuwa mimi sio mfanyabiashara kwa kuwa sikuweka vielelezo, japo ni wazi kuwa sikupaswa kuweka vielelezo vyovyote kwani fomu haikuwa inanitaka kuweka vielelezo vya aina yoyote kama ambavyo hata yeye hakuweka vielelezo kuwa anafanya shughuli gani. Ninasikitika kuwa hata wewe Msimamizi umekubaliana na hoja hii dhaifu ya pingamizi na kunitaka mimi kuijibu wakati unajua wazi kuwa haina mshiko wala mantiki kwa mujibu wa sheria za uchaguzi. Naambatanisha leseni yangu ya Biashara yenye jina langu namba B.No. 01299270-iliyotolewa tarehe 19/09/2011 na huo ni uthibitisho kuwa mimi ni mfanya biashara (kielelezo A) -
2.-HOJA YA PILI: Kwamba, mimi Mathayo Torongey sijui kusoma wala
kuandika Kiswahili au Kiingereza, na kwamba nimedanganya na hivyo sina
sifa za kuwa Mgombea Ubunge.
MAJIBU YA HOJA YA PILI; Kwanza,-nieleze wazi kuwa nimesikitishwa sana na
tuhuma hizi ambazo zina lengo la kunichafua mbele ya jamii na Taifa kwa
ujumla, zina lengo la kuichafua jamii ya watanzania kutoka familia za
wakulima na wafugaji, watu ambao wana kipato kidogo na ambao wanaishi
vijijini kuwa ni watu wa hovyo na hawajui kusoma wala kuandika, ni
tuhuma za kuwadhalilisha watanzania ambao ni kutoka jamii za wananchi wa
vijijini wanaotafuta fursa ya kuchaguliwa kwamba ni watu wa wanaoomba
nafasi wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, kwa kweli nasikitika sana
kwa hili na lilikuwa tusi ambalo msimamizi wa uchaguzi hukupaswa
kulipokea. Aidha, nashindwa kutoa ushahidi hapa kwani hata wewe
umeziamini tuhuma hizi kuwa mimi sijui kusoma wala kuandika na ndio
maana ukanitaka nizijibu, japo ni ukweli ulio wazi kuwa sahihi yangu
kwenye fomu haikuwa ya "kuweka dole gumba" niliweka sahihi kwa kuandika
na mbele yako na sikuandikiwa.
Pili;-Yafaa mgombea huyu pamoja na wale wote waliomtuma wakatoa ushahidi
wake kwako kuwa mimi Mathayo Mang'unda Torongey-sijui kusoma wala
kuandika, na hii itamsaidia kuaminika mbele ya jamii ya wananchi wa
Chalinze ambao anataka kuwaongoza. Hata hivyo naomba nitoe majibu mbele
yako kwa maandishi na kwa kusoma kitu ambacho wewe utataka nisome na
kuandika ili uwe uthibitisho kwako kuwa najua kusoma na kuandika .
3.-HOJA YA TATU: Kwamba, mimi Mathayo Torongey nimedanganya kwa
kughushi/kufoji sahihi za wadhamini walionidhamini kuwa Mgombea -na kuwa
sahihi zote zimefojiwa na hazifanani na zile zilizokuwepo kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuwa sahihi zote hizi zimesainiwa na
mtu mmoja ambaye sio mhusika .
MAJIBU YA HOJA YA TATU: Kwanza, nieleze wazi kuwa nilipokamilisha kujaza
fomu zangu na kudhaminiwa na wadhamini 25 kwa mujibu wa sheria ,
nilikuja ofisini kwako na tukakagua kwa pamoja majina ya wadhamini wote
waliokuwepo kwenye fomu zangu na nilikuja na shahada zote za wapiga kura
ambao walinidhamini na wewe ulizikagua na kuridhika kuwa walikuwa ni
wapiga kura sahihi na saini zao zilikuwa sahihi na uliandika hilo kama
uthibitisho wako kwenye fomu zangu za uteuzi na ndio maana uliniteua
kuwa mgombea .
Pili,-Namshangaa mweka Pingamizi kwa kuja na tuhuma kuwa saini za wapiga
kura zinatofautiana na saini zilizoko kwenye Daftari la kudumu la
wapiga kura ,hii ni kutokana na ukweli kuwa kwenye Daftari la kudumu la
wapiga kura hakuna saini za wapiga kura isipokuwa saini zipo kwenye
vitambulisho vya wapiga kura, na vitambulisho hivyo niliviwasilisha
kwako na wewe kama msimamizi wa uchaguzi baada ya kukagua vitambulisho
hivyo uliridhika kuwa saini za wadhamini wangu zilikuwa sahihi na ndio
maana uliniteua kuwa Mgombea na kuweka "uthibitisho wako" katika
kifungu-F.-kwa maandishi kwenye fomu zangu za uteuzi. Naomba kunukuu
maelezo yako uliyoyaandika kwenye fomu yangu ya uteuzi tarehe 12.03.2014
saa 9.05 Alasiri kama ifuatavyo ‘(i) Nimekagua majina yote ya
waliomdhamini mgombea aliyetajwa hapa naninathibitisha kwamba wote
wameandikishwa kuwa wapiga kura katika Daftari la kudumu la wapiga kura
katika Jimbo la Chalinze'
Tatu,-Mweka pingamizi anatakiwa kuthibitisha kwako kuwa saini hizo
zimeghushiwa kwani ni ukweli ulio wazi kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi
yetu kughushi ni kosa la Jinai na hivyo ushahidi wake huo unaweza
kuwasilishwa mbele ya vyombo vya dola kwa hatua zaidi.
Nne,-mweka pingamizi ana wajibu wa kuthibitisha kuwa saini hizo
zinafanana zote kwani ni ukweli uliowazi kuwa saini za wadhamini wangu
hazifanani kutokana na kuwa wapo wadhamini ambao waliweka "dole gumba"
kuthibitisha saini zao na wengine walisaini kwa maandishi, sasa kufanana
anakosema ni kwa aina gani? Kwamba alama ya dole gumba ina fanana na
saini ya kuandika?!
Tano,-yafaa mweka pingamizi na wale wote ambao walishirikiana naye
kuweka hoja hii katika pingamizi hili kujitokeza na kueleza kwa uwazi
lengo la kuweka pingamizi hili ambalo ni la kutungwa na lenye nia ovu
dhidi yangu, Chama changu na Wananchi wote wa Jimbo la Chalinze.
4.-HOJA YA NNE Hoja ya mweka pingamizi iliyonihusu mimi Mgombea wa chama
cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ilidai kuwa nimeshindwa kutimiza
mahitaji ya kisheria ya kuwa na wadhamini wasiopungua 25, badala yake
nimedhaminiwa na wadhamini 28 ambao kati yao wadhamini 7 sio wapiga kura
halali wa jimbo la CHALINZE, na kwamba Taarifa zao na namba zilizojazwa
hazifanani. Hivyo nabakiwa na wadhamini halali 21 ambao kisheria
hawatoshi kutimiza matakwa ya kisheria. Majina ya wadhamini hao ambao
hawakidhi matakwa ya kisheria na namba zao kutajwa kuwa ni:- 1. HABIBU
ALLY SAIDI - 16886275 2. MOHAMMED RAMADHANI - 30376567 3. ABDULKADIR
ALLY - 49264905 4. SHABANI SULEYMAN - 16984045 5. JUMA MRISHO - 48759563
6. RAJABU ALLY - 16872368 7. MANENO MIRAJI - 16872059 MAJIBU YA HOJA YA
NNE (4).
Mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimekidhi vigezo na masharti ya
wadhamini wote 25 wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria kama nilivyo
orodhesha kwenye fomu ya wadhamini na hivyo basi pingamizi namba nne
lililowekwa na mgombea ubunge wa chama -cha The Civic United Front (CUF)
Kuwa Bwana HABIBU ALLY SAIDI mwenye namba 16886275 kuwa sio mdhamini
halali, nikiri kuwa ni kweli sio mdhamini wangu halali; Mdhamini wangu
halali ni Bwana HABIBU ALLY DAUDI-mwenye namba --16886275.
Na vilevile ni kweli kwamba Bwana MOHAMMED RAMADHANI mwenye ‘30376567'
si mdhamini wangu halali, Mdhamini wangu halali ni Bwana MOHAMMED
RAMADHANI mwenye namba 30576567. Pia napenda kukuthibitishia bila chembe
ya shaka kuwa Bwana ABDULKADIR ALLY-mwenye namba 49264905-aliyezaliwa
wilaya ya Bagamoyo tarehe 17/04/1974 ni mdhamini wangu halali aliye
andikishwa tarehe 02. 03. 2010 kwenye kituo cha shule ya msingi Mkoko
kata ya Msata halmashauri ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Hata hivyo amesema Bwana SHABANI SULEYMAN mwenye namba -16984045 si
mdhamini wangu halali, Napenda kuthibitishia kuwa mdhamini wangu halali
ni Bwana SHABANI SELEMANI-mwenye namba 16984045 -na si Bwana SHABANI
SULEYMAN.
Hata hivyo, nadhibitisha kuwa Bwana -JUMA MRISHO-mwenye namba 48759563,
aliyesema sio mdhamini wangu halali ni halali kwani amezaliwa tarehe
04.04.1981 wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa kijiji cha Msinune
halmashauri ya Bagamoyo mkoa wa Pwani na shahada yake ya kupigia kura
imeandikishwa kwenye kituo cha shule ya msingi Msinune, hivyo ni
mdhamini wangu halali na amekidhi vigezo vya kunidhamini sawa na Bwana
RAJABU ALLY-mwenye namba 16872368-aliyezaliwa tarehe 28.09.1979 wilaya
ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa kijiji cha Kiwangwa mkoa wa Pwani naye ni
mdhamini halali aliyejiandikisha kwenye kituo cha Kibaoni ofisini; Kama
ilivyo kwa mdhamini halali Bwana MANENO MIRAJI-mwenye namba 16872059
aliyezaliwa wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa mkoa Pwani na
kaandikishwa kituo cha Kibaoni Ofisini.
Muweka pingamizi angekuwa sahihi Kama ningekuwa sijatoa uthibitisho kwa
msimamizi wa uchaguzi. Hoja yake ingekuwa na uzito unao bebwa na kifungu
6.3 (iv) kwenye kitabu cha tume ya taifa ya uchaguzi cha maelekezo kwa
vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa urais, ubunge na madiwani
kinasema, "Uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi unaopaswa kutolewa
haukutolewa".-Lakini kwenye fomu namba 88 F ukurasa 8, -"UTHIBITISHO WA
MSIMAMIZI WA UCHAGUZI" -msimamizi wa uchaguzi kwenye F( i) amekiri
kukagua na kuthibitisha ya kuwa wadhamini wote walioandikishwa kuwa
wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura katika jimbo la
CHALINZE ni halali. - Kwa maana hiyo, udhibitisho wa msimamizi wa
uchaguzi ni kwamba wadhamini wangu ni halali hivyo hoja ya muweka
pingamizi kwenye swala la wadhamini haina mashiko na msimamizi wa
uchaguzi hakupaswa kupokea pingamizi hilo bali alipaswa kulitupa kabla
ya kufikiria kulileta kwangu. Hata hivyo, nichukue fursa hii adhimu
kumuelimisha muweka pingamizi wa chama cha wananchi CUF (Civic United
Front) ya kuwa majina yanaweza kufanana kwenye kituo kimoja au kituo
kingine -ama kata nyingine au wilaya na mkoa mwingine lakini namba ya
kadi halali ya mpiga kura haiwezi kufafana na kadi ya mpiga kura
mwingine halali, kwa mfano kwenye kituo 00006347 kata ya Bwilungu jimbo
la CHALINZE wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani mpiga kura HAMZA
ATHUMANI-mwenye shahada namba 17023223--anafanana jina na HAMZA
ATHUMANI-mwenye shahada namba 1702107-sawa na Bwana BONELA SHABANI
MADEGA-mwenye shahada namba 19534653-na BONELA SHABANI MADEGA-mwenye
shahada namba 19525475. Hawa wote wakitazamwa kwa majina kwa jicho la
muweka pingamizi wa CUF wataonekana ni mtu mmoja au ni mapacha wakati
uhalisia ni watu tofauti wanao tofautishwa na namba za shahada zao
halali za kupigia kura.
5.-HOJA YA TANO. Kuwa Mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimedanganya Uraia
wangu na kuwa mimi sio Mtanzania wa kuzaliwa -kwa kuwa sikuweka
vielelezo vyovyote halali.
MAJIBU YA HOJA YA TANO . Napenda kurudia kuwa huenda mweka pingamizi
ameamua kukupotosha na kuandika taarifa za uongo kwa lengo ambalo yeye
na wale wote waliomtuma wanalijua wao. Napenda kurudia kuthibitisha kama
nilivyoandika kwenye fomu zangu za kuomba uteuzi kuwa mimi ni mzaliwa
wa Kijiji cha Kaloleni katika Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro nchini
Tanzania . Naomba kuweka kielelezo -"B" kuthibitisha uraia wangu wa
Kuzaliwa kama ifuatavyo;
1.-Naweka nakala ya kitambulisho changu cha kuandikishwa kuwa mpiga kura
katika Jimbo la Ubungo chenye namba *46670962*.-Na kwa mujibu wa sheria
ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 ,kifungu cha 10 (1) ‘sifa na kukosa
sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura na kupiga kura' kinasomeka
‘Hakutakuwa na mtu zaidi ya raia wa Tanzania ambaye ametimiza umri wa
miaka kumi na nane na ambaye hajapoteza sifa kwa masharti ya Sheria hii
au sheria nyingine yoyote ya Bunge atakayestahili kuandikishwa kuwa
mpiga kura kwa mujibu wa masharti ya sheria hii' Hivyo kwa kuwa
nimekidhi vigezo vya kuwa mpiga kura ,mimi ni raia halali, naambatanisha
nakala ya shahada yangu ya Mpiga kura kama kielelezo ‘C'.
- Aidha, ukisoma majibu ya tume ya taifa ya uchaguzi kuhusu mapingamizi
yaliyowekwa na wagombea wa CHADEMA dhidi ya uraia wa wagombea wa CCM
Sioi Sumari-2012-na Godfrey Mgimwa 2014 -katika majimbo ya Arumeru
Mashariki na Kalenga ,Tume iliamua kuwa jukumu la kuthibisha /kutoa
vielelezo kuhusu tuhuma za uraia wa mgombea ni kwa mtoa tuhuma (who
allegies-must prove), hivyo mweka pingamizi atakiwe -kuwasilisha
vielelezo vya tuhuma zake kwako ili kuthibitisha madai yake kuhusu uraia
wangu.
HITIMISHO. Baada ya maelezo tajwa hapo juu na uthibitisho ambao
nimeuwasilisha kwako naomba kukujulisha kuwa mimi nina sifa zote kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mgombea halali
wa ubunge jimbo la Chalinze na yafaa ukatupilia mbali pingamizi
lililowekwa dhidi yangu kama jinsi ambavyo ulipaswa kulitupilia mbali
kabla hujalileta kwangu kwani lilikosa sifa na vigezo vya kuwa
pingamizi. -
…………………………………
Mathayo Mang'unda Torongey
Mgombea Ubunge wa CHADEMA jimbo la CHALINZE.
14 Machi, 2014.
No comments:
Post a Comment