Baadhi ya wananchi wa Namanyere wilayani Nkasi wakichangia damu katika siku ya uzinduzi wa siku ya Utepe mweupe.
MTANDAO wa Utepe Mweupe na Uzazi Salama (White Ribbon Allience for Safe
Motherhood) umekemea vikali tabia zinazofanywa na baadhi ya watumishi wa
hospitali na vituo vya afya ya kuuza damu ambayo kimsingi inatakiwa
kutolewa bure kwa wahitaji. Kauli hiyo ya pamoja imetolewa jana wilayani
Nkasi na wanaharakati wa mtandao huo walipokuwa katika hafla ya
uzinduzi wa wiki ya Utepe Mweupe wilayani hapa, mkoani Rukwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ‘Evidence for Action’ ambao
wanatekeleza mradi ujulikanao kama ‘Mama Ye’, Craig John, alisema
wamepata malalamiko toka kwa wananchi ya kuwa kuna tabia ya baadhi ya
watendaji kwenye sehemu za kutolea huduma za afya huwauzia wagonjwa damu
kitu ambacho hakikubaliki.
“...Wakati tunapita pita mitaani kuhamasisha wananchi kuja kujitolea
damu kwa ajili ya akinamama wajawazito wanaohitaji kuongezewa damu,
wananchi walituambia kuwa baadhi ya watendaji wa afya wamekuwa kero kwao
kwani wanawauzia damu pindi wanapokuwa wanaihitaji,” alisema Craig.
Naye Mratibu wa Utepe Mweupe nchini, Bi. Rose Mlay aliitaka serikali
kutenga bajeti mahususi katika mwaka wa fedha 2014/2015 ili kuhakikisha
vituo vya afya wanatoa huduma za dharura ikiwemo upasuaji na damu
salama.
“...kama mtoto amekaa vibaya tumboni kwa mama au hata kama amepigwa
mwanamke huyu anaweza kusaidiwa kwa kufanyiwa upasuaji na kuongezewa
damu salama pekee, hivi ndivyo vitakavyo muokoa,” alisema Rose.
Sherehe za kilele cha Wiki ya Utepe Mweupe zinatarajiwa kufanyika Machi
15, 2014 wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, ambapo mgeni rasmi
anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Idd Kimanta akiwa na Mkurugenzi wa Evidence for
Action, Craig John wakiwa kwenye viwanja vya Sabasaba ambapo mamia ya
wananchi walijitolea damu.
No comments:
Post a Comment