
Kocha mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic.
Na John Joseph
TABIA ya ukali uliopitiliza, kutoa lugha kali inawezekana ikawa ni chanzo cha Kocha Zdravko Logarusic kuendelea kukwaruzana na wachezaji wake, ambapo sasa habari kamili ni kuwa, wengi wao hawana amani wanapocheza chini ya kocha huyo.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Loga ambaye ni kocha wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya, ameendeleza ukali wake na kutoa lugha kali kwa wachezaji wake huku akiwaambia hawana hadhi ya kuichezea timu hiyo, vitendo ambavyo awali viliwahi kuripotiwa lakini safari hii ameenda mbali kwa kuamua kupiga mateke ovyo vitu mbalimbali katika vyumba vya kubadilishia nguo.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo kimelithibitishia gazeti hili kuwa, wachezaji hawampendi kocha huyo na inawezekana ndiyo maana wanashindwa kucheza kwa kiwango cha juu kutokana na hofu kubwa kila wanapofanya makosa.
“Huyu Loga sidhani kama atakuwa na maisha marefu, anatutukana sana, kuna wakati inafikia mtu unacheza ukiwa na hofu, yaani sasa hata kama ni ukali basi yeye amepitiliza,” alilalama mchezaji mmoja.
Chanzo kingine kikaliambia gazeti hili: “Mfano katika ile mechi ya Mbeya, wakati wa mapumziko alipofika vyumbani akaanza kupiga mateke madumu ya maji na kila kilichopo mbele yake, akawa anabwatuka hovyo, akawatukana wachezaji, mara anawaambia hawana uwezo wa kuichezea Simba, uwezo wao ni kucheza timu kama Ashanti.
“Badala ya kutoa maelekezo kutokana na mchezo ulivyokuwa, yeye akawa anatukana tu mwanzo-mwisho, yaani hata kama ni hasira, zile zake zimepitiliza, wachezaji hawana amani kabisa, hawapendi kufanya naye kazi na sijui kama atadumu muda mrefu, hasa ukizingatia kuwa timu ina matokeo mabaya.”
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alikuwa na haya ya kusema: “Utaratibu uliopo na ambao pia Loga anautumia ni kuwa, viongozi hawatakiwi kuingia kwenye vyumba wakati wa mapumziko, hilo ni suala la kiufundi.
“Labda kama ungenitajia wachezaji waliokwambia juu ya tukio hilo ningeelewa, lakini uongozi hatujapata taarifa rasmi au malalamiko yoyote juu ya Loga. Siwezi kujibu taarifa ambazo ni tetesi, tutakapobaini ukweli tutalifanyia kazi.”
No comments:
Post a Comment