ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 22, 2014

WAPINZANI WAIPINGA HOTUBA YA KIKWETE

Wenyeviti wa vyama vya upinzani nchini, kutoka kushoto ni James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF).
Dodoma.
Wenyeviti wa vyama vya Upinzani vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha NCCR-Mageuzi, jana usiku walikutana ili kutoa kauli ya pamoja, kutokana na hotuba ya ufunguzi wa Bunge kwa maelezo kuwa tayari Rais amevuruga mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.

Wakati viongozi hao wakikutana, Mwenyekiti wa Chama cha DP Mchungaji, Christopher Mtikila alisema, Rais ameingilia mchakato na kutoa maelezo jinsi ya kuandika Katiba.

Wakizungumza na gazeti hili jana mara baada ya hotuba hiyo, Freeman Mbowe, James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba, walisema wameipokea kwa masikitiko makubwa hotuba hiyo.

“Tunakwenda kujadili hotuba ya Rais na tutatoa msimamo wetu,” alisema Mbowe.

Awali Katibu wa muda wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Julius Mtatiro alisema Rais Jakaya Kikwete amevuruga mchakato wa Katiba, kwani walitarajia angetumia mamlaka yake kama Rais kuwaunganisha.

“Rais tulitarajia angeongea kama mkuu wa nchi, lakini amezungumza kama Mwenyekiti wa CCM na kutoa msimamo juu ya muundo wa Muungano jambo ambalo hatukulitegemea,” alisema Mtatiro.

Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni sawa na mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato mzima.

Hofu ya kuvunjika Bunge
Wakizungumza nje ya Bunge, baadhi ya wajumbe wameeleza kuwa hotuba ya Rais Kikwete kama ikitekelezwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya utakuwa mgumu.

Mjumbe Luhaga Mpina alisema kwa jinsi rasimu ilivyoandikiwa na kama muundo wa serikali mbili ukipita basi rasimu ya Katiba itabidi iandikwe upya.

“Rasimu yote imetengenezwa kwa mfumo wa serikali tatu sasa hapa kuna hatari ya Bunge kukwama ,” alisema.

Mtatiro kwa upande wake alisema sasa kuna hofu ya kushindwa kupatikana Katiba Mpya kwani Rais amewachanganya wajumbe na kama watapitisha maoni yake itabidi rasimu kuandikwa upya.

Mjumbe Mustapha Akoonay, alisema upatikanaji wa katiba upo shakani kwani sasa upinzani utakuwa mkubwa juu ya muundo wa muungano.

“Kwa sasa nadhani itabidi turudi upya kwa wananchi kupata kura ya maoni juu ya muundo wa muungano,” alisema.

Lucy Owenya alisema Rais amegeuza mkutano wa Bunge kuwa ni mkutano wa Chama Cha Mapinduzi, kwani ameshindwa kabisa kutoa mwelekeo wa nchi na badala yake ametoa msimamo wa CCM.

“Kutokana na hili, naamini kabisa Bunge halitakuwapo na ni bora iwe hivyo kwa kuwa amejibu hotuba ya Warioba na kwa maana hiyo amepingana na mawazo ya wananchi.”

Godbles Lema alisema kuwa Rais hakuja kuhutubia taifa bali alikuja kufanya semina na kujibu hotuba ya Warioba.

Mjumbe huyo ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini alionyesha shaka kuwa baada ya muda wa wiki tatu hakutakuwa na Bunge la Katiba kwa kuwa wako baadhi ya watu ambao hawatakubali kilichofanywa na Rais Kikwete.

“Waliochukua fedha ni vyema wakaenda kumalizia nyumba zao kwa kuwa kiongozi wetu amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafurahisha wanaCCM lakini kwa Watanzania hatutakubali,” alisema Lema.

John Cheyo alisema, “Mimi ninachokiona ni maridhiano tu, suala la kufumua rasimu halinipi shida kwa kuwa vitu vyote vinavyoletwa bungeni huwa ni mali ya Bunge na hivyo tutafanya tunavyoona sisi inafaa.”

Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuwa kosa kubwa ambalo lilifanywa na upinzani ni kukubali na kuruhusu Jaji Warioba atangulie kuwasilisha rasimu yake akasema hilo ndilo lililowagharimu.

Alitaka Bunge livunjwe mara moja ili warudi kwa wananchi wakaamue na kuwahukumu kutokana na kile ambacho walikifanya katika Bunge ambalo kwa maoni yake wamekula fedha za walipa kodi bure.

Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa aliipongeza hutuba ya Rais Jakaya Kikwete ya uzinduzi wa Bunge la Katiba.

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge la Katiba, alisema kwa kifupi hotuba ya Rais Kikwete ni nzuri. Lowassa alitoa kauli hiyo, wakati akitoka nje ya Bunge, muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza hotuba ya uzinduzi wa Bunge hilo.

Naye Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mchungaji Ernest Kadiva, alisema hotuba ya Rais imetoa mwanga kwa wajumbe.

“Rais ameonyesha upungufu wa hoja mbalimbali hasa katika mfumo wa serikali tatu na sasa ameacha kazi ya kuamua tuwe na mfumo wa serikali mbili au tatu ni ya wajumbe,” alisema Mchungaji Kadiva.

Hata hivyo, mjumbe mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema Rais alizungumza kama si mkuu wa nchi bali Mwenyekiti wa CCM kwa sababu amesimamia hoja za chama chake.

Alisema hata kama mapendekezo ya Rais Kikwete yatatekelezwa, kamwe hayatakuwa mwarobaini wa muungano. Mbunge wa Mwibara, Khangi Lugora alisema hotuba hiyo waliitarajia na ndio maana kulikuwa na ubishi wa nani atangulie kati ya Jaji Joseph Warioba na yeye kwa mujibu wa kanuni.

“Hotuba ilikuwa ikijaribu kumjibu Jaji Warioba na kwangu mimi nilikuwa naona kuwa Rais naye alikuwa anachangia katika kuitunga Katiba kwa kupitia hotuba yake hiyo. Tumeyasikia na sisi tutakwenda kutafakari katika kutunga Katiba ambayo itakuwa ya Watanzania wote,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Mkiwa Kimwanga, alisema kilichofanyika ni Rais kwenda kutoa uamuzi juu ya mchakato uliokuwa ufanywe na Bunge hilo.

Kwa upande wake, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hakuitendea haki Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba Bunge hilo haliwezi kutengeneza Katiba ambayo inalenga katika mfumo wa serikali la mbili.

“Itakuwa ni vigumu zaidi kupata Katiba Mpya, alikuwa anapinga mambo ya msingi yaliyoelezwa katika rasimu ya kwanza. Hayo angeyaeleza katika hatua ya awali ili rasimu hiyo ibadilishwe na si katika hatua hii ya mwisho kabla ya kwenda kupigiwa kura na wananchi,” alisema.

Alisema ndani ya siku 70 haiwezekani kubadili rasimu hiyo ambayo imejikita katika muundo wa serikali tatu kwenda katika muundo wa serikali mbili.

Ezekiah Olouch alitahadharisha wajumbe wenzake kutodharau maoni ya wananchi waliyoyatoa katika rasimu hiyo ya pili.

Alisema haiwezekani tume zote ambazo zimeundwa kuangalia aina ya muundo wa serikali zije na jibu moja kuwa namna ya kuimarisha muungano ni kuwapo kwa serikali tatu.

Jussa Ismail Ladu alisema kwa ufupi kwamba hotuba ya Rais Kikwete imekuwa yenye sura ya CCM zaidi.

Naye Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi, aliielezea hotuba ya Rais kuwa imeibua mambo mengi ambayo baadhi ya watu walikuwa wakiyaelewa tofauti, hivyo imeweka uelewa mzuri katika baadhi ya maeneo.

Profesa Costa Mahalu alisema ni hotuba ambayo imewaachia changamoto, hasa katika eneo la muungano kwa sababu wanahitajika kuunda muungano usiotetereka.
Chanzo: Mwananchi.

3 comments:

Anonymous said...

Kwanza niseme kuwa siko affiliated na chama chochote cha siasa nchini.
Kwa kifupi sioni tatizo la hotuba ya Raisi ambayo kwa mtazamo wangu nimeiona kama imewapa watu mwanga wa kuziona issues zinazojadiliwa kwa mapana zaidi kuliko ambavyo awali wengi walikuwa wanaburuzwa na hoja bila kujua undani wake.na zaidi Raisi alicho lishauri bunge nikufanya maamuzi wakitafakari kila hoja kwa marefu na mapana.Tatizo hapo liko wapi?

Anonymous said...

Tukiweka siasa pembeni, alichosema Rais Kikwete ni kweli kwamba serikali ya Muungano kama inavyopendekezwa katika rasimu ya pili ya katiba itakuwa powerless, toothless, and all you can call it. Huwezi kuwa na serikali isiyo kuwa na full taxing authority. Serikali kama hiyo ni sawa na quasi-governmental entities kama vile UN, AU, EU, n.k., ambazo zinaendeshwa kwa michango ya wanachama na zinategemea goodwill ya wanachama wake. Hili lazima lipatiwe ufumbuzi kama kuna utashi na nia nzuri ya kuwa na Muungano wa serikali tatu. Vinginevyo, this will be the beginning of the end of the Union.

Anonymous said...

Kwa maoni yangu ni kuwa, hotuba ya Mhe. Rais imeonesha hana umiliki wa zao la Tume aliyoiunda mwenyewe! Na hali hii siyo ya kwanza kwa mtazamo wa Maraisi wanaounda Tume zote zilizotangulia kama ile ja Jaji Kisanga! La Msingi ni kuwa Tume hii ya Jaji Warioba imeonesha ilikuwa huru kabisa na aliyeiteuwa! Maoni ya Tume ni msingi wa yaliyotokanana Wadau wakuu ambao ni Wenye NCHI!Kimasingi Katiba siyo zao la viongozi bali Wananchi! Kama serekali tatu imekosa miguu, kazi ya Bunge Maalum ni kuipatia miguu imara ili iwepo kwani sasa ni hitaji la Kisheria wala si la matakwa tu ya Kisiasa! Kwa hatua Zanzibar ilipofikia ya kuwa na Katiba yao inayotambua Utaifa wao na uwepo wao kama Nchi kamili (Autonomy) hakuna budi iwepo Nchi nyingine Kamili iliyoungana nao, na si kusema wanaunganana "Muungano"kisha watake haki zao kutoka kwa 'Marehemu' Tanganyika! Hofu kubwa aliyoisema Mhe. Rais ni kuwa Tanganyika ikifufuka itaimeza Zanzibar! Wabunge kazi kwenu!