Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta na makamu wake, Samia Suluhu Hassan, wameapishwa kushika nyadhifa zao jana, huku Sitta akiahidia kuwapatia Watanzania Katiba bora zaidi.
Sitta na mwenzake waliapishwa na Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad, majira ya saa 10: 24 na baadaye mwenyekiti huyo mpya aliwaapisha Pandu Ameir Kificho na kufuatiwa na Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda na viongozi wengine kwa kuzingatia nyadhifa zao. Ingawa alisema jana haikuwa siku ya hotuba, lakini Sitta alitumia muda huo kumshukuru Kificho aliyekuwa mwenyekiti wa muda kwa kazi kubwa ya kuliongoza bunge kutunga kanuni ambazo zitatumika kuendesha kikao hicho cha Bunge Maalum.
“Nimejifunza mengi toka kwa Kificho, nimejifunza namna ya kuendesha mkutano mkubwa bila kanuni. “Tulikuwa hatuna kanuni, baadhi yetu tulikuwa tukifanya vituko vya kila aina, lakini sasa tuna kanuni.
“Yale mambo ya kuwasha tu kipaza sauti na kuanza kuzungumza bila ruksa, mtanisamehe na kunionea bure, nitakuwa makini kwa hilo kutoruhusu,” alisema.
Pia alisema amejifunza toka kwa Kificho jinsi alivyowateua baadhi yao kuwa wajumbe wa kamati ya kanuni, alikuwa makini sana kuwapata wajumbe makini. (Kamati ya Kanuni ilikuwa chini ya uenyekiti wa Profesa Costa Ricky Mahalu (MJ) ).
“Nami nitawachukua na kuwapanga kwenye kamati kwa kuzingatia umakini na umahiri wao,” alisema.
Akimkaribisha kuchukua nafasi yake kwenye kiti, Kificho, alisema, “pamoja na utamu wa kiti hiki, sasa nachukua nafasi ya kumwita Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge Maalum ambaye ameapishwa hivi punde aje achukue kiti chake.”
Mapema akisoma taarifa yake, Kificho, aliwapongeza mwenyekiti na makamu wake ili Mwenyezi Mungu azidi kuwabariki ili shughuli hiyo iliyo mbele yao iwe na baraka.
“Falsafa yako ya kasi na viwango itaweza kufanikisha upatikanaji wa Katiba bora kwa wakati,” alisema.
Aliwataka kuifanya hivyo kwa kuzingatia azma na maslahi ya kitaifa na siyo kikanda na maslahi ya watu au kikundi cha watu binafsi.
Akizungumzia kazi aliyokuwa akiifanya kuanzia alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa muda Februari 18, mwaka huu, hadi jana alipomaliza muda wake, Kificho, alisema haikuwa rahisi hata kidogo.
Alisema sasa hivi kazi hiyo vikao vya bunge hilo vitakuwa vikiendeshwa kwa kuzingatia kanuni za bunge zitakazosimamia upatikanaji wa mchakato wa katiba.
“Kazi hii haikuwa rahisi hata kidogo kwa sababu kila mjumbe alikuwa na imani na msimamo wa kundi lake alilokuwa akiliwakilisha,” alisema.
Alisema kazi iliyopo mbele yao bado ni ngumu lakini ana imani kuwa chini ya falsafa ya viwango na kasi ya mwenyekiti wa kudumu, itawezesha kufanikisha upatikanaji wa Katiba bora.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kuapa, Sitta alisema wanatarajia kutumia siku tatu kuanzia jana, leo na kesho ambapo wataapa hadi saa 3 usiku.
Awali alimwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kutengua kanuni za bunge hilo ili kutoa muda zaidi wa kuapa hadi saa 3 usiku badala ya kuishia saa 2 usiku, shughuli ambayo ilianza kufanywa tangu jana.
Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge hilo, Hamad, shughuli ya kula kiapo ilianza kwa viongozi wakuu na kufuatiwa na watu wenye mahitaji maalum, halafu mawaziri (ili waweze kuondoka leo kwenda kwenye shughuli zingine za kitaifa za maandalizi ya Bajeti ya Serikali hapo Mei na Juni mwaka huu).
Mwishowe alisema utaratibu utakaotumika kwa wajumbe wengine ni kuapa kwa kufuata alfabeti zao.
Kwa mujibu wa Sitta, shughuli za kuapa zinatakiwa zimalizike kesho Jumapili na kuanzia Jumatatu, wajumbe watakuwa na siku tatu za mjadala wa jumla kuhusu malengo na mwelekeo wa majukumu waliyopewa.
Pia alisema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba anatarajiwa kuwasilisha bungeni Rasimu ya pili ya Katiba, kuanzia saa 10 jioni siku ya Jumatatu na Jumanne au Jumatano Rais Jakaya Kikwete atakuja kuongea nao.
“Jumatatu au Jumanne kama mambo yatakwenda vizuri, Rais Kikwete atakuja kuongea nasi, kwani alikwishazindua Bunge Februari 18, mwaka huu, kwa Tangazo la kuitisha Bunge Maalum,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment