
Beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (katikati), akijaribu kupiga kichwa mbele ya mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Mussa Mgosi, huku David Luhende pia wa Yanga akiwa tayari kumsaidia wakati timu hizo zilipokutana raundi ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Cairo, Misri. Baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na Al Ahly ya Misri, Yanga sasa wamepania kupoza machungu yake kwa Mtibwa Sugar Jumamosi ijayo.
Yanga imewasili Dar es Salaam alfajiri ya leo wakitokea Cairo baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 na Al Ahly na sasa kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm amesema akili yake yote ipo katika kuhakikisha wanatetea ubingwa Ligi Kuu.
Kocha Pluijm alisema baada ya kuondolewa katika michuano hiyo sasa akili ni moja tu kuhakikisha tunashinda kila mechi ya ligi kuu iliyo mbele yao.
Pluijm, alisema tayari ameshawaambia wachezaji wake kusahau kila kitu kuhusu matokeo ya Ahly ambapo sasa wanatakiwa kuhakikisha wanafanya vizuri katika ligi wakianzia katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
“Tunatakiwa kusahau kila kitu sasa kuhusu haya matokeo na tunarudi nyumbani (Tanzania) tukiwa na akili moja ya kutaka kutetea taji la ubingwa wetu. Hilo nimeshawaambia wachezaji wangu tunatakiwa kulinda heshima yetu kwa kuchukua ubingwa, sioni wa kutuzuia kwa uwezo tulionao sasa,” alisema Pluijm.
Yanga wanarejea katika ligi wakiwa nafasi ya tatu pia wako nyuma kwa pointi mbili kwa vinara Azam (40), na michezo mitano mkononi. Endapo itashinda mechi hizo itafikisha pointi 53, wakati Azam nayo ikishinda mechi nne itafikisha pointi 52.
Wakati Simba kama watashinda mechi zake zote tano itakuwa
na pointi 51, huku Mbeya City yenyewe wakiwa nafasi ya tatu na pointi 49 kama itashinda mechi zote tano itamaliza ligi ikiwa na pointi 54.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment