ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 26, 2014

Azam yamshutumu Mkwasa

Nahodha wa zamani wa Azam,Aggrey Morris
Nahodha wa zamani wa Azam, Aggrey Morris amemlaumu kocha msaidizi wa Yanga Chares Boniface Mkwasa kwa kuwa na wivu wa mafanikio dhidi ya timu nyingine.

Akizungumza na Nipashe jijini mwishoni mwa wiki, Morris alisema Azam ilistahili kutwaa ubingwa wa Bara msimu huu kutokana na maandalizi mazuri ya miaka mitatu.

Ingawa mchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars, Morris hakumtaja Mkwasa kwa jina, alisema wote wanaowaponda ni wale wasiokubali kushindwa na wenye dhana kuwa hakuna bingwa wa Bara nje ya timu za Simba na Yanga.

Mkwasa ni mmoja wa watu walionukuliwa wakiiponda Azam kuwa ni bingwa wa 'mizengwe'. Inakuwa klabu ya tisa kunyakua ubingwa huo tangu mwaka 1965.

Hata hivyo, baada ya kunyakua taji hilo kumekuwa na kauli za kejeli dhidi ya mafanikio ya Azam ambayo ilipanda daraja mwaka 2008.

Morris, alisema mashabiki wa soka walipaswa kuipongeza Azam kwa kuonyesha ushindani wa kweli na kuweza kuzisimamisha Simba na Yanga zilizotwaa taji hilo kwa jumla ya miaka 42.

Alisema hata timu nyingine zinaweza kuwa bingwa kama zikijipanga.

"Nadhani wanaofanya hivyo wanasumbuliwa na wivu wa mafanikio yetu na pia kushindwa kuamini kuwa nje ya Simba na Yanga bingwa anaweza kupatikana tena kwa kuweka rekodi kama wao," alisema.

Alisema anaamini kuwepo kwa Mbeya City kunaweza kuongeza chachu iliyoanzishwa na Azam ili kuifanya ligi iwe ya kusisimua zaidi.

Morris, alisema pamoja na kauli za kejeli dhidi ya Azam, timu hiyo inaendelea kufurahia ubingwa wake na kwamba inajipanga kuendelea kutamba nchini kwa muda mrefu zaidi ya msimu huu.

Aidha, Morris alisema Azam imepania kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ili kuondoa kasumba ya timu za Bara kuwa wasindikizaji kwenye Ligi ya Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
CHANZO: NIPASHE

No comments: