Majeneza yenye miili ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani waliofariki dunia baada ya kugongwa na basi wakati wakipima ajali usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Utaho wilani Ikungi mkoa wa Singida kabala ya kuagwa na kusafirishwa kwenda makwao. Picha na Gasper Andrew
Singida/Pwani. Watu 19 wakiwamo askari polisi wanne wa Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Singida wamekufa papo hapo baada ya kugogwa na basi la Sumry lililokuwa linatoka Kigoma kwenda Dar es Salaam.
Wengi waliofariki katika ajali hiyo, iliyotokea juzi saa tatu na nusu katika Kijiji cha Utaho, Tarafa ya Ihanja mkoani Singida, ni wa ukoo mmoja wa Bulali.
Watu hao pamoja na wanakijiji wenzao, wakiwamo sita waliojeruhiwa, walikuwa wamekusanyika kando ya barabara kushuhudia ajali iliyotokea awali, ambayo mwendesha baiskeli alikuwa amegongwa na lori na kufariki dunia papo hapo. Katika mkusanyiko huo, ndipo basi hilo lilipowapitia na kukatisha maisha yao.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema miongoni mwa waliouawa, wapo waliokuwa wakikata majani kuweka barabarani ili kutoa ishara kuwa kuna ajali katika eneo na askari hao walikuwa hapo kuchunguza ajali hiyo ya awali.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Joseph Malunda alisema miili ya marehemu iliyofikishwa katika hospitali hiyo ilikuwa imeharibika vibaya, baadhi ilikatika viungo mbalimbali kama shingo, miguu, mikono na nyingine utumbo na ubongo ulimwagika nje.
“Hadi jana mchana, miili yote ya marehemu ilikuwa imetambuliwa na kuchukuliwa na gari la halmashauri ya Ikungi tayari kwa mazishi,” alisema.
Dk Malunda alisema miili ya askari hao wanne ilikuwa bado katika chumba cha maiti katika hospitali hiyo ikitarajiwa kusafirishwa baada ya maandalizi kukamilika.
Kamanda wa Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alisema baada ya basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Paul Njilo mkazi wa Dar es Salaam kukanyaga watu hao, halikusimama hapohapo, badala yake alikimbia na kwenda kulitelekeza baada ya kilomita 25 katika Stendi Kuu ya Utaho na kukimbilia kusikojulikana.
Kamanda Kamwela alitaja majina ya askari waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni; F.849 D/CPL Boniface Magubika wa Ofisi ya CID Wilaya ya Singida ambaye ni mwenyeji wa Kihesa mkoani Iringa.
Mwingine ni F.6837 PC Jumanne Mwakihaba wa Kikosi cha FFU Singida, mwenyeji wa Kisarawe, Pwani, G.7993 Novatus Tarimo wa Ofisi ya RTO mwenyeji wa Rombo -Kilimanjaro na G.8948 Michael Mwakihaba wa FFU Singida, ambaye ni mwenyeji wa Mbalizi, Mbeya.
Kamanda Kamwela aliwataja marehemu wengine ambao wametambuliwa kuwa ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Utaho, Ramadhani Mjengi, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Paul Hamisi na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Utaho, Ernest Salanga.
Miili mingine iliyotambuliwa ni ya Saidi Rajabu, Usirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhani, Mwinyi Hamisi na Issah Hussein.
Alisema miili ya wakazi wengine ambayo haijatambuliwa imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha Hospitali ya Mkoa mjini Singida.
Kamanda huyo alisema utaratibu ulikuwa unafanyika kuwasaidia abiria wa basi hilo kupata gari jingine kuendelea na safari ya Dar es Salaam, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
Mashuhuda
Mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida, Mussa Mohamed (31) aliyeumia kifuani na mguu wa kulia alisema ajali hiyo ilimkuta alipokuwa na wenzake wakikata majani kuweka ishara ya ajali ya awali na hakujua kilichoendelea hadi alipojikuta hospitalini.”
Shuhuda wa ajali hiyo, Ramadhani Ally alisema ajali ya awali ilimhusisha mwendesha baiskeli, Jaredi Zephania (24), mkazi wa Kijiji cha Minyinga ambaye aligongwa na lori na kufariki dunia hapohapo alipokuwa akitoka kusaga nafaka.
Alisema baada ya ajali hiyo, askari walipigiwa simu na kwenda kupima na kuchukua mwili wa marehemu kabla na wao kukutwa na janga hilo.
Diwani wa Kata ya Mungaa, Matheo Max alisema baada ya kijana huyo kugongwa, kundi la watu wa kijiji hicho, walifika eneo la tukio kwa ajili ya kushuhudia.
Alisema wakati upimaji ukiendelea, polisi walikuwa wameegesha gari lao, upande wa pili wa barabara ambao basi hilo lilikuwa lipite na kwamba dereva wa gari hilo ambaye pia ni askari aliyekuwa kwenye usukani, alilimulika basi hilo kwa taa kali.
“Inawezekana dereva wa basi alihisi ni majambazi akalitoa barabarani na kwenda nje ambako ndiko alikokutana na kundi la watu wakiwamo askari hao na kuwagonga,” alisema.
Max alisema baada ya tukio hilo, askari waliosalimika walikimbilia kusikojulikana na kuacha gari lao pamoja na funguo.
“Nilimpigia simu RCO aturuhusu kutumia gari la polisi kuwahisha majeruhi hospitali, lakini hata hivyo hakuwa tayari,” alisema diwani huyo.
Alisema majeruhi sita wamelazwa katika Hospitali ya Puma wakiwa na hali mbaya.
55 wanusurika Chalinze
Abiria 55 waliokuwa wakisafiri kwa basi, mali ya Kampuni ya Hood kutoka mkoani Mbeya kwenda Arusha juzi walinusurika kifo huku baadhi ya mizigo yao ikiteketea baada ya gari hilo kupata hitilafu na kuwaka moto.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni katika Kijiji cha Makole Kata ya Mbwewe, Barabara Kuu ya Chalinze - Segera basi hilo lilipokuwa likienda Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ulrich Matei alisema basi hilo lilipasuka gurudumu la mbele na dereva alijitahidi kulinusuru lisipinduke lakini baada ya kusimama ghafla lilishika moto ambao ulisambaa kwa kasi na kuliteketeza kabisa.
Abiria waliokuwamo kwenye basi hilo walitoka kupitia mlango wa kawaida na ule wa dharura bila kupata majeraha makubwa.
Imeandikwa na Gasper Andrew na Awila Silla (Singida) Julieth Ngarabali (Kibaha).
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment