MARAFIKI zangu naamini mpo sawa na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku salama kabisa. Kwa upande wangu, mambo ni mazuri na nimejiandaa kikamilifu kuwapatia mada nzuri kila siku kwa ajili ya kuboresha uhusiano wetu.
Leo somo letu linafikia ukingoni baada ya kudumu hapa kwa wiki tatu. Kwa bahati mbaya, wiki iliyopita sikuwepo uwanjani, nilipata dharura kidogo. Leo tunaendelea.
Nimeshafafanua mengi na kujenga hoja thabiti kuhusu namna ambavyo kijana mwenye elimu na mafanikio anavyokuwa katika wakati mgumu wa kupata mwenzi sahihi.
Nilifafanua kuwa mwanamke anavutika na vitu viwili kwa mwanaume; uanaume wake kiasili na mafanikio yanayotokana na mwanaume mwenyewe na namna anavyojituma.
Ikiwa mwanamke amekutana na mwanaume akiwa tayari ana mafanikio yake, anaweza kushawishika na fedha zake na akaonyesha kila dalili kuwa amempenda kwa dhati lakini ndani ya moyo wake kukawa hakuna mapenzi ya dhati.
Mwanamke wa namna hiyo ni rahisi na hodari wa kuigiza mapenzi zaidi ya yule ambaye amempenda mwanaume kiasili kwa kuwa tu amevutika naye kama mwanaume. Mambo ya mafanikio huja baadaye. Ni sifa za ziada.
YUPI SAHIHI?
Mwanamke anayekupenda kiasili ndiye mwenye penzi la dhati na nafasi kubwa katika maisha yako ya ndoa. Hakuna majaribio katika ndoa, lazima mnaoungana humo muwe kweli na penzi la dhati.
Ikiwa unaye mwanamke wako ambaye mlipendana tangu zamani, kabla hujawa na kitu/mali au kazi nzuri, huyo kwa asilimia kubwa, huwa sahihi zaidi.
Hata hivyo, wapo baadhi ambao mnaweza kukutana ukiwa tayari na mafanikio yako na ndoa ikawa yenye amani lakini kwa kuzingatia mambo kadhaa. Tutaona baadaye hapa chini.
ANGALIA HAPA
Tatizo linalotokea baada ya kuoana na mwanamke ambaye kumbe hakukupenda wewe isipokuwa mafanikio yako ni usaliti. Kwa kuwa hakuwa na mapenzi na wewe ni wazi kuwa atatafuta mwingine kwa ajili ya kumtuliza moyo wake.
Mifano ipo mingi; hujawahi kusikia mke wa mtu ambaye yupo kwenye ndoa halafu anarudiana na mwanaume wake wa zamani ambaye alikutana naye chuo?
Mambo haya yanatokea sana, kwa sababu bado anamkumbuka mwanaume huyo kwa namna alivyompenda kwa dhati, hata kama hampi kitu, kwa sababu tu moyo wake umeridhika naye, anaweza kurudi kwake na kuiacha ndoa yake.
Usaliti ni sumu ya kwanza ya wanandoa wanaokutana mmoja wao akiwa hana pendo la kweli kwa mwenzake.
UNATAKA KUOA?
Hebu tulia; kuoa si kukurupuka. Unaingia kwenye mkataba wa maisha na mtu. Si jambo la pupa. Lazima uwe makini kabla ya kuingia kwenye muunganiko huo.
Mwanamke sahihi zaidi ambaye anafaa ni yule ambaye ulipendana naye ukiwa huna kitu. Huyo alikupenda wewe kwa pendo la asili na si mali zako.
Inawezekana tayari umeshafanikiwa kimaisha na unataka kuoa, hakikisha unaposaka mwanamke wa kuoa, usijitape kuhusu cheo, nafasi yako kazini au fedha zako.
Usionyeshe kuwa una mafanikio makubwa kimaisha. Mwache mwanamke akukubali jinsi ulivyo badala ya kutumia mali kama chambo cha kumpata mwanamke huyo. Wengi hukosea katika eneo hili, hufikiri kujionyeshea mali na fedha ndiyo kumpata mwanamke kirahisi.
Ni kweli, unaweza kumpata kirahisi zaidi ukitumia njia hiyo, lakini je, upo tayari kugeuzwa benki?
UMESHAOA TAYARI?
Kwa msingi huo, mwanaume ambaye tayari ameshaoa mwanamke aliyekutana naye akiwa amesha fanikiwa, anatakiwa kumuacha? Hapana.
Kuna vitu vingi vya kufanya kwa ajili ya kujenga upendo.
Watu wengi wakishaingia kwenye ndoa hujisahau, hawana muda na familia zao tena. Jambo hilo siyo sahihi. Jenga upendo wa ziada kwa mwenzako. Fanya vitu ambavyo vitamfanya akuone wewe mwanaume sahihi na wa kipekee kwake.
Ni vizuri kuwa naye karibu na kusikiliza hisia zake kuhusu matatizo yake binafsi na hata ya familia yake. Kinachowezekana kufanyika, jitahidi kukifanya, ikitokea umeshindwa basi zungumza naye vizuri na umweleweshe.
Ni mambo yanayowezekana kwa kujengwa katika msingi wa masikilizano ndani ya nyumba.
Hadi wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
GPL
No comments:
Post a Comment