Kubwa zaidi, nilieleza umri ambao ni sahihi zaidi kwa vijana kwa maana ya uwezo wa akili na utayari wa kuingia kwenye muunganiko wa ndoa na kuachana na ujana.
Ndoa ina raha yake, lakini lazima iwe kwa muda na mtu muafaka. Kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya kutamani tu, kunaweza kusababisha kuanzisha maisha mapya ya dhiki na mateso ya moyo.
Wiki iliyopita, nilimalizia mada iliyowalenga zaidi wanawake na namna wanavyopotezewa muda wao kwenye uhusiano wa muda mrefu na baadaye kuachwa kwenye mataa. Naamini nilieleweka vizuri.
Leo nina kitu kipya kabisa, lakini kwa sababu wiki iliyopita nilimaliza mada inayowahusu wanawake, leo nitazungumza na wanaume zaidi. Wanaume wengi hubabaika sana baada ya kufikia umri wa kuoa.
Suala la uchaguzi wa nani anafaa kuwa mke huwa tatizo kubwa sana wakibaki njia panda na kukosa maamuzi sahihi. Wakati hilo likiwasumbua wengi, kuna wengine hutumia muda mrefu kuwa masomoni na baadaye kuanza kazi, kisha kutafuta wake sahihi wa kuoa.
ELIMU
Ukweli ambao wengi wanaweza kupingana nao ni kwamba, mtu anavyozidi kusoma, upeo wake kuhusu mpangilio wa maisha na mambo mengine hubadilika. Mawazo yake yatafanana zaidi na namna ya elimu yake ilivyo.
Kukutana na watu wengi wenye tabia tofauti pia huchagia kumbadilisha mtu kutoka kwenye tabia yake ya awali na kuwa wa tofauti. Kwa maana hiyo ni lazima afikirie kuoa mwanamke mwenye elimu kama yake, mrembo sana n.k kulingana na mabadiliko aliyoyaona wakati akiwa masomoni.
MAFANIKIO
Mwanaume mwenye mafanikio anaweza kuingia kwenye mtego wa kumjua mwanamke mwenye mapenzi ya kweli. Kutokana na mafanikio yake, anaweza kupata mwanamke ambaye atakuwa amevutiwa zaidi na mafanikio yake na si penzi la dhati.
Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, baadhi ya wanaume wakishakuwa na mafanikio, huwaacha wenzi waliokuwa nao kabla ya mafanikio. Mathalani mwanaume amekuwa kwenye uhusiano na mwanamke kwa takribani miaka mitano, akiwa hana kitu kabisa, akishapata kitu kikubwa humsahau mwenzake.
Labda nisisitize kuwa, tafiti hazisemi wanaume wote bali baadhi tu. Wengine wanaweza kujitahidi kuendelea nao lakini si kwa mahaba kama yaliyokuwa awali.
HUJAONA?
Vipi katika watu wanaokuzunguka hujawahi kuona mtu ametoka mbali na mwanamke wake lakini baada ya mafanikio anamuacha? Hao wapo wengi sana. Angalia hata watu maarufu, baadhi wana tabia hiyo.
Kinachowasumbua ni fikra kwamba, hao si watu wanaoendana nao tena baada ya mafanikio jambo ambalo si la kweli. Hili halipo kwa wanaume pekee, hata wanawake nao wapo baadhi wenye mtindo huu.
UKWELI NI HUU
Mtaalamu mmoja aliwahi kuandika: “Kadiri unavyozidi kusoma na unavyozidi kufanikiwa kiuchumi na kimaisha ndivyo ugumu wa kumpata mke mwema unavyozidi kuongezeka. Hii ni kwa sababu unapomchumbia binti hutaelewa kuwa amekupenda wewe ama amevutiwa na mafanikio yako.”
Hapo ina maana kuwa, kwa kuwa tayari utakuwa upo kwenye mafanikio ni vigumu kujua upendo wake wa ndani. Je, hiyo humaanisha wenye mafanikio wasioe au hawatakuwa na uwezo wa kutambua penzi la dhati? La hasha!
Bado kuna mambo zaidi ya kujifunza marafiki zangu, lakini nafasi yangu ni ndogo. Kwa leo tuishie hapa, wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
GPL
No comments:
Post a Comment