ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 29, 2014

HESHIMU NAFASIYA MWENZAKO KWENYE MAPENZI


MAPENZI ni sanaa yenye wigo mpana sana. Unahitajika uwe mbunifu ili uweze kuendelea kuwa bora kwa mpenzi wako kila siku.

Lazima uwe mtafutaji wa kitu kipya ili uweze kuwa wa tofauti kwa mwenzako.Huwezi kuwa yuleyule, ikiwa hivyo maana yake utakinaiwa. Naam! Love & Life ni safu nzuri kwako kwa ajili ya kuongeza maarifa na kukufanya uendelee kuwa bora zaidi kwa mpenzi wako.

Rafiki zangu, nataka kuzungumzia mada moja muhimu sana. Nazungumza na wale wenzangu ving’ang’anizi. Ni suala linalowasumbua wengi.

Mtu anajua kabisa kwamba mtu anayemshawishi awe wake, tayari ana mpenzi wake, inakuwaje hapo?
Nimepata kesi nyingi sana za aina hiyo. Mwanamke anamtaka mwanaume ambaye ana mchumba wake au mume kabisa. Upande wa pili nao, mwanaume anamtaka mke wa mtu au mpenzi wa mtu.

Maana yake ni nini sasa?
Mbaya zaidi, mwingine anaambiwa wazi kwamba ana mtu wake, lakini bado anang’ang’ania, inasababishwa na nini? Haya ndiyo ambayo ninakwenda kuzungumza nanyi. Kwa nini unashindwa kuheshimu nafasi ya mwingine?
MALI ZA WATU VIPI?
Marafiki zangu asikudanganye mtu, mume/mke wa mtu sumu! Fanya ujanja wako uwezavyo, jifanye mhuni unavyoweza lakini si tabia njema kutoka na mtu ambaye ana mwenza wake.

Kwanza jiulize, kama ingekuwa ni wewe ungejisikiaje? Ukisikia mkeo anatoka na mwanamke mwingine utajisikiaje? Au pengine umeolewa, halafu ukasikia au kupata uhakika kuwa mume wako anatoka na mwanamke mwingine utajisikiaje? Achana na hilo, unajiweka kwenye hatari kubwa, mwenye mali atakapogundua.

WALIO KWENYE UHUSIANO
Katika hali ya kawaida kabisa, unawezaje kumtaka mtu ambaye tayari unajua kuwa ana mtu wake? Busara hapo iko wapi?Ukijichunguza kwa makini lazima utagundua kwamba una tatizo.

Mtu ambaye tayari ana mpenzi wake, maana yake ni kwamba amefika; kitendo cha kumtongoza, kinaonesha ni kwa kiwango gani umejaa tamaa ambazo ndizo zinazokuongoza, maana kwa busara huwezi kumtaka mtu ambaye ana mpenzi wake.

Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba, kuna wengine wanaambiwa wazi kuwa wana watu wao, lakini ndiyo kwanza mtu anaendelea kulazimisha, tena akitoa ahadi kedekede ili ampate. Huo ni ujinga usio na maana.

HEBU JIFUNZE!
Kwa bahati mbaya, wanapokutana wote wa ‘hovyo’ wanajikuta wameingia kwenye mapenzi. Hebu jiulize wewe ambaye umeingilia penzi la mtu, akili yako inafanya kazi sawasawa kweli? Unawezaje kuingia kwa mtu ambaye tayari ana wake? Kuna vitu kadhaa vya kujifunza hapa.

Lazima utambue kuwa huyo ambaye amekukubali wakati ana wake, maana yake hana penzi la dhati.
Si ajabu akiwa nawe, akatafuta kuwa na mwingine pembeni yako!

Hekima iko wapi? Kuna tatizo gani kusubiri mwingine ambaye atakuwa wako peke yako?
Lazima uwe na msimamo katika maisha yako.

Siyo sifa kuwa na wapenzi wengi au kuingia kwenye uhusiano wa mwingine. Unadhani mwenzako anaumia kwa kiasi gani? Vipi kama na wewe ukija kuingiliwa na mtu mwingine? Unahitaji kutulia na kuijua thamani yako, ni sifa njema kuwa na mwenzi wako peke yako bila kuchangia na mwingine.

Hilo litawezekana kama nawe utaacha tabia ya kuingilia uhusiano wa wengine. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.

GPL

No comments: