Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimtunuku Nishani ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano Daraja la Kwanza Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia alikuwa Mwenyekiti Tume ya kurekebisha Katiba Mhe. JajiJoseph Sinde Warioba wakati wa Sherehe hizo zilizofanyika katika ukumbi wa mikutano ikulu jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Nishani ya Kuuenzi Muungano aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete, haina uhusiano wowote na yaliyomo katika Rasimu ya Katiba.
Jaji Warioba alisema hayo alitakiwa kueleza furaha yake baada ya Rais Kikwete kutambua mchango wake kwa Taifa na kuamua kumtunuku nishani hiyo Jumamosi iliyopita Ikulu.
“Sikupewa nishani ile kwa sababu ya mchakato wa Katiba. Nishani ile inahusu miaka 50 ya Muungano, msihihusishe na mchakato wa Katiba,” alisema.
Jaji Warioba ambaye amewahi kulieleza gazeti hili kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipendekeza muundo wa serikali tatu kwa ajili ya kuunusuru Muungano, alisema baadhi ya wananchi wamelitafsiri suala hilo kisiasa.
Alisema kuwa tume yake ilipendekeza muundo wa serikali tatu kutokana na maoni yaliyotolewa na wananchi na kusisitiza kuwa jambo hilo haliwezi kuhusishwa na nishani aliyopewa.
“Rasimu ya Katiba imekusanya maoni ya wananchi na ndiyo maana tume ikapendekeza muundo ule. Sasa suala hili lisihusishwe na nishani kwani ni vitu viwili tofauti,” alisisitiza.
Wakati akipewa nishani hiyo, Jaji Warioba alisifiwa kuwa ni mmoja wa viongozi waliouenzi Muungano kupitia nyadhifa mbalimbali alizoshika wakati akiwa mtendaji mwandamizi wa Serikali.
Tangu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikabidhi Rasimu yake Desemba 30 mwaka jana, imekuwa ikipingwa kila kona na makundi mbalimbali hasa la wanaCCM ambao wanapigia debe muundo wa serikali mbili.
Baadhi ya viongozi wa chama hicho wamekuwa wakitamka wazi kuwa muundo wa serikali tatu unaopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba ni tishio kwa uhai wa Muungano.
Mtizamo kuhusu muundo huo pia ulizua msuguano katika Bunge Maalumu la Katiba kutokana baadhi ya wajumbe wake kutoa lugha za kejeli na kuudhi kwa Jaji Warioba, wakidai kuwa ni msaliti.
Mwananchi
1 comment:
Asante Vijimambo kwa mchango uno saidia wasomi kuwa na sauti,haki ya maoni. Hongera Jaji Warioba kwa Tuzo. Nina penda kushirikiana na wananchi pamoja na Rais Kikwete kwa pongenzi ya kazi na mchango wako kwenye Tume ya Katiba Mpya. Poleni Gazeti la Habarileo kuvunja maktaba na wasomaji wasiweze kuweka maoni.
Post a Comment