Advertisements

Friday, April 18, 2014

Kaimu Mkurugenzi TANESCO Mbaroni kwa matumizi mabaya ya Ofisi!

ALIYEKUWA Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Robert Semtutu, na wenzake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh.milioni 200.
Washtakiwa wengine ni pamoja na aliyekuwa Afisa Ugavi wa Tanesco, Hanin Mahambo, Mkurugenzi wa fedha Lusekeo Kasanga, Mwanasheria Godson Ezekiel pamoja na mkandarasi Martin Abraham.
Aidha mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Isidori Kyando, alidai kuwa washtakiwa walifanya makosa hayo katika tarehe tofauti mwaka 2011.
Kyando alidai kuwa shitaka la kwanza ni la
matumizi mabaya ya madaraka, ambapo Desemba 2011, katika ofisi za Tanesco Ubungo, jijini Dar es Salaam washtakiwa kwa pamoja walimtumia madaraka yao vibaya kwa kufanikisha malipo kwa msambazaji M/S Young Doing Electronic Co Ltd , bila kuhakikisha kwamba mkandarasi anafika katika kituo cha mwisho kama ilivyokuwa katika makubaliano yao.
Hata hivyo, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa walifanya kosa hilo kinyume na kifungu namba 35 (21) cha sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 na kusababisha, Martin Abraham, kupata faida kutokana na ukandarasi huo.
Aidha katika shitaka la pili ni la kuisababishia serikali hasara linalowakabili washtakiwa Semtutu, Mahombo, Kisanga na Ezekiel ambao wanadaiwa kwamba kati ya Januari hadi Desemba 2011 katika ofisi za Tanesco Ubungo waliisababishia serikali hasara ya sh.275, 040,000 kutokana na matumizi yao mabaya ya madaraka.
Washtakiwa wote walikana kutenda kosa hilo ambapo upande wa mashitaka ulidai kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba kupangwa kwa tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.
Hakimu aliwaeleza washtakiwa hao kwamba dhamana yao iko wazi, ikiwa watajidhamini wenyewe kwa kuwasilisha mahakamani hapo fedha taslim sh.milioni 27.5 au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika, pia wawe na wadhamini wawili kila mmoja watakaoweka ahadi ya dhamana ya kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo wadhamini hao hawakutimiza masharti na wamerudishwa rumande hadi Aprili 30, mwaka huu kesi hiyo itakaposikilizwa tena.
Chanzo hapa>>FIKRA PEVU

No comments: