Advertisements

Wednesday, April 16, 2014

KIKAO CHA ISHIRINI NA TANO(25) CHA BODI YA TAIFA YA PAROLE CHAANZA LEO JIJINI ARUSHA

 Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo(kushoto) akiongoza kikao cha kujadili Wafungwa waliopendekezwa kuachiliwa kwa Parole(kulia) ni Kaimu Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa (kulia). Kikao hicho cha siku mbili kimeanza leo Aprili 16, 2014 katika Hoteli ya Charity iliyopo Jijini Arusha.
 Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Parole wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo(hayupo pichani) wakati akitoa hoja ya kufungua Kikao cha kupitia mapendekezo ya Wafungwa waliopendekezwa kuachiliwa kwa Parole( wa kwanza kulia) ni Bw. Francis Stolla akiwa na Wajumbe wenzake wakipitia makabrasha ya mapendekezo hayo.
 Wajumbe wa Sekretarieti ya Taifa ya Parole wakifuatilia majadiliano katika Kikao cha Bodi ya Taifa ya Parole(wa pili kulia) ni Mkuu wa Kitengo cha Parole, Makao Makuu ya Jeshi la Magereza  akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wakati majadiliano ya Wafungwa watakaoachiliwa kwa Parole(wa kwanza kulia) ni Mjumbe wa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Rose Odemba(wa pili kulia) ni Mrakibu wa Magereza, Lipinalyimo Lyimo.
 Wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Parole wakifuatilia kwa makini majadiliano ya Wafungwa watakaoachiliwa na Parole katika Kikao cha Bodi ya Taifa ya Parole kitakachofanyika kwa siku mbili kuanzia leo Aprili 16 - 17, 2014 katika Ukumbi wa Hoteli ya Charity, Jijini Arusha(wa kwanza kulia ni Mjumbe na Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Bw. Edgar Luoga(katikati) ni Mjumbe wa Bodi, Dkt. Joseph Chuwa toka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali(kushoto) ni Bw. Jonas Tarimo, Mjumbe wa Bodi ya Taifa ya Parole.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Mnuo(kushoto) akiteta jambo na Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(katikati) kabla ya kuanza rasmi Kikao cha Ishirini na Tano(25) cha Bodi ya Taifa ya Parole mapema leo Aprili 16, 2014. Kikao hicho kitafanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Hoteli ya Charity, Jijini Arusha(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Na; Inspketa Lucas Mboje, Arusha
Kikao cha Ishirini na Tano (25) cha Bodi ya Taifa ya Parole kitakachofanyika kwa siku mbili chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo kimeanza leo Aprili 16, 2014 katika Ukumbi wa Hoteli ya Charity iliyopo Jijini Arusha ambapo kikao hicho kitajadili Wafungwa waliopendekezwa na waliopendekezwa kuachiliwa kwa Parole.

Kufanyika kwa kikao hiki ni utekelezaji wa Sheria ya Parole ya Mwaka 1990 ambayo inalenga kupambana na uhalifu nchini na hivyo kudumisha Usalama wa jamii kwa ujumla.

Dhana hii ya Parole ambayo huishirikisha jamii katika kufanikisha Urekebishaji wa wale wanaopata msamaha wa Parole tayari imekwishatumika duniani kwa zaidi ya miaka 300 na imethibitika kwamba ni mfumo sahihi katika kuimarisha Urekebishaji wa Wahalifu na hivyo kuimarisha Usalama wa Jamii.

Ipo dhana kuwa kuanzishwa kwa mfumo huu hapa nchini Tanzania ni kuweka rehani dhamana Kuu ya kudumisha Usalama wa jamii. Ukweli ni kuwa Sheria hii ya Parole haipo ili kulegeza misingi ya Usalama wa raia.

Hivyo jamii yote kwa ujumla inapaswa kuielewa na kuikubali dhana hii ya Parole na kuachana na tabia ya mtindo wa kumpeleka kila mkosaji gerezani kwani tabia hii husababisha Magereza mengi kufurika na kuwa na msongamano usioruhusu utekelezaji wa programu za Urekebishaji, achilia mbali matatizo mengineyo mengi yatokanayo na hali ya Msongamano.

Kutokana na hali hii iliilazimu Jumuiya ya Kimataifa kupitisha suala zima la Adhabu mbadala wa kifungo kuwa ni miongoni mwa maadhimio mawili ambayo kimsingi yanahimiza matumizi ya adhabu mbadala wa kifungo kama njia ya kuwarekebisha Wahalifu wa kawaida na kuyaacha Magereza yatumike kwa Wahalifu wenye kutishia Usalama wa jamii.

Hiki ni kikao cha Nne kufanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo tangu ateuliwe rasmi na Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Taifa ya Parole kuanzia Aprili 24, 2013.

No comments: