ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 18, 2014

Kipa Simba afunguka kuhusu ushoga

Kipa wa zamani wa Simba, Andrew Ntalla.

Na Sweetbert Lukonge
WIKI iliyopita, kipa wa zamani wa Kagera Sugar na Simba, Andrew Ntalla alielezea mikasa aliyokutana nayo kwenye Klabu ya Simba, nyakati ngumu na ahadi hewa kutoka kwa viongozi waklabu hiyo likiwemo suala la kukosa mahali pa kuishi wakati aliahidiwa kupewa nyumba ya kuishi.
Endelea…
NILIPOTOKA kwenye ile gesti ya Manzese ambayo walikuwa wamenipangia kisha kuhamia katika nyumba moja ya mzee Kinesi ambayo ipo Magomeni Kagera ambayo wanaishi wachezaji wa Simba B, kama nilivyosema kuwa mambo yalikuwa yaleyale.

Furaha yote iliondoka kutokana na mazingira mabovu kama vile wadudu wengi kwenye vitanda, kwa ufupi ni kuwa haikuwa nyumba nzuri ya kuishi mchezaji wa klabu kubwa kama ya Simba ambayo ina historia kubwa zaidi katika soka la Tanzania.

Maana ile kambi ni kama vile kambi ya mende, kunguni na mbu, ni kama hakuna mtu anayeishi humo ndani, labda kama wawe wametengeneza sasa hivi, lakini uliza hata wachezaji wa Simba wanajua hilo.

Sisemi yote hayo kwa kuwa sipo Simba, asikwambie mtu kaka, kuna baadhi ya wachezaji hapo Simba wana mateso makubwa, utakuta katika mikataba yao imeandikwa kuwa watalipwa shilingi laki nane (800,000) kumbe za kwao hapo ni laki nne (400,000).

Fedha nyingine ni za watu ambao wanawafanya waendelee kuwa klabuni hapo.

Ndiyo maana unaweza kuona mchezaji kiwango chake ni cha chini na hana sifa ya kucheza ligi kuu lakini hafukuzwi, kumbe yupo hapo kwa maslahi ya watu fulani.

Tuachane na hayo, mateso yalinizidi nikawa sina tena amani kwa sababu ya mazingira hayo mabovu niliyokuwa naishi, amani nilikuwa naipata pindi tulipokuwa tunakwenda kupiga kambi Bamba Beach.

Lakini baada ya kurudi kutoka huko, mawazo yaliongezeka kwa sababu nilikuwa naingia tena katika mateso makubwa.

Kila nilipokuwa nikiwambia viongozi wangu waliitikia tu kuwa watanitafutia nyumba lakini baada ya hapo hakuna aliyenijali, kila mtu aliendelea na 50 zake.

Kusema kweli hali hiyo ilikuwa ikiniumiza zaidi kila nilipokuwa nikifikiria hali nzuri ya maisha niliyokuwa nayo kabla ya kujiunga na Simba.

Msongo huo wa mawazo (stress) niliokuwa nao ulisababisha hata kiwango changu cha kudaka kushuka sana kwa kuwa muda mwingi nilikuwa nafikiria hatima ya mateso yote yale.

Kuna wakati ilifikia kipindi nilitumia muda wangu mwingi kufikiria maisha yangu nikiwa langoni na siyo kuwaza nini kinaendelea kwenye mechi husika.

Mashabiki wakawa wananitukana na kunilaumu kila mara, siwalaumu kwa kuwa siyo makosa yao na hawakujua lolote lililokuwa likiendelea.

Nilipoona mambo yanazidi kuwa mabaya nilikata tamaa na kuacha kujituma tena mazoezini na hata katika mechi.

Nilifanya hivyo kwa sababu niliona kuwa sithaminiki tena katika klabu hiyo, wachezaji wa kigeni walipokuwa wanafika tu siku chache wanapitiwa nyumba, mimi nikiendelea kusota katika jumba hilo bovu.

Hata hivyo mambo yalivyozidi kuwa mabaya ilinibidi niondoke katika nyumba hiyo na kwenda kuishi na dada yangu huko Salasala.

Nilifanya hivyo baada ya kumsimulia kila kitu juu ya shida hizo nilizokuwa nazipata Simba, alinishauri na kuniambia kuwa kama itawezekana ni bora niachane na soka kwanza nifanye mambo yangu na baadaye ndipo nirudi kuendelea kucheza.

Nilifanya hivyo na sasa namshukuru Mungu nina kwangu naishi na mke wangu, pia nafanyabiashara zangu za kuuza nguo nazitoa Dar es Salaam na kwenda kuziuza Mbeya.

Lakini wakati huo natoa Mbeya nafaka na kuja kuuza Dar es Salaam, maisha yanaenda vizuri, mtoto wangu Frank ambaye yupo darasa la kwanza anaendelea vizuri.

Kuhusu ushoga
Tuhuma hizo siyo za kweli na sijawahi kabisa kufanya jambo kama hilo maishani mwangu, huyo kocha ambaye walikuwa wananihusisha naye hata mawasiliano yake sina.

Siyo kwa sasa tu hata wakati nilipokuwa Simba sikuwa nayo, tulikuwa tunakutana mazoezi tu baada ya hapo kila mtu aliendelea na mambo yake.

Hata mimi nilikuwa nasikia tu watu wakimtuhumu kocha huyo kuwa anajihusisha na mapenzi ya jinsi moja lakini siyo kwangu mimi, kama alikuwa anafanya mchezo huo labda na wachezaji wengine.

Nakuhakikishia kwa mara nyingine tena kuwa mchezo huo sifanyi na wala sijawahi kufanya na waliokuwa wasema hayo sijui niliwakosea nini mpaka wakafikia hatua hiyo ya kunichafulia jina langu kwa kiasi kikubwa namna hiyo, Mungu yupo na atalipa.

Namshukuru Mungu kwa yote. Hakika uwepo wangu Simba umenifundisha mengi kuhusu maisha (Anainama na kufuta machozi).

1 comment:

Anonymous said...

watanganyika ni watu wenye roho mbaya sana popote pale walipo wanatabia za kuwachafulia wenzao lakini si kitu mungu yupo