Advertisements

Wednesday, April 23, 2014

MAKONDA AWAITA VIONGOZI WA UKAWA "WATOTO WA SHETANI"-AGOMA KUFUTA KAULI

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Paul Makonda, jana aligoma kufuta kauli yake baada ya kuwaita viongozi wakuu wawili wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwa ni watoto wa shetani.

Akichangia bungeni, Makonda alisema Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, Mwenyekiti mwenza , Profesa Ibrahim Lipumba na mjumbe wa Ukawa, Ismail Jussa ni watoto wa shetani.

Shetani alikuja duniani kuiharibu dunia na kuteketeza kila kilichostahili kuungana… Lakini Yesu alikuja kuponya na kurekebisha kile kilichopotea,” alisema na kuongeza:


“Bahati mbaya sana shetani ni baba wa uongo, watoto wake ni mheshimiwa Jussa, watoto wake ni mheshimiwa Mbowe, watoto wake ni mheshimiwa Lipumba…Hawa ni watoto wa shetani.” Makonda aliwataka vijana nchi nzima wasikubali kupoteza muda wake kuambatana na viongozi hao katika matembezi yao, badala yake wajikite katika kufanya kazi za kiuchumi na kujiingizia kipato. Hata hivyo, baada ya kauli hiyo, mjumbe mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, aliomba mwongozo wa Mwenyekiti akisema Makonda alikuwa ametumia lugha ya kuudhi na isiyofaa.

“Huwezi kumwita mwanadamu mwenzako shetani… Aombe radhi na aondoe kauli hiyo mara moja” alisema na kumlaumu Mwenyekiti, Samuel Sitta kwa kuruhusu hali hiyo.

Sitta alisema “Ni kweli haipendezi kuitwa shetani nitamuomba mheshimiwa Paul Makonda aliangalie katika mazingira yetu na aweze kuyafuta hayo maneno”.

Hata hivyo, Makonda alisisitiza kuwa hawezi kufuta kauli yake wala kuomba radhi kwa sababu alikuwa amenukuu Biblia inayosema shetani ni baba wa uongo.

Baada ya kauli hiyo, Sitta alimtaka mjumbe aliyeomba mwongozo kurudi kwenye kanuni ili suala hilo liweze kupelekwa kamati ya maadili kama atataka kufanya hivyo.

No comments: