ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 17, 2014

Mrema atetea serikali mbili

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Augustino Mrema (pichani), amesema mfumo ambao utaweza kuwasaidia na kuwavusha Watanzania ni muundo wa serikali mbili.

Kauli hiyo ya Mrema ambaye ni Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) na Mbunge wa Vunjo, ziliibua shangwe na vigerere kutoka upande wa wajumbe wanatetea serikali mbili.

“Mheshimiwa mwenyekiti, nimekuwa Afisa Usalama wa Taifa kwa miaka mingi katika nchi hii, nimefanya kazi karibu na Marehemu Edward Sokoine, kwa hiyo ninajua tunachokisema.

“Nimekuwa nikiwasikiliza watu hapa, naweza nikawapa mifano halisi kwamba mkataa pema pabaya panamuita…pia asiyejua kufa atazame kaburi,” alisema na kuongeza:

“Naona kuna mchezo unaofanyika hapa bungeni, tunatania nchi hii…tunatania usalama wa nchi yetu.”

Hata hivyo, Mrema alisema hali ya usalama nchini ni siyo nzuri kama baadhi ya watu wanavyofikiria.

“Tuangalie Kenya kinachotokea sasa hivi, Kenya imepakana na Somalia angalia Al-Qaeda, Somalia inafanya nini, Al-Shaabab inafanya nini na wamekuja Kenya mpaka Mombasa, wanalipua makanisa wanaua wakristo…usalama wa Kenya upo hatarini,” alisema Mrema.

“Angalia kinachotokea Zanzibar, kinaashiria mambo mabaya sana, msidhani yataishia hapo baharini hapo Magogoni yatakuja mpaka huku bara kwa hiyo hatutakuwa salama, leo Zanzibar mapadri wanauawa, wachungaji, wakristo wanauawa, makanisa yanachomwa moto,” alisema.

Alisema kwa usalama wa nchi ya Tanzania, serikali ambayo inaweza kuleta amani na utulivu kwa miaka yote ni muundo wa serikali mbili na wala si vinginevyo.
 
SOURCE: NIPASHE

No comments: