ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 25, 2014

MZEE MOYOWATAKA CCM WAJIPIME.

Mzee Hassan Nassor Moyo, akiwa katika moja ya mikutano yake na vyombo mbalimbali vya habari akizungumzia mustakbali wa ZanzibarDodoma. Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Mzee Hassan Nassor Moyo amesema wajumbe wa CCM ndani ya Bunge la Katiba wanatakiwa kujiuliza sababu zilizolifanya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutoka nje ya Bunge na ndipo watafute suluhu.Akizungumza na Mwananchi kwa simu kutoka Zanzibar, Moyo alisema haitoshi kwa wajumbe wa CCM na wale wa kundi la 201, kuendelea na mijadala bila kukaa chini na kutafakari kwa nini Ukawa wametoka na hatima yake ni nini ndipo wajisahihishe.

“Hii hali ya mgawanyiko si nzuri hata kidogo. Kinachoendelea hakileti mantiki kwani kutengeneza Katiba ni kwamba, kila jambo linafanyika kwa maridhiano. Sasa hawa wako ndani hawa wako nje, ina maana wanataka kutupa Katiba yenye mpasuko?” alihoji Mzee Moyo.Alisema kuwa kutoka nje ya mkutano wowote si jambo geni, kwamba ikiwa upande mmoja utaona mambo hayaendi inavyotakiwa, unatoka kwa sababu hakuna kinachokufanya uendelee kukaa.

“Haya mambo hayakuanza leo, hata wakati nikiwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria Zanzibar, katika mikutano ya pamoja na Hizbu, ZNP, ZPP na ASP wajumbe wa ASP waliwahi kutoka nje kwa kupinga mwenendo wa mkutano.“Katika mkutano lazima watu waelewane, wakae mstari mmoja ndipo mambo yaende. Siasa ni mapambano na hakuna kuogopa. Lazima kusimamia pale mtu anapopaamini na kutambua mambo yanavyoendeshwa ama ndani au nje ya mstari,” alisema.Hata hivyo, Mzee Moyo alielezea kuchukizwa na mipasho, kejeli, kebehi na vijembe ndani ya chombo hicho muhimu cha kutengeneza Katiba ya Tanzania.“Hawa wamepewa jukumu la kutengeneza katiba, lakini inasikitisha wanatuletea mambo yao hapa. Wanapashana, matusi, kejeli kwani hayo ndiyo tuliyowatuma? Pale tumewapa kazi ya kututengenezea Katiba ya Watanzania kwa maendeleo ya Tanzania, kwa kweli imenisikitisha sana,” alisema.Kwa upande mwingine, alimshutumu mjumbe wa Bunge hilo, Mohamed Seif Khatib kwa kutumia muda mwingi kumshambulia, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Shariff Hamad badala ya kujadili kilichompeleka bungeni.“Badala ya kuchangia yake anamjadili Maalim Seif, inamhusu nini? Ya nini hayo wakati mambo yalishapita. Kwa kweli imenikera hasa kwa mtu mzima kama yule kujadili ya kale. Pale tunataka Katiba, azungumze yanayotokana na mkutano ule,” alisema.Juzi wakati akiwasilisha hoja zake, Khatib alitumia muda mwingi kumshambulia Maalim Seif hasa katika utendaji wake hata kutimuliwa kwake katika chama na Serikali pamoja na watumishi wengine.“Tunataka yeye (Khatib) na hata wengine, wazungumze yanayohusu mkutano huo, lakini si ya Maalim Seif, si ya Aboud Jumbe hayana faida leo, hayo yameshapita. Sasa kama alikuwepo wakati huo na kilimuuma, si angemtetea Maalim Seif palepale kusema anaonewa.“Alikuwa na nafasi katika Serikali, alikuwa na uwezo wa kuwasilisha hoja za kumtetea, hakufanya hivyo, leo anakuja kutusimulia. Sasa tufanye nini, haina maana. Hayo yameshatokea, tuyaache yabaki kumbukumbu tu.“Hata mimi nilipokuwa Waziri wa Kilimo, kuna jambo lilitokea na Maalim akiwa Waziri Kiongozi alitaka kunishtaki, lakini imebaki historia. Ya nini kuweka nongwa leo bado niko naye na tunafanya kazi. Khatib ameonyesha upungufu wake, haina maana hata kidogo. Azungumzie yaliyompeleka pale,” alisema Mzee Moyo.

Chanzo: Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Chakushangaza nikuwa, linapokuja swala la namna ya muungano & serikali ngapi zinatufaa, limekuwa la ushabiki km wa mpira.Hakuna anaetoa maelezo ya kina ni jinsi gani I.e serikali 2 au 3 zinavyoweza kutatua matatizo ya muungano na kuleta maendeleo.Kinachoendelea ni mipasho bila hoja nzito.

Anonymous said...

Mzee moyo ameongea jambo la maana sana , linalo sumbua wazanzibar na watanzania kwa ujumla , ukiangalia wakina nahodha, raza, khatibu na wengine walivyokuwa wanaongea kwenye vikao zanzibar na walivyofika dodoma ni vitu tafauti kabisa.. Inasikitisha kweli..