Advertisements

Monday, April 21, 2014

NJIA YA MKATO KATIKA MAISHA INAUA, WASANII TAFUTENI TAARIFA


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

MRISHO Mpoto `Mjomba` amewaonya vijana wanaopenda njia za mkato katika kusaka mafanikio.

Mpoto ameueleza mtandao huu kuwa mafanikio yana njia zake, hivyo lazima vijana wakubali kujituma zaidi katika kazi zao ili kutimiza ndoto zao na si kufikiria kufanikiwa kwa muda mfupi.
“Mjomba njia za mkato ni hatari. Vijana hasa wanasanii wenzangu wasipende njia za mkato. Lazima wafanye kazi na kuwa na subira ili wakati wao ufike”. Alisema Mpoto.
Mjomba aliongeza kuwa vitendo vya wasanii vijana kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na matendo mengine ya uovu wanaufanya muziki uonekane wa wahuni tu.

“Kijana unawekwa dawa tumboni sijui kwenda China na kwingineko. Mimi nadhani ni kuwa na haraka ya maisha”.

“ Tuacheni njia za mkato, twendeni njia ndefu tutafika tu japokuwa tutaona kama tunachelewa”. Alisema Mpoto.

Akiwazungumzia watu maarufu wakiwemo wanasiasa na wafanya biashara wakubwa kuwatumia vijana katika biashara haramu ya dawa za kulevya Mpoto alisema:

“Hawa jamaa Mjomba hawafai kabisa, Sijui tuwape jina gani. Nikisema ni wanyama, naona halina uzito. Ngoja niwatafutie jina lao mjomba”.

Aidha, Mpoto alisema wasanii wanatakiwa kujenga utaratibu wa kusoma vitabu ili wawe na ufahamu wa kutunga mashairi.

“Wasanii wengi Mjomba hawasomi. Wanakosa taarifa na ndio maana kila mtu anaimba mapenzi”.

“ Hivi kweli Mjomba kuna suala la mapenzi tu? Hapana! Yapo mengi ya kuimba, lakini vijana hawana taarifa mjomba”. Alisema Mpoto.

Pia aliawaasa vijana kuwa na utamaduni wa kupenda vitu vyao na kuachana na kuiga mambo ya kigeni.

“Nasema mjomba tena na tena, utandawazi umetufanya tuwe watumwa.”.

“Angalia vijana wetu wanavyovaa mjomba! Ni aibu kubwa”.

“Mjomba hivi kweli usanii lazima uvae vimini, milegezo?, hapana mjomba, turudi katika tamaduni zetu”

“ Sisemi wasivae nguo za kisasa, lakini nadhani wanatakiwa kukumbuka maadili yetu”

Akizungumzia wimbo wake wa `Waite`, Mjomba alisema ameamua kuuweka katika hali nzuri kifani na maudhui.

“Watu wengi walikuwa wananilaumu, ooh! Mjomba nyimbo zako unajikita zaidi kwenye maudhui zaidi ya fani”.

“Sasa nikaona ni vyema kuja kivingine. Ukisikia mdundo wa Waite, hakika mjomba naupenda sana”.

“Lakini nilivyoona mdundo ni wa nguvu, nami nikaingia ,..nikaingia Mjomba ..nikasema Waite wakalishe mjomba..hahahahahah”. Alisema Mpoto na kucheka.

Mrisho Mpoto alizaliwa tarehe 27 Oktoba 1978 huko Songea mkoani Ruvuma.

Ni msanii wa muziki wa dansi, filamu, mwongozaji, ngonjela,mshairi, na sanaa ya ngoma kutoka hapa nchini.

Mjomba ameimba nyimbo mbalimbali kama vile Salam Zangu Mjomba, Nikipata Nauli aliyoimba na Banana Zorro na sasa anatamba na kibao cha Waite.

Mjomba ni mmoja kati ya waanzilishi wa kundi la muziki la Parapanda.
Credit:ShaffihDauda

No comments: