ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 1, 2014

Pluijm awapigia saluti Mgambo

Kocha Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Mholanzi Hans van der Pluijm, ameipigia saluti JKT Mgambo baada ya kukiri kuwa kikosi chake kilistahili kichapo kutoka kwa 'wajeda' hao katika mechi yao iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa.

Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa 'maafande' hao na kuifanya Azam ya jijini Dar es Salaam pamoja na Mbeya City ya Mbeya kuendelea kuwaweka kwenye wakati mgumu wa kutetea ubingwa huo.

Akizungumza na gazeti hili juzi baada ya mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wachache tofauti na msimu uliopita, Pluijm alisema timu yake ilicheza chini ya kiwango na ilikosa nidhamu ya mchezo jambo ambalo lilichangia kushindwa kuibuka na ushindi.

Pluijm alisema haistahili kumlaumu mchezaji mmoja mmoja kwani timu nzima ilicheza chini ya kiwango na kwamba ameshangaa kuona wachezaji wake walikuwa wakicheza mipira mirefu ya juu kila mara, hivyo kupoteza nafasi ya kutawala mchezo huo uliokuwa muhimu kwao kushinda.

Alisema wachezaji wake walicheza tofauti huku wakiwafuata wapinzani wao JKT Mgambo ambao hawakuwa na mfumo maalumu na kuwaweka katika mazingira magumu ya kurudisha bao la mapema ambalo walilipata dakika ya kwanza na kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa nyuma kwa bao 1-0.

"Kiufundi timu yangu haikuwa na nidhamu, haikucheza kama tulivyotarajia, niliwaandaa vingine na wao wamecheza vingine si suala la mchezaji mmoja mmoja, nasema ni timu nzima nilikuwa siielewi," alisema kocha huyo.

Aliongeza kwamba pamoja na matokeo hayo bado hajakata tamaa ya kutetea ubingwa huo kwa kueleza kuwa watapambana hadi dakika ya mwisho.

"Tulijiandaa kushinda lakini hali imekuwa tofauti na matarajio, tutajiandaa pia kushinda katika mechi ijayo na tunaamini ushindi utapatikana, mechi ni ngumu," aliongeza.

Alisema ameshangaa kukiona Kikosi cha JKT Mgambo kikiwa tofauti na alivyokiona kwenye mechi zake nyingine zilizopita za ligi.

Naye nahodha wa Yanga, Nadir Haroub'Cannavaro', alisema matokeo hayo yamewasikitisha kwa sababu yanawapa Azam nafasi nzuri ya kuendelea kuongoza ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Aprili 19, mwaka huu.

Yanga iliondoka jijini hapa jana asubuhi na kurejea Dar es Salaam tayari kuanza maandalizi ya mechi yake inayofuata dhidi ya JKT Ruvu.

Baada ya mechi hiyo ya juzi, Yanga imefikisha pointi 46 na iko katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo wakati vinara Azam wana pointi 53 na Mbeya City walio nafasi ya tatu wana pointi 45.
CHANZO: NIPASHE

No comments: