ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 29, 2014

SALA KWA WATANZANIA YAFANYWA WESTMINSTER ABBEY, LONDON

 Balozi Peter Kallaghe, akitoka kanisa maarufu la Westminster Abbey, alipohudhuria misa ya kuiombea Tanzania katika maadhimisho ya miaka ya muungano 50 Alhamisi jioni. Kati kati ni Trevor Francis wa jumuiya ya Uingereza na Tanzania (British Tanzania Society). 



Picha na Rashid Dilunga 

Balozi Peter Kallaghe akisalimiana na Watanzania wa madhehebu ya Kibhora waliohudhuria misa iliyotayarishwa kila mwaka kwa mataifa yaliyo ya Jumuiya ya Madola, jengo la Westminster Abbey, London.

Picha na Rashid Dilunga..


Picha ya pamoja kwa baadhi ya washiriki wakiwa Balozi Mhe Peter Kallaghe 

Picha na Rashid Dilunga


Ratiba ya ibada. Picha na F Macha

Baadhi ya Watanzania waliohudhuria misa kanisa la Westminster Abbey. 
Picha na Rashid Dilunga




Westminster Abbey kwa nje . Ndani kamera haziruhusiwi. 
Picha na F Macha
Na Freddy Macha Alhamisi jioni, Wazalendo na marafiki zao walishiriki misa kuiombea Tanzania ndani ya kanisa mashuhuri la Westminster Abbey kuadhimisha miaka 50 ya muuungano. Misa hizi hutayarishwa kila mwaka kwa heshima ya nchi za Jumuiya ya Madola. Mgeni rasmi alikuwa Balozi wetu Uingereza Mheshimiwa Peter Kallaghe, maofisa ubalozini na wawakilishi wa Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (British-Tanzania Society). Kwaya ya Chuo cha Lancing, iliimba nyimbo za kizamani za Kizungu na Kikristo katika mahadhi yaliyorembwa na vinanda na maandiko matakatifu. Westminster Abbey iliyo eneo la majengo mahsusi ya kiserikali na saa maarufu - Big Ben, iliasisiwa mwaka 1245 na Mfalme Henry wa Tatu. Ni moja ya majumba yanayothaminiwa na kuheshimiwa sana tena sana Uingereza. Toka mwaka 1066 watawala wa kifalme, watu mashuhuri na muhimu nchini huzikwa ndani humo. 
Kati ya waliozikwa hapa ni William Shakespeare na Charles Dickens (waandishi mashuhuri) ;mmisionari aliyesafiri Afrika Mashariki na Kati karne 19, Dk. David Livingstone; wanasayansi Isaac Newton na Charles Darwin. Vile vile Waziri Mkuu Wiston Churchill aliyeongoza taifa hili wakati wa vita vikuu vya pili vya Wazungu (1939-45). Mwili wa Baba wa taifa Mwalimu Nyerere uliwekwa hapa kutazamwa na kadamnasi kabla ya kusafirishwa Tanzania, Oktoba 1999. Sala maalum kwa ajili ya marehemu Nelson Mandela ilifanywa Westminster mwezi Machi mwaka huu. Mbali na misa na mazishi -Westminster Abbey huwa ukumbi wa sherehe maalum. Mathalan miaka ya karibuni ndoa za mtoto wa Malkia Elisabeth (Prince Charles na Diana, 1981) na mjukuu William (2011) na Catherine, zilisheherekewa hapa. Akizungumza kwa Kiswahili na Kiingereza baada ya sala, Balozi Kallaghe aliwashukuru wote waliohudhuria. “Ni heshima iliyoonyeshwa na watu wa madhehebu mbalimbali kujumuika pamoja kuombea taifa letu na kumtakia kila Mtanzania mazuri,” alisema. Kati ya Watanzania niliozungumza nao ni Zarina na Zehra Jafferji wa dhehebu la Kibohra waliolitakia taifa letu mema na mfanyabiashara Abubakari Faraji na Mariam Kilumanga wa jumuiya ya wanawake London (TAWA). “Watanzania ni ndugu moja,” alisema Mariam Kilumanga. “Ndani ya familia yangu tunao watu wa dini kadhaa bila ubaguzi.” Mtanzania mshindi wa taji la Jumuiya ya Madola la Africa (Miss Commonwealth Africa 2013) Malkia Kassu, alisema ni kitendo cha amani kuwa ndani ya Westminster Abbey na ishara ya matumaini kwetu sote.

No comments: