Advertisements

Friday, April 25, 2014

SIRI MUHIMU KUZIJUA KUHUSU WANAWAKE!



UKWELI ambao haukwepeki kuhusu uhusiano na mapenzi ni uwepo wa furaha, amani na maelewano. Hivi ni vitu muhimu sana. Msingi wa yote ni pendo la dhati. Ikiwa wapendanao wana upendo wa kweli toka mioyoni mwao ni rahisi kutunza vitu hivyo.
Hakuna asiyependa kuwa na uhusiano wenye furaha na amani. Uhusiano wenye masikilizano huzaa matunda mema – kama ni marafiki tu, basi ujue ndoa inanukia lakini kama tayari ni wanandoa, maana yake mafanikio ndani ya nyumba yatakuwa rahisi kupatikana.
Marafiki katika yote hayo, inategemewa zaidi na namna wahusika wanavyoendesha uhusiano wao; kwa maana kwamba, yote yanahitaji ushirikiano wa wote. Hapo ndipo mwanzo wa matatizo. Wenzi wawili huwa na tofauti za hulka.

Kwa wanawake, wengi hupenda sana kufuatilia na kuhakikisha uhusiano unakuwa imara. Likitokea tatizo, mwanamke huwa mstari wa mbele kulishughulikia ili mambo yaishe. Wanawake wengi hawapendi kuwa wamewaudhi wenzi wao.
Ikitokea wakiona kuna tofauti ya kimawasiliano, mara moja husaka mbinu za kutatua na kubakisha uhusiano ukiwa kwenye hali nzuri. Hiyo ni tofauti na wanaume ambao mara nyingi wao ni watu wa harakaharaka.

Ni wepesi wa kusahau mambo au kuyachukulia kwa wepesi. Mfano, mwanamke wake akikasirishwa na jambo fulani, ni rahisi tu kuishia kusema: samahani. Wakati mwingine anaweza asiseme kabisa, akijua mambo yameshaisha. Wanawake ni tofauti. Wanafanya mambo yao kwa taratibu sana. Hasira zao zinachelewa kuisha, lakini ni rahisi zaidi kuzimaliza kwa kumwambia tu: nakupenda mpenzi, najua nimekosea, samahani mama.

Ni sentesi fupi sana lakini kwao ina maana na thamani kubwa sana. Mapenzi ni sawa na bustani, wakati mwingine inahitaji kumwagiliwa na kuwekewa mbolea. Kama ni kweli unampenda, tuliza akili na muda wako kuhakikisha furaha yake inaendelea kuwepo.

Inamaanisha kuwa, upendo wake kwako ukitamalaki muda wote – mafanikio ya kazi ya mikono yako yapo jirani tu. Mfanye mwanamke wako atabasamu. Pamoja na ubize wako, tenga nafasi kidogo kwa ajili yake.

MSAMAHA SI KUJISHUSHA!
Wanaume wengi wanaamini kumwambia mwanamke samahani ni kujishusha na kuwa chini yake, si hisia sahihi. Msamaha ni uungwana. Kama kweli unampenda kwa dhati, una shaka gani kumwambia akusamehe ili uhusiano uendelee kuwa wenye nguvu?

Hutapungua mahali popote kukubali kosa, ikiwa umekosea au kumrekebisha mwenzako badala ya kubaki bubu huku ukiwa umenuna na kusitisha baadhi ya huduma. Kama ilivyo kwako, tambua kuwa mwanamke naye ni binadamu, anaweza kufanya makosa lakini asijue!

Kumwambia kwa upole ni jambo zuri. Atakusikiliza, atakuelewa na atajirekebisha alipokosea. Kukaa nalo moyoni hakuna maana.

UBABE SIYO MPANGO
Wapo baadhi ya marafiki wanaamini kuwa ubabe ni sehemu ya ukamilifu wa uanaume. Siyo kweli. Huna sababu ya kuwa mkali sana au mwenye amri muda wote. Mwanamke anahitaji kubembelezwa, upendo na kuonyeshwa namna anavyothaminiwa.

Wengine wana tabia ya kuwapiga wenzi wao, kitu kidogo tu, tayari kipigo. Vipi akikutana na mkarimu, asiyepiga na anayebembeleza? Akiachana na wewe utamlaumu nani? Ni kweli kuna wakati mwanamke anahitajika kukaripiwa akikosea, lakini si sawa kuwa mkali kupitiliza wakati wote.
Wiki ijayo tutamalizia mada yetu, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
Credit:GPL

1 comment:

Anonymous said...

very nice nimeipenda hii ile mbaya na imekaa poa sana ahsante sana mwandishi nimepata darasa tayari hapa big up na dj luke na vijimambo team wote nakushukuruni jamani kwa kutupa habari njema nzuri moto moto kutoka nyumbani bila malipo mungu atakubarikini sana ahsanteni nyote jamani

mdau New York