ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 17, 2014

Slaa: CCM wanang`ang`ania Serikali mbili kuhofia kung`olewa 2015

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Silaa amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kinang'ang'ania kuendelea mfumo wa Serikali mbili kwa kuhofia kung'olewa na wananchi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini endapo wa Serikali tatu utapita.

Akihutubia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika mji wa Kibaigwa, Kongwa mkoani Dodoma na Gairo Morogoro, aliwataka wananchi waukatae mfumo huo wa Serikali mbili kwakuwa umeipotezea nchi dira na maendeleo na kuleta malalamiko kwa pande zote mbili za Muungano.

Slaa ambaye aliongozana na Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Masena Nyambage na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Shaweji Mketo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi nje ya Bunge (Ukawa), alisema kutokana na hali hiyo, CCM imelazimika kutumia nguvu kwa wajumbe wake wa Bunge la Katiba kuhakikisha wanapitisha mfumo wa Serikali mbili kwa kutumia hoja dhaifu ili kujiwekea mazingira mazuri ya kuendelea kuwapo madarakani licha ya wananchi kukichoka.

“Wananchi nyinyi ndiyo mliotoa maoni yenu kwa Jaji Warioba, iweje leo maoni yenu yaonekane hayana maana na CCM kulazimisha maoni ya wanachama wao, leo Jaji Warioba ndiyo anaonekana mbaya kwa kuwakilisha maoni yenu mnayotaka?

Msikubali nawaombeni tuunge mkono mfumo wa Serikali tatu ndio suluhisho la kuondoa kero za Muungano,” alisisitiza.

Kwa upande wake Nyambage alitaja baadhi ya ibara ikiwamo ya 37 inayotoa haki ya kumiliki mali ikiwamo ardhi na ibara ya 24 inayotoa uhuru wa mtu binafsi, akisema zinawasumbua watawala wakihofia kubanwa ubwanyenye walionao katika kudhurumu haki za Watanzania.

Naye Mketo wa CUF, alisema nchi imefikishwa kwenye ukosefu wa maadili, kukithiri rushwa na ubadhirifu wa mali za wanachi kutokana na kuondolewa kwa dira ya taifa kwa kusudi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: