Na Mwandishi Wetu
Katika kutekeleza Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu, Serikali itawazawadia
wanafunzi na shule zilizofanya vyema katika mitihani ya Elimu ya msingi
na Sekondari.
Hayo yamesemwa jijini Dar es
Salaam Jumatatu April 14, 2014 na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi, Dkt. Shukuru Kawambwa alipozungumzia na waandishi wa habari
kuhusu maandalizi ya Wiki ya Elimu.
Kwa mujibu wa Dkt. Kawambwa,
maadhimisho ya wiki hiyo ya Elimu itakayoanza Mei 3 hadi 9 mwaka huu ni
ya kwanza nchini na yanalenga katika kutambua juhudi za kuendeleza ubora
wa Elimu nchini.
“Pamoja na malengo mengine, wiki
hii italenga katika kutoa motisha na zawadi kwa shule na wanafunzi
waliofanya vizuri ikiwa ni utekelezaji wa wa Mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa,” alisema Waziri Kawambwa.
Miongoni mwa malengo ya BRN katika
kukuza ubora wa elimu nchini ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu na
wanafunzi wa shule zinazoonekana kuvuka viwango vya kukuza ubora.
Kwa mujibu wa Dkt. Kawambwa,
maadhimisho hayo yatakayofanyika mjini Dodoma yatazinduliwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda pia yatafungwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa Waziri Kawambwa, maadhimisho hayo yataanzia katika ngazi ya Wilaya, Mikoa na kasha kufanyika Kitaifa.
Alisema viongozi wote wa Mikoa na Wilaya wamekwishapewa taarifa ya kufanya maandalizi hayo ili kufanikisha sherehe hizo.
BRN ni Mpango wa utekelezaji wa
miradi mikubwa chini ya Ofisi ya Rais ukilenga kuhakikisha kuwa miradi
iliyopewa kipaumbele inapewa fedha za kutosha ili kupata maendeleo ya
haraka.
No comments:
Post a Comment