Advertisements

Saturday, April 19, 2014

UCHAMBUZI WA MECHI ZA KUFUNGA PAZIA LIGI KUU BARA HUU HAPA

IMG_8659
Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inafikia tamati leo (Aprili 19 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani, huku mabingwa wapya Azam fc wakikabidhiwa kombe lao Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu.
Mechi zote saba zitachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mtandao huu unajaribu kukupatia tathmini ya mechi zote saba zikazopigwa leo hii.

YANGA SC VS SIMBA SC
Mechi hii haina mchecheto sana kwasababu timu zote zimeshapoteza nafasi ya ubingwa, japokuwa lengo kubwa leo hii ni kutafuta heshima kwa klabu zote.
Simba wamefanya vibaya msimu huu na kuelekea kuishia nafasi ya nne ambayo inategemeana na matokeo watakayopata dhidi ya Yanga, wakati huo huo matokeo ya Kagera Sugar waliopo nyuma yao yakisubiriwa huko Mkwakwani.
Simba wamecheza mechi 25 na kujikusanyia pointi 37 katika nafasi ya nne, wakati Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 55 kwa kucheza mechi 25.
Endapo Yanga watashinda leo, basi watafikisha pointi 58, lakini hazitawasaidia kitu zaidi ya kulinda heshima,  kwasababu Azam fc walishazivuka na kuchukua taji msimu huu.
Kwa mazingira haya matokeo ya ushindi kwa timu yoyote hayatakuwa na maana hususani kwa Yanga, lakini angalau Simba yanaweza kuwahakikishia kushika nafasi ya nne.
Makocha wa timu hizi, Dravko  Logarusic ( Simba) na Hans Van der Pluijm ( Yanga) wanakutana kwa mara ya kwanza katika mechi ya watani wa jadi.
Lakini Loga aliwashawahi kuonja raha ya ushindi desemba 21 mwaka jana baada ya kuwafunga Yanga mabao 3-1 kwenye mechi ya `Nani Mtani Jembe`.
Pluijm leo ndio mara yake ya kwanza kukutana na presha ya mechi ya watani wa jadi.
Yanga na Simba zinakutana zikiwa na malengo yanayofanana, ingawa Simba wanakuwa kwenye presha kubwa zaidi.
Kama kweli wamedhamiria kupata nafasi ya nne, basi ni muhimu kushinda kwasababu wakifungwa wataipoteza endapo Kagera Sugar watashinda.
Kwa ujumla heshima ni muhimu sana na ndio maana timu hizi zilijificha kambini ambapo Simba walijichimbia Zanzibar na Yanga walikuwa Kunduchi jijini Dar es salaam.
Kwahiyo mechi hii itakuwa na ushindani mkubwa na timu yoyote inaweza kushinda.
JKT RUVU V AZAM FC  
Mechi hii itapigwa katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mechi hii itatumika kuwakabidhi Azam fc ubingwa wao wa kwanza waliofanikiwa kuutwaa.
Kwa mechi 25 walizocheza, Azam fc hawajafungwa hata mechi moja, na leo hii wanahitaji kushinda ili kuandika historia ya kubeba taji lao la kwanza bila kufungwa.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog amewataka wachezaji wake kucheza kwa kujituma ili kushinda mechi ya leo na kushangilia ubingwa kwa raha zote.
Baada ya mechi hii, Azam fc wameandaa sherehe za kushangilia ubingwa wao huko Chamazi, hivyo ushindi utanogesha zaidi.
Kwasababu hii ya Azam kutaka kuandika rekodi, mechi hii itakuwa ngumu kwa kocha wa JKT Ruvu, Fredy Minziro.
Hata hivyo kama Minziro atapoteza mechi hii haitakuwa na madhara kwake kwasababu poiniti 31 alizonazo sasa katika nafasi ya 10 zinamfanya awe mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kwa ujumla mechi itakuwa na mvuto kwasababu Azam fc wanahitaji kushinda.
TANZANIA PRISONS VS ASHANTI UNITED
Hii ni mechi ngumu mno na inahitaji maarifa makubwa kwa kocha wa Ashanti, Mzee Abdallah Kibadeni na David Mwamwaja wa Tanzania Prisons.
Kati ya timu hizi mbili, moja lazima iungane kushuka daraja na timu za JKT Oljoro ya Arusha na Rhino Rangers ya Tabora.
Timu zote zimecheza mechi 25 na kujikusanyia pointi 25. Kinachozitofautisha ni mabao ya kufunga na kufungwa.
Prisons wamecheza mechi 25 ambapo wameshinda mechi 5, sare 10 na kupoteza mechi 10.
Wajelajela hao wamefumania nyavu mara 25 na kufungwa mabao 33. Ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa unapata hasi (-8).
Ashanti United wameshinda mechi 6, sare 7 na kufungwa mechi 12.
Wamefunga mabao 20 na kufungwa mabao 38. Ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa anapata hasi kumi na nane (-18).
Kwa wastani huo wa mabao ya kufunga na kufungwa, Prisons wanakuwa juu ya Ashanti United.
Katika msimamo, Prisons wapo nafasi ya 11, huku nafasi ya 12 ikikaliwa na Ashanti United, lakini zimefungana pointi.
Kuelekea katika mechi hiyo, klabu zote zinahitaji ushindi, lakini Ashanti ndio wahitaji wakubwa zaidi kwasababu wamezidiwa mabao mengi ya kufunga na Prisons.
Endapo Ashanti United watashinda mechi hiyo watafikisha pointi 28 na kuvuka mkasi wa kushuka daraja, wakati Prisons watakuwa wameshashuka daraja.
Matokeo ya sare ya aina yoyote ile yatawashusha daraja Ashanti kwasababu ya wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kama Prisons watapata sare siku ya leo, watakuwa wamenusurika kushika daraja kwa faida ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Kitendawili cha timu gani inashuka baina ya Prisons na Ashanti United kitageguliwa kesho uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
MBEYA CITY FC VS MGAMBO JKT
Hii itakuwa mechi muhimu kwa kocha mkuu wa klabu hiyo ya Mbeya City fc,  Juma Mwambusi kutokana na matokeo aliyoyapata wiki iliyopita dhidi ya Azam fc ambapo alifungwa mabao 2-1 nyumbani na kuwapa ubingwa rasmi.
Endapo Mwambusi atashinda mechi hii, basi  itakuwa faraja kubwa kwake na kwa mashabiki wa klabu hiyo iliyoleta ushindani mkubwa mno msimu huu.
Mbeya City FC mpaka sasa wamecheza mechi 25 na kujikusanyia pointi 46 katika nafasi ya tatu ambayo tayari wamefanikiwa kuichukua.
Kwa upande wa Mgambo JKT, wanauchukulia mchezi huo kwa uzito wa hali ya juu ili kuweza kupata pointi tatu muhimu na kufikisha pointi 29.
Japokuwa maafande hawa wapo nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi 25 na kujikusanyia pointi 26 na kujiweka mazingira mazuri ya kubaki ligi kuu, lakini bado wanahitaji ushindi katika mechi ya leo.
Kwa mazingira haya, mechi hii itakuwa na mvuto mkubwa na soka la ushindani linatarajiwa.
COASTAL UNION VS KAGERA SUGAR
Katika mechi hii itakayopigwa uwanja wa Mkakwani, timu zote zinaingia kwa mitazamo tofauti.
Coastal Union hawana cha kupoteza, lakini  wakishinda wanaweza kusogea nafasi moja mbele kutegemeana na matokeo watakayopata Mtibwa Sugar leo hii.
Wagosi wa Kaya waliotabiriwa kufanya makubwa msimu huu wamedoda katika nafasi ya 9 kwa pointi 29 baada ya kucheza mechi 25.
Mtibwa wapo nafasi ya 8 kwa pointi 30, hivyo wakifungwa leo hii wataporomoka nafasi moja chini.
Kagera wao wanahitaji pointi tatu muhimu ili angalau kuambulia nafasi ya nne, lakini kama Simba watafungwa leo ndio itawasaidia.
Kagera wapo nafasi ya 5 kwa pointi 35 na kama watashinda watafikisha 38, na kama Simba wenye pointi 37 watafungwa, basi watachukua nafasi ya nne.
Kwa mazingira haya, Kagera Sugar watakuwa washindani wazuri leo hii na kuufanya mchezo uwe na mvuto.
RHINO RANGERS VS RUVU SHOOTING
Mechi hii haitegemewi kuwa ya ushindani hata kidogo kwasababu matokeo ya ushindi yatawasaidia Ruvu Shooting  kusogea nafasi ya juu kutoka ya 6 kwenda ya 5.
Ruvu Shooting wapo nafasi ya 6 katika msimamo wakiwa na pointi 35 swa na Kagera, lakini Wakata miwa wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kama Kagera na Simba zitafungwa leo, halafu Ruvu Shooting wakashinda, basi watafanikiwa kuchukua nafasi ya 4.
Rhino walishashuka daraja, hivyo hawana wanachokitafuta leo hii zaidi ya kukamilisha ratiba tu.
Kwa ujumla mechi hii itakuwa na presha kwa Ruvu Shooting kwasababu watakuwa wanahitaji matokeo mazuri huku wakiwaombea mabaya Simba na Kagera.
JKT OLJORO V MTIBWA SUGAR
Mechi hii haina jipya kwasababu Oljoro wameshashuka daraja msimu huu.
Mtibwa watahitaji ushindi ili kuendelea kukaa nafasi yao ya nane.
Kwa ujumla mechi hii haitakuwa na msisimko hata kidogo na mpira wa kawaidia unategemewa, japokuwa Mtibwa wanaweza kuingia kwa nguvu.
Mtandao huu utakuletea matokeo ya mechi zote hapo baadaye.

No comments: