ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 8, 2014

UNAKUBALIKA KWENYE JAMII-2

BADO tunaendelea na somo letu ambalo safari hii nagusia upande wa maisha. Ndugu zangu, kukubalika kwenye jamii kuna manufaa makubwa kama nilivyosema wiki iliyopita.
Niliishia pale nilipofafanua hasara za kutokubalika kwenye jamii. Sasa leo tuendelee.

KWA NINI HUKUBALIKI?
Wakati naanza kabisa kuandika mada hii, nimeeleza kwamba kila kinachotokea duniani huwa na sababu zake. Haiwezekani ukawa hukubaliki kwa chuki za watu au watu kukuonea wivu.
Lazima kuna sababu zinazosababisha usikubalike. Najua kila mmoja anaujua ukweli wa maisha yake ndani ya moyo wake.

Hapa nitakuandikia sababu muhimu zaidi ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kusababisha kutengwa na jamii na usikubalike, jambo ambalo athari zake nimeshazieleza hapo juu katika mada hii.

Hebu fuatilia kwa makini hapa chini halafu ujichunguze, wewe ukoje? Uko kwenye kundi gani? Ikumbukwe kwamba, si lazima kutengwa na kutokubalika na jamii nzima kwa sababu ya jambo moja. Inawezekana kabisa, una udhaifu katika eneo fulani, ndiyo maana baadhi ya aina fulani ya jamii inakuchukia. Twende tukaone...

FAMILIA
Kukubalika huanzia katika ngazi ya kwanza kabisa ya familia. Hapa namaanisha kuanzia mke, watoto, wazazi, ndugu na ukoo mzima kwa jumla. Hebu jiulize, hujawahi kukutana na mtu ambaye hakubaliki na jamaa zake? Hata katika vikao vya kujadili mambo mbalimbali ya familia, mchango wake wa mawazo hauthaminiwi.

Hapa inakwenda mbali zaidi, hata kama ana hoja za msingi, lakini kwa sababu ana dhambi ya kutokubalika, inakuwa si rahisi kupokelewa mawazo yake kwa urahisi.
Mtu ambaye anakubalika, mawazo yake hupewa kipaumbele, huonekana ana uwezo mzuri wa kufikiria na mwerevu.

NINI CHA KUFANYA?
Jenga utaratibu mzuri wa mawasiliano na ndugu zako. Waheshimu wakubwa kwa wadogo. Kuwa na lugha nzuri ya kuwasiliana.

Achana na maneno makali hata kwa wale ambao wapo chini yako kiumri. Kamwe usiwe mtu wa kulaumu bila sababu za msingi.

Ishi katika misingi ya kufundisha zaidi wenzako kuliko kujiona upo sawasawa kwa kila idara na kwamba hupaswi kufundishwa, badala yake wewe ndiye mwenye mamlaka juu ya wenzako.
Heshimu wazazi wako, wawe mwongozo wako kwa kila kitu. Jenga tabia ya kuwasaidia wanapokuwa na matatizo, dumisha mawasiliano ya kudumu na wazazi, ndugu na wengine wote wa ukoo wako.

Hii itakufanya uonekane ni binadamu unayejitambua na mwenye heshima, unayejali ndugu zako. Ishi nao kama jamii moja, ukielekezwa jambo fulani na wenzako kubali badala ya kuwa mbishi pasi kuwa na sababu za msingi.

Shiriki nao katika matatizo ya ugonjwa, kufiwa, sherehe n.k. Mathalani kama ukoo mmeamua kuchangishana kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kumsaidia mwenzenu, usikwamishe bali kama huna uwezo, toa taarifa katika njia sahihi na si kukatisha tamaa wengine.

Kumbuka ndugu zako wa damu na wa ukoo ndiyo wa kwanza kukusaidia matatizo yatakapokukuta. Ndiyo mwanzo wa cheni ya kuelekea kwenye kukubalika na wengi zaidi.

Tafuta kukubalika katika familia yako. Inatakiwa ifikie hatua, kama kuna jambo linatakiwa kufanyika, kama usipotokea wenzako wawe na hofu ya ubora wa jambo husika kwa kukosekana kwako.
Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

GPL

No comments: